Thursday, December 21, 2017

TANESCO "YALIA" NA WAHARIBIFU WA MAZINGIRA MITO INAYOLISHA BWAWA LA MTERA

 Taswira ya daraja la Mtera, ambalo pia hutumika kama milango ya kupitishia maji ya kusukuma mashine za kufua umeme. picha hii imepigwa Desemba 20, 2017.


NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, Mtera


UHARIBIFU wa mazingira unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu kwenye bwawa la Mtera sio tu unaathiri kiasi cha maji kwa matumizi ya Kituo cha kufua umeme cha Mtera bali pia unaathiri pakubwa kituo kingine cha kufua umeme cha Kidatu mkoani Morogoro, Mtaalamu wa Mazingira wa Shirika la Umeme nchini TANESCO, Bw. Yusuf Kamote amewaambia waandishi wa habari waliotembelea Kituo cha Kufua Umeme wa Maji cha Mtera, kilichoiko mpakani mwa mikoa ya Dodoma na Iringa.

Ukiachilia mbali mabadiliko ya tabia nchi, shughuli za kibinadamu kandokando ya mito, kunachafua mazingira ya mito hiyo na kupunguza kiasi cha maji na hivyo kuathiri uzalishaji umeme wa maji.

“Tatizo hili ni kubwa watu wanaingilia mito hii, kuna wakulima na wafugaji wanathiri sana, shughuli za kilimo na ufugaji zinaleta mchanga mwingi kwenye maji na hivyo kupunguza kina cha mto na maji yenyewe tunaita siltation, na hiyo ikitokea ujio wa maji kwenye mitambo unapungua na hivyo uzalishaji unapungua kama hivi sasa mnavyoona maji yamepungua.” Alisema.

Bw. Kamote aliwaasa wananchi kuacha kuaharibu mazingira kwani athari zake ni kubwa katika kuendesha mitambo ya kufua umeme ambao ni muhimu kwa uchumi wanchi.“Yawezekana wanafanya shughuli hizo kwa kutokujua athari zake katika uzalishaji umeme, kwa hivyo tunashauri wananchi waelewe kwamba hilo ni tatizo na waache.” Alisetoa rai Bw. Kamote.

Naye Kaimu Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme wa maji Mtera, Mhandisi David Myumbilwa, ambaye kitaaluma ni Mhandisi wa Ujenzi, alisema lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho mwaka 1988 lilikuwa ni kutunza maji kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kufua umeme wa maji kwenye kituo cha Kidatu mkoani Morogoro kabla ya kuongeza matumizi ya kituo hicho na kufanya kazi zote mbili kufua umeme na kutunza maji (water storage).

“Kidatu ndio kilikuwea kituo lengwa cha kufua umeme wa maji wakati huo, lakini baada ya wataalamu kuona maji yanayotumika kwa kazi hiyo ni kidogo ukilinganisha na mashine zilizokuwepo pale ikaonekana upo umuhimu wa kutengeneza storage ya maji hapa Mtera na bwawa hili ndio kubwa kabisa katika mabwawa ya kufua umeme wa maji nchini.” Alisema Mhandisi Myumbilwa.

Alisema, kiwango cha juu cha ujazo wa maji kwenye bwawa hilo ambao unahitajika kwa ajili ya kuendesha mitambo ni 698.5 m.s.a.l na kiwango cha chini ni 690 m.s.a.l, chini ya hapo kwa usalama wa mitambo lazima izimwe.Mhandisi Myumbilwa amesema, Bwawa hilo linategemea maji kutoka mito mitatu, Mto Kizigo unaotoka mkoani Singida, Ruaha Mkuu, na Ruaha ndogo.

“Mto Kizigo ni mto wa msimu wakati wa kiangazi unakauka, Ruaha ni mto asili na hapo nyuma ulikuwa na kiwango cha juu cha maji lakini hivi sasa maji hakuna kabisa, na huu ndio mto mkubwa unaotegemewa na Kituo cha Mtera.” Alifafanua.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bi. Leila Muhaji alisema lengo la ziara hiyo, ni kuweapa uelewa wahariri ili kujionea juhudi za TANESCO katika kuhakikisha vyanzo vya maji yanayozalisha umeme vinatunzwa kwani umeme wa maji ndio umeme nafuu zaidi.

“Mtakumbuka kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri katika kipindi cha tunatekeleza alisema baadhi ya mashine za kufua umeme wa maji zinatengenezwa na kama zinatengenezwa maana yake haitatoa umeme kwa kiwango chake cha kawaida.” Alisema.
Milango ya kuruhusu maji kupita kwenye Bwawa la Mtera.
Mtaalamu wa Mazingira wa Shirika la Umeme nchini TANESCO, Bw. Yusuf Kamote, akielezea jinsi mabadiliko ya tabia nchi na shughuli za kibinadamu zinavyoathiri bwawa la Mtera. Kushoto ni Mhandisi Myumbilwa
Daraja la Mtera, ambako pia ndiko iliko milango ya kupitishia maji ya kufua umeme
Kaimu Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme wa maji Mtera, Mhandisi David Myumbilwa, akielezea jinsi mashine za kufua umeme zinavyotegemea maji.
Wahariri na maafisa wa TANESCO, wakiwa kwenye eneo la Bwawa la Mtera, ambalo linategemewa kutoa maji ya kuzalisha umeme kwenye kituo cha Mtera na Kidatu mkoani Morogoro, na hii ndio hali halisi kama picha hii ilkiyopigwa Desemba 20, 2017 inavyoonyesha
Mhandisi Myumbilwa na baadhi ya wahariri
Mwendesha mitambo Mwandamizi kwenye Kituo cha kufua umeme wa maji cha Mtera, Mhandisi Asanterabi Naaman, akitolea ufafanuzi wa jinsi wanavyosimamia mitambo hiyo wakiwa shimoni, (mgodini), kwenye kituo hicho,
Wahariri wakiangalia jinsi moja kati ya mashine mbili za kufua umeme wa maji inavyofanya kazi
Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bi. Leila Muhaji, (kushoto), akiwa na wasimamizi wa chumba cha udhibiti mwenendo wa mitambio kilichoko chini ya ardhi kwenye kituo cha kufua umeme wa maji Mtera.
Mhariri wea Mwanancvhi, Bi. Lilian Timbuka.
Bi. Leila Muhaji, akiwapongeza wasimamizi wa chumba hicho
Fundi wa umeme mdogo, Elisha Kamenya akiwa kazini.

No comments: