Wednesday, December 13, 2017

PROF. MBARAWA ATAKA UJENZI RELI YA KISASA KUHARAKISHWA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa maelekezo kwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali ya Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa (kushoto), kuhusu kusimamia kwa karibu mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge), wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo katika kijiji cha Soga Mkoani Pwani na Ngerengere mkoani Morogoro.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akimsikiliza Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali ya Reli (RAHCO), Masanja Kadogosa (kulia), alipomweleza hatua za ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge), wakati Waziri huyo alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Mkoani Pwani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akichanganya zege katika moja ya Makalvati yanayojengwa katika mradi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge), katika eneo la Kisarawe alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Mkoani Pwani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), akibonyeza kitufe cha kuruhusu zege kwenda kwenye kalvati linalojengwa kwenye Reli ya Kisasa (Standard Gauge), wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo Mkoani Pwani.
Muonekano wa moja ya kalvati linalojengwa kwenye Reli ya Kisasa (Standard Gauge), katika eneo la Kisarawe Mkoani Pwani. Mradi huo unajengwa kwa awamu mbili ambapo sehemu ya kwanza inajengwa kutoka Dar es Salaaam mpaka Morogoro ambapo sehemu ya pili itajengwa kutokea Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma.
Mafundi wa Kampuni ya Yapi Merkezi wakiendelea na kazi ya kujaza zege kwenye moja ya kalvati linalojengwa kwenye Reli ya Kisasa (Standard Gauge), katika eneo la Kisarawe Mkoani Pwani.
Tingatinga likiendelea na kazi ya kuchenjua tabaka la chini la Reli ya Kisasa (Standard Gauge), katika eneo la Soga, Mkoani Pwani.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa wito kwa mkandarasi Yapi Merkezi na Motaengil Africa wanaojenga reli ya kisasa (Standard Gauge Railway), kufanya kazi kwa uadilifu, kulingana na vipimo vilivyo kwenye mkataba ili kuwezesha mradi huo kukamilika kwa wakati.

Aidha, ameitaka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za reli (RAHCO), kuhakikisha kuwa inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo kwani wananchi wamekuwa wakisubiri kukamilika kwake na kuanza kupata huduma za usafiri wa treni zitakazorahisisha shughuli zao za kibiashara na kijamii.

Akizungumza leo mara baada ya kukagua mradi huo katika kijiji cha Soga mkoani Pwani, Waziri Mbarawa amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya wakandarasi hao na kuagiza kuongeza spidi zaidi ili ifikapo mwaka 2020 mradi huo uwe umekamilika.“Kasi mnayoenda nayo sio mbaya, ila naomba RAHCO mhakikishe mnasimamia kwa karibu kuhakikisha spidi inaongezwa ili kazi ikamilishwe haraka na kwa viwango”, amesema Profesa Mbarawa.

Akiwa katika kijiji hicho, Waziri Mbarawa amemwagiza Kaimu Mtendaji Mkuu wa RAHCO, Masanja Kadogosa, kukutana na uongozi wa kampuni hizo kujadili na kuangalia fursa za upatikanaji wa ajira kwa watanzania hususan wakazi wa eneo inapopita reli hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa RAHCO, Masanja Kadogosa, amesema mpaka sasa mradi huo upo ndani ya muda na kumhakikishia Waziri Mbarawa kuwa mradi utakamilka kwa wakati kwani kazi inayofanyika sasa ni kuweka zege kwa ajili ya ujenzi wa boksi kalvati ambapo kazi hiyo inaendelea vizuri.

Ameongeza kuwa katika kipindi hiki mradi ulisuasua kutokana na changamoto za mvua za vuli, hivyo amefafanua kuwa wana mpango wa kuongeza kambi nyengine nane upande wa Soga na nane upande wa Ngerengere ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Mradi wa SGR unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza unahusisha ujenzi wa reli kutoka Dar es salaam – Morogoro na ya pili itahusisha sehemu ya Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma pamoja na njia za kupishana ambapo kwa pamoja itakuwa na urefu wa kilometa 722 na itajengwa kwa gharama ya shilingi Trilioni 7.1.

No comments: