Thursday, December 21, 2017

HOTUBA YA WAZIRI WA AFYA MHE.UMMY MWALIMU KATIKA HAFLA YA MAKABIDHIANO YA MAJENGO YA CHUO CHA UUGUZI MIREMBE YALIYOJENGWA KUPITIA UFADHILI WA MFUKO WA DUNIA WA KUPAMBANA NA UKIMWI KIFUA KIKUU NA MALARIA (GLOBAL FUND) TAREHE 20 DISEMBA 2017

  • Katibu Mkuu – Wizara ya Afya, Dkt. Mpoki Ulisubisya
  • Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
  • Mganga Mkuu wa Manispaa ya Dodoma,
  • Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mirembe na Taasisi ya Isanga
  • Mkurugenzi wa Hospitali kuu ya Benjamin Mkapa
  • Mkuu wa Gereza la Isanga
  • Mkuu wa Chuo cha Uuguzi Mirembe
  • Wakurugenzi na Watumishi wote wa Wizara ya Afya, Watumishi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
  • Mwakilishi wa Global Fund Nchini kutoka PwC,
  • Waandishi wa Habari,
  • Wageni Waalikwa,
  • Ndugu Wananchi,
  • Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote ninapenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha siku hii ya leo. Kwa namna ya pekee ninapenda kuwashukuru watekelezaji wa mradi huu wa ujenzi kwa kunialika katika hafla hii muhimu ya ufunguzi wa majengo yaliyojengwa na kukarabatiwa katika chuo hiki cha Uuguzi Mirembe. Vile vile, napenda kutoa shukrani za kipekee kwa kiongozi wangu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa kipaumbele kikubwa Sekta ya Afya za Watanzania. Pia, ninamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuipa sekta ya elimu fursa ya pekee katika kuhakikisha idadi ya wahitimu kutoka katika vyuo mbalimbali inaongezeka ili kufikia azma ya uchumi wa viwanda kama nguzo kuu ya maendeleo ya nchi yetu. Pamoja na yote hayo ninapenda kutoa pongezi za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza Bajeti ya Afya kutoka  asilimia 9.2 ya bajeti ya Serikali mwaka 2016/17 hadi asilimia 10 ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/2018 na kuifanya Sekta ya Afya kuwa miongoni mwa Sekta za Kipaumbele katika mgao wa Bajeti.
Ndugu Wananchi,
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye Sekta ya Afya yenye lengo la kuboresha huduma za afya na kuimarisha afya za wananchi. Aidha, Serikali imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutekeleza miradi hiyo ikiwemo miradi ya kuimarisha mifumo ya afya nchini. Mikakati na jitihada za makusudi zimeendelea kutekelezwa katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya hususan katika vituo vya kutolea huduma za afya na vyuo vya mafunzo vya wataalam wa afya nchini.
Ndugu Wananchi,
Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Afya nchini imeendelea kutekeleza afua mbalimbali zenye lengo la kuwajengea uwezo na taaluma katika rasilimali watu. Baadhi ya mafanikio ambayo Sekta ya Afya imeyapata katika eneo la rasilimali watu hadi kufikia mwaka 2016/17 ni pamoja na:
  • Kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watarajali (pre-service) wanaodahiliwa katika vyuo vya afya kutoka 3,025 mwaka 2007/2008 hadi kufikia 13,632 mwaka 2016/17. Ongezeko la wadahiliwa limetokana ukarabati na upanuzi katika vyuo vya Tukuyu, Kiomboi, Mbulu, Mirembe, Mbeya, Tarime na Kagemu kupitia bajeti ya Serikali pamoja na kufunguliwa kwa vyuo vya Nzega, Kibondo na Nachingwea ambavyo vilikuwa vimefungwa. Aidha, kupitia ufadhili wa Global Fund, ongezeko la wanafunzi limetokana na upanuzi wa vyuo vya Mtwara, Bagamoyo, Tanga, Njombe, St. Bakhita, Hubert Kairuki kupitia ufadhaili wa Global Fund.
  • Vilevile, udahili kwa wanafunzi wa uzamili umeongezaka kutoka 146 mwaka 2007/2008 hadi 404 mwaka 2016/2017. Ongezeko hili ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kupunguza uhaba wa wataalam wanaotoa huduma za kibingwa nchini.
  • Kuajiri Madaktari wapya 258 waliosambazwa katika Halmashauri mbalimbali nchini ili kuendelea kupunguza tatizo la watumishi wa afya nchini hasa maeneo ya vijijini
