Sunday, December 17, 2017

UZIKWASA YAZIPA ZAWADI KAMATI ZA KUDHIBITI UKIMWI PANGANI


Mheshimiwa Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Hamidu Awesso akitoa ngao ya ushindi kwa mjumbe wa kamati ya kudhibiti Ukimwi, Jinsia na Uongozi ya kijiji cha Msaraza wakati wa tamasha hilo
Mheshimiwa Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Hamidu Awesso akitoa zawadi kwa kijana bora wa mfano wa kuigwa kwa mwaka 2017 nafasi ya kwanza ilichukuliwa na kijana Selemani Hamisi kutokea kijiji cha Kimang'a(Habari kwa Hisani ya Blog ya Kijamii ya Tanga Raha)
Mheshimiwa Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Jumaa Hamidu Awesso akitoa zawadi kwa mama bora wa mfano kwa mwaka 2017 ambapo nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Mama Hadija Mrisho wa kijiji cha Kwa-Kibuyu pichani
Hatimae shindano la kutafuta kamati bora za kudhibiti Ukimwi, Jinsia na Uongozi vijijini lililokuwa linaratibiwa na shirika la UZIKWASA wilayani Pangani limemaliza kwa kishindo huku kamati ya kijiji cha Msaraza kikiibuka na ushindi.


Shindano hilo ambalo lililokuwa linashirikisha vijiji 33 kutokea wiayani humo, limehudhuriwa na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji ambaye pia ni Mbunge wa jimbo hilo Mheshimiwa Jumaa Hamidu Awesso ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi.

Awali akitangaza kamati tatu bora zilizofanya vizuri kwa mwaka huu mbele ya mgeni rasmi, mkurugenzi msaidizi kutokea shirika la UZIKWASA Bwana Novatus Urassa alisema, mchakato wa kupata washindi hao ulikuwa mgumu kwa kuwa mwaka huu kamati zote zilionesha ushindani wa hali ya juu katika kutekeleza mipango kazi yao waliyojiwekea.

"Mheshimiwa mgeni rasmi, takribani vijiji vyote 33 vilivyoshiriki shindano hili kwa mwaka huu vilikuwa moto, kwa maana kila kijiji kilikuwa na mpango kazi wake, na kwa asilimia kubwa wote wamefanikiwa kutekeleza mipango kazi hiyo, lakini wapo waliotekeleza vizuri zaidi na tukaona hao ndio watakuwa mfano mzuri kwa wenzao, hivyo mpaka kupata kumia (10) bora haikuwa kazi rahisi, hivyo hivyo mpaka kupata hizi tatu (3) bora pia haikuwa rahisi" alisema Bwana Urassa.

Bwana Urassa alizitaja kamati hizo zilizofanya vizuri kuwa ni kamati ya kijiji cha Msaraza ambacho ndicho kiliibuka na ushindi na kukabidhiwa zawadi ya hundi ya shilingi laki saba, mshindi wa pili ni kijiji cha Mwera ambacho kilipewa hundi ya shilingi laki sita na mshindi wa tatu ni kijiji cha Mkwajuni ambapo walikabidhiwa hundi ya shilingi laki tano.

Kamati nyengine ambazo ziliingia katika hatua ya kumi bora ni pamoja na kamati ya kudhibiti Ukimwi, Jinsia na Uongozi ya kijiji cha Tungamaa ambacho kilishika nafasi ya nne, Kijiji cha Mwembeni nafasi ya tano, Kijiji cha Mbulizaga nafasi ya sita, Kijiji cha Kimang'a nafasi ya saba, Kijiji cha Mikocheni nafasi ya nane, Kijiji cha Mikinguni nafasi ya tisa, na Kijiji cha Kwa-Kibuyu kilishika nafasi ya kumi.

Mbali na ushindani wa kamati hizo, pia tamasha hilo liliwatambua na kuwazawadia washindi wa shindano la Kijana Bora wa mfano wa kuigwa pamoja na Mama Bora wa mfano wa kuigwa kwa mwaka 2017 kutokana na kujikita katika shughuli za kimaendeleo na kupambana na ukatili wa kijinsia.

Upande wa kijana bora wa mfano wa kuigwa kwa mwaka 2017 nafasi ya kwanza ilichukuliwa na kijana Hamisi Salemani kutokea kijiji cha Kimang'a, nafasi ya pili kijana Geofrey Kalala kutokea kijiji cha Boza, nafasi ya tatu kijana Mohammed Zuberi kutokea kijiji cha Mkwaja, na kwa upande wa mama bora wa mfano kwa mwaka 2017 nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Mama Hadija Mrisho wa kijiji cha Kwa-Kibuyu, nafasi ya pili Mama Pili Yusufu wa kijiji cha Mwembeni na nafasi ya tatu ni ilienda kwa Mama Halima Hamisi wa kijiji cha Mivumoni

Kwa upande wake mgeni rasmi Mheheshimiwa Jumaa Hamidu Awesso mbali na kulipongeza shirika la UZIKWASA kwa kuandaa shughuli hiyo, pia aliwapongeza washindi wote wa mashindano hayo na kuwataka waendelee kuwa chachu ya maendeleo wilayani Pangani hasa wakati huu ambao jamii imekuwa ikikumbwa na matukio ya ukatili wa kijinsia.

"Shirika la UZIKWASA linafanya mambo makubwa sana hapa wilayani Pangani, wananchi walikuwa wanaogopa kupaza sauti zao, lakini leo wananchi wanabanja, wanaeleza matatizo ya ukatili, wanajadili masuala ya maendeleo, wanawahoji viongozi wao wa vijiji kama kuna ubadhilifu, leo wananchi wanafatilia masuala ya elimu kwa watoto wao, kamati za shule zinafanya kazi, na pia tunaona hapa mpaka kamati za kudhibiti Ukimwi zimeanzishiwa mashindano ili kuleta ufanisi wa kazi zao, yote hii ni juhudi za UZIKWASA, na naomba washindi wote mkawe chachu ya maendeleo katika maeneo yenu" alisema Mheshimiwa Awesso.

Tamasha hilo lilihudhuriwa na Mkurugenzi wa halmashauri ya Pangani Bwana Sabas Damian Chambasi, mkuu wa TAKUKURU wilayani Pangani Bwana Joseph Paul, Ofisi ya manedeleo ya jamii Pangani ikiwakilishwa na Bi Vicky Mfinanga na Bi Rose Kaskazi pamoja na mkurugenzi mtendaji wa shirika la UZIKWASA Mama Vera Pieroth.

Pia Tamasha lilipambwa na burudani mbali mbali za sanii, ambapo kundi la maigizo na ngoma za asili kutokea Pangani linalofahamika kwa jina la Banja Basi lilikuwa kivutio kikubwa kwa wageni waalikwa, kadhalika wasanii wa Bongo Flava kutokea Pangani G-Man, Ram Bize pamoja Mavokali waliacha historia katika tamasha hilo.

Tamasha la kukabidhi zawadi kwa kamati bora za kudhibiti Ukwimwi, Jinsia na Uongozi kwa mwaka 2017 limeandaliwa na shirika la UZIKWASA lenye maskani yake wilayani Pangani huku likibeba kauli mbiu isemayo "Lisilowezekana, Linawezekana". Mwaka jana mshindi wa kamati bora kilikuwa kijiji cha Mseko.

No comments: