Kaimu Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kuzalisha Dawa ya Viuadudu vya Mbu waenezao Malaria Tanzania (TBPL), Mhandisi Aggrey Ndunguru (katikati) akitoa taarifa ya utekelezaji mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu baadhi ya Halmashauri zilizopatiwa dawa ya viuadudu vya mbu waenezao malaria, Wilayani Kibaha Mkoani Pwani 17 Desemba, 2017.
Mkuu wa Kitengo cha Mauzo na Masoko wa Kiwanda cha Kuzalisha Dawa ya Viuadudu vya Mbu waenezao Malaria Tanzania (TBPL), Bi. Upendo Ndunguru (kushoto) akifafanua masuala mbalimbali mbele ya Waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu mikakati wa kiwanda hicho katika kutafuta masoko ndani na nje ya nchi, Wilayani Kibaha Mkoani Pwani, 17 Desemba, 2017.(PICHA ZOTE NA MAELEZO)
Na Mwandishi Wetu, Kibaha-Pwani.
Kiwanda cha kuzalisha Dawa ya Viuadudu vya Mbu waenezao Malari Tanzania (TBPL) kimefanikiwa kusambaza dawa katika Halmashauri zaidi ya 174 nchini zenye viwango vikubwa vya malaria ikiwa ni sehemu ya mpango wa Serikali katika kupambana na ugonjwa wa malaria.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo Wilayani Kibaha Mkoani Pwani na Kaimu Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Mhandisi Aggrey Ndunguru, usambazaji wa dawa hizo umefuatia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati alipotembelea kiwanda hicho Juni 22 mwaka huu.
Akifafanua kuhusu agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mhandisi Ndunguru alisema kwamba, Rais alizitaka halmashauri zote nchini kununua dawa hizo kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kwasababu kiwanda hicho kimejengwa na Serikali kwa lengo la kupambana na ugonjwa wa malaria.
“Moja ya mambo ambayo Mhe. Rais alituagiza ni kuhakikisha kwamba kiwanda hiki kinatumika kutengeneza dawa za kuua mbu waenezao malaria na pia alituagiza kwamba halmashauri zote nchini zihakikishe zinanunua dawa hizi, na kwamba Serikali ilitenga shilingi bilioni 250 kwa ajili ya kununulia madawa mbalimbali nchini kwa mwaka huu wa fedha”, alisema Ndunguru.
Aliongeza kuwa, wakati wa ziara ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kiwanda hicho kilikuwa na akiba ya takribani lita 100,000 za viuadudu zenye thamani ya shilingi bilioni 1.3 ambazo zilikuwa hazijapata wateja, ndipo Rais akatoa agizo kuwa halmashauri zote nchini kufika kiwandani hapo na kuchukua viuadudu hivyo.
Alifafanua kuwa, kufuatia agizo hilo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilikishauri kiwanda hicho kuanza kusambaza viuadudu hivyo kwa kuanzia Mikoa 14 yenye halmashauri 96 kwa awamu ya kwanza ambayo ina kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria kisha mikoa 12 iliyobaki ifuatie baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza.
“Hadi kufikia sasa, kiwanda kimefanikiwa kusambaza viuadudu kwa halmashauri 174, halmashauri 96 kutoka katika mikoa 14 zilichukua viuadudu katika awamu ya kwanza na halmashauri 78 kutoka mikoa 12 zilichukua katika awamu ya pili, lakini hadi sasa zimebaki halmashauri nne tu ambazo bado hazijachukua”, alisema Ndunguru.
Aidha, aliongeza kuwa, hadi sasa kiwanda kina jumla ya lita 64,280 ambazo zipo katika ghala huku akifafanua kwamba, katika soko la Kimataifa kiwanda kimeuza dawa hizo kwa nchi ya Niger lita 90,371 na nchi nyingine kadhaa zimeonyesha nia ya kutaka kununua dawa hizo zikiwemo nchi za Angola ambayo imeonyesha nia ya kuhitaji lita 106,060 na nyingine yenye mahitaji ya dawa hizo ni Msumbiji.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa kiwanda hicho, Bi. Upendo Ndunguru ameeleza kwamba, moja mikakati wanayofanya katika matumizi ya dawa hizo ni uelimishaji kwa jamii ili kuhakikisha kwamba jamii inapata uelewa wa matumizi ya dawa hizo na kuzitumia kwa kuweka katika maeneo yenye mazalia ya mbu ili kuikinga jamii hususani akina mama wajawazito na watoto wadogo.
Kuhusu suala la upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi, alifafanua kwamba, wanaangalia sana soko la ndani ambalo kwa ukubwa wake limeongezeka baada ya agizo la Rais kutolewa mwezi Juni mwaka huu, huku akisisitiza kwamba jamii hainabudi kuzingatia suala la kutokomeza mbu kwa kutumia viuadudu hivyo.
No comments:
Post a Comment