  • Kuajiri watumishi wa kada za afya 3,152 waliosambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini hasa maeneo ya vijijini. Aidha kwa mwaka wa fedha 2017/18 Serikali imetoa vibali vya ajira 3,152 ambapo watumishi hawa wamekwishaajiriwa na kupangwa kwenye vituo mbalimbali vya kutolea huduma za Afya hasa maeneo yenye upungufu wa watumishi wa Afya.
  • Kuwepo kwa wahitimu 4,352 wa kada ya wahudumu wa Afya ya Jamii (Community Health Workers) ambao wanatarajia kutoa huduma mbalimbali ikiwemo za kinga katika ngazi ya jamii.
Pamoja na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali pamoja na wadau wa Maendeleo ikiwemo Global Fund, Sekta ya afya bado inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi wa afya. Mwaka 2015, sekta ya afya ilikuwa inahitaji jumla ya watumishi 179,509 ambao wangetoa huduma za afya kwenye zahanati, vituo vya afya, hospitali za mikoa na wilaya pamoja na hospitali zote za rufaa nchini, watumishi waliopo ni 90,791 ambao ni 51% ya mahitaji yote, hivyo upungufu uliopo ni watumishi 88,718 sawa na (49%).
Ndugu Wananchi,
Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto itaendelea na jitihada zake za kuhakikisha kuwa huduma bora za afya zinapatikana kwa Watanzania wote ikiwa ni pamoja na kuboresha vyuo vya kutolea mafunzo ya kada za afya. Ninapenda nitambue mchango mkubwa uliotolewa na Mfuko wa Dunia (Global Fund) katika kuboresha vyuo vyetu na pia kuongeza wigo wa kudahili wanafunzi kwa kutoa udhamini katika kada mbalimbali. Natambua, pamoja na jitahada zinazofanywa na Wizara yangu, bado vyuo vyetu vingi vinakabiliwa na changamoto mbalimbali kama ifuatavyo;
  • Upungufu wa miundombinu ya kufundishia, vifaa, makazi ya watumishi na uchakavu mkubwa kwa majengo yaliyopo. Wizara inaendelea kutatua changamoto hii na tayari tumefanya ukaguzi wa vyuo vyote ili tuweze kuweka mipango ya namna ya kupunguza changamoto hii.
  • Upungufu wa watumishi wa afya katika vyuo vyetu vyote nchini ambao ambao sasa umefikia asilimia 51. Ninapenda kuwahakikishia kuwa, Serikali na wadau wake tunaendelea na jitihada za kuajiri watumishi zaidi katika vyuo vyetu ili kupunguza na kumaliza kabisa uhaba huu.
  • Suala la madeni kwa wazabuni ikiwemo deni la wazabuni wa Chuo cha Mirembe. Wizara imeshawasilisha madeni hayo kwa Mlipaji mkuu wa serikali. Aidha, Wizara inaendelea kufuatilia ulipwaji wa madeni hayo.
  • Suala la kutokamilika kwa jengo la utawala la kanda ya kati lililopo kwenye Chuo cha Uuguzi Mirembe. Wizara yangu inaendelea na jitihada za kutafuta fedha za kukamilisha ujenzi wa jengo hilo, baada ya wahisani waliokuwa wanafadhili ujenzi kusitisha msaada.
Niendelee kuwaomba ndugu zetu wa Mfuko wa Dunia kuendelea kutuunga mkono katika kutatua changamoto hizi. Mchango wenu tunauthamini na tutahakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kuitunza miundombinu hii.
Maelekezo yangu kwa Mkuu wa Chuo na Mkurugenzi wa Idara ya Mafunzo ni kuhakikisha kuwa fedha za matengenezo (maintenance) zinatengwa katika bajeti yetu ya Wizara ya kila mwaka ili kuhakikisha miundombinu hii inayokabidhiwa leo inaendelea kuwa bora kama ilivyo sasa.
Hitimisho:
Kabla sijamaliza hotuba yangu, ninapenda kuchukua fursa hii kuwahakikishia kuwa, dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa afya za Watanzania zinaboreshwa. Hivyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua za dhati ili kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya afya hususan uhaba wa watumishi, upungufu wa nyumba za watumishi wa afya hasa waliopo vijijini na kuboresha miundombinu ya vyuo vya kutolea mafunzo ya afya ili wataalamu watakaozalishwa wawe bora.
Baada ya kusema hayo, machache sasa niko tayari kwenda kufungua na kupokea majengo yaliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Funds).
Asanteni kwa kunisikiliza.

No comments: