Friday, December 15, 2017

WATOTO 82 WENYE MATATIZO YA MOYO YA KUZALIWA NAYO WAFANYIWA UPASUAJI WA KUFUNGUA NA BILA KUFUNGUA KIFUA KATIKA KAMBI MAALUM YA MATIBABU

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na mradi wa Little Hearts wa nchini Saudi Arabia ambao ni moja ya mradi wa Afya ulioko ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao Makuu yake mjini London nchini Uingereza zimefanya uchunguzi kwa watoto 131.

Uchunguzi huo umefanyika katika kambi maalum ya siku sita ya matibabu ya moyo kwa watoto wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi miaka kumi na nne ilianza tarehe 10/12/2017 na kumalizika leo tarehe 15/12/2017.

Kati ya watoto waliofanyiwa uchunguzi watoto 54 wamefanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na 28 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na hali zao zinaendelea vizuri. Kupitia kipimo cha kuangalia mtoto aliyepo tumboni kama anatatizo la moyo au (Fetal Echocardiography) tulimpima mama mwenye ujauzito wa miezi minne na kugundua kuwa mishipa ya damu ya mtoto imepishana. Mama huyu yuko chini ya uangalizi wetu hadi pale atakapojifungua.

Watoto waliofanyiwa uchunguzi na kufanyiwa upasuaji ni wale wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo. Mioyo ya watoto hao ina matundu na mishipa ya damu ya moyo haipitishi damu vizuri.Changamoto kubwa tuliyokabiliana nazo katika kambi hii ni upatikanaji wa damu na ufinyu wa chumba cha uangalizi maalum (ICU) kwa wagonjwa ambao wanatoka katika chumba cha upasuaji.

Tunawaomba wananchi waendelee kujitokeza kwa wingi kuchangia damu. Mgonjwa anayefanyiwa upasuaji wa moyo anatumia kati ya chupa sita hadi saba za damu. Hivyo mahitaji ya damu ni makubwa kwa mgonjwa anayefanyiwa upasuaji wa Moyo.

Kwa upande wa wazazi na walezi wasisahau kupima afya za watoto wao pale watakapoona kuna hali ya tofauti katika ukuaji wa mtoto kwani magonjwa mengi ya moyo yanaanzia utotoni. Mtoto akianza kuuguwa magonjwa ya moyo wazazi wengi wanadhani ni matatizo ya kifua baada ya kumfikisha Hospitali na kufanyiwa vipimo ndipo inagundulika mtoto anasumbuliwa na magonjwa ya moyo.Kwa wamama wajawazito wafanye uchunguzi (Fetal Echocardiography) wa kuangalia kama mtoto aliyeko tumboni anamatatizo ya moyo.

Tunawashauri watu wazima kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara hii itawasaidia kujuwa kama wana matatizo ya moyo au la na hivyo kupata tiba kwa wakati. Changamoto kubwa tunayokabiliana nayo katika matibabu ya wagonjwa wetu ni wagonjwa wengi tunaowapokea mioyo yao kutokuwa katika hali nzuri.

Taasisi inawashukuru sana wenzetu hawa wa Taasisi ya Msaada ya Muntada katika mradi wake wa afya wa Little Hearts kupitia Taasisi ya Kiislamu ya DHI NUREIN yenye makao yake Makuu mkoani Iringa kwa kutuwezesha kutoa huduma ya matibabu kwa watoto wetu. Hii ni mara ya nne kwa wenzetu hawa kuja katika Taasisi yetu na kutoa huduma tangu mwaka 2015 tulipoanza kufanya matibabu ya pamoja kwa watoto.

Kwa mwaka huu wa 2017 hii ni kambi ya 15 na ni ya mwisho kufanyika. Tumefanya matibabu ya pamoja na washirika wetu kutoka mabara ya Asia, Australia, Ulaya na Amerika. Katika kambi zote hizo kambi za watoto ni tano na kambi za watu wazima ni 10. Jumla ya wagonjwa 120 walifanyiwa upasuaji wa kufungua kifua kati ya hao watoto ni 80 na watu wazima ni 40.

Aidha wagonjwa 169 walifanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab. Kati ya hawa watoto ni 93 na watu wazima 76.

Kwa wagonjwa wote hawa 289 kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na bila kufungua kifua hapa nchini Taasisi imeweza kuokoa zaidi ya bilioni 7 (Tshs. 7,225,000,000/=) ambazo Serikali ingezilipa kama wagonjwa hawa wangetibiwa nje ya nchi. Gharama za mgonjwa mmoja anayetibiwa nje ya nchi ugonjwa wa moyo ni zaidi ya milioni 25.

Kwa namna ya kipeke tunaishukuru sana Serikali kwa kuhakikisha tunafanya kambi maalum za matibabu ya moyo katika Taasisi yetu na hivyo wagonjwa kupata huduma za matibabu kwa wingi. Licha ya wagonjwa kupata matibabu wataalam wetu wa afya wamekuwa wakijifunza mambo mbalimbali katika kambi hizi hii ikiwa ni pamoja na kubadilishana ujuzi wa kazi.

No comments: