Saturday, December 9, 2017

WALIOVUNJIWA VIBANDA KWENYE HIFADHI YA RELI DODOMA WAPATIWA ENEO NA MANISPAA


NA RAMADHANI JUMA.OFISI YA MKURUGENZI
MANISPAA YA DODOMA

HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma inatarajia kuwapatia eneo wafanyabiashara zaidi ya 550 waliovunjiwa vibanda vyao na kampuni hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) katika stendi ya mabasi madogo ya Jamatini ili kupisha utekelezaji wa mradi wa Reli ya kisasa, ili waendelee kufanya biashara zao kama kawaida.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa, Manispaa iko katika hatua za mwisho kuandaa eneo la Makole D-Center kwa kuweka miundombinu muhimu ikiwemo mfumo wa maji safi na maji taka ili wafanyabiashara hao waanze kufanya shughuli zao mara moja na katika mazingira rafiki na salama katika eneo hilo.

Aliyasema hayo alipotembelea eneo la Jamatini na Stendi Kuu Novemba 6 mwaka huu, akiambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Ajira Anthony Mavunde ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma, pamoja na Naibu Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Jumanne Ngede kwa lengo la kuwapa pole wafanyabiashara hao na kuwajulisha hatua zilizochukuliwa na Viongozi mbalimbali katika kuhakikisha tatizo linalowakabili linapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Aliwatoa hofu ya kuwa eneo hilo halitakuwa na wateja wengi kama ilivyokuwa eneo la stendi ya Jamatini, ambapo aliwaambia tayari Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Daktari Binilith Mahenge ametoa maelekezo kwa Manispaa na Sumatra kuhakikisha daladala zinakuwa na ruti inayopita katika eneo hilo jipya la biashara ambapo abiria watakuwa na kituo cha kupanda na kushuka na hivyo kuongeza mzunguko wa wateja katika eneo hilo, na kwamba utekelezaji wa maelekezo hayo umeshaanza kufanyiwa kazi na Sumatra.

Akizungumza na wafanyabiashara ya usafiri wa mabasi katika Stendi Kuu ya mabasi ya mikoani, Mkurugenzi Kunambi aliwaambia kuwa, Manispaa kwa kushauriana na uongozi wa Mkoa na wadau kama Sumatra imepanga kuhamishia Stendi hiyo katika eneo la Chaduru au kwenye eneo la viwanja vya Nanenane vilivyopo Kata ya Nzuguni barabara kuu ya Dodoma-Dar es Salaam.

Alisema Manispaa itazungumza na uongozi wa wasafirishaji ili kupata mapendekezo yao juu ya eneo rafiki zaidi miongoni mwa maeneo hayo mawili.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mavunde aliwataka wote walioathiriwa na zoezi hilo la bomoabomoa wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati Mamlaka na Viongozi wakifanya juhudi za makusudi kuwatafutia maeneo rafiki kwa shughuli zao huku Naibu Meya Ngede akiwahakikishia kuwa Baraza la Madiwani litasimamia kikamilifu suala la upatikaaji wa maeneo hayo.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde (wa pili kushoto) akizungumza katika mkutano na Wafanyabiashara wa eneo la Jamatini Manispaa ya Dodoma baada ya Vibanda vyao kubomolewa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) kupisha mradi wa ujenzi wa Reli kisasa. Kulia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi. Kushoto ni Katibu wa Wafanyabiashara hao John Banda. 
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi (wa pili kushoto) akiteta jambo na wafanyabiashara wakati akitoka katika eneo la Stendi ya Jamatini Mjini Dodoma baada ya kuzungumza na wafanyabiashara waliovunjiwa vibanda vyao kupisha mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa.
Baadhi ya wafanyabiashara wa eneo la Jamatini Manispaa ya Dodoma wakifuatilia mkutano wao na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Anthony Mavunde, Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma Jumanne Ngede na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Godwin Kunambi. PICHA NA RAMADHANI JUMA-OFISI YA MKURUGENZI

………..

No comments: