Saturday, December 16, 2017

Mpango wa Malipo kwa Ufanisi waleta Mabadiliko Sekta ya Afya Rufiji


Na.WAMJW-Rufiji.

Utekelezaji wa mpango wa malipo kwa ufanisi(RBF) Wilayani Rufiji umeleta mabadiliko makubwa katika Vituo vya afya na Zahanati kwa uboreshaji wa miundombinu pamoja na upatikanaji wa dawa muhimu

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  wakati alipotembelea Kituo cha Afya cha Ikwiriri na Zahanati ya Nyamwage katika ziara yake ya kuangalia utekelezaji unaofanyika kupitia mpango wa malipo kwa ufanisi unaotekelezwa katika mikoa nane nchini

Waziri Ummy alisema mabadiliko hayo katika sekta ya afya yamefanyika katika maeneo ya utoaji huduma,Uongozi na Utawala,Rasilimali watu,Mifumo ya usimamizi wa utoaji taarifa za afya,madawa na teknolojia ya afya ambapo mfumo huo umesaidia maboresho, uwajibikaji,ufanisi na usawa kwani dhana hiyo inamfanya mtoa huduma kulipwa kulingana na matokeo ya kazi yake ambayo amehakikiwa na hivyo kufanya vituo hivyo kuongeza hali ya upatikanaji wa dawa na kuboresha miundombinu ya vituo hivyo

"Tumeanza mpango huu katika mikoa 8,tumefanya tathimini kwenye vituo vya afya na zahanati zote za Mkoa wa Pwani ikiwemo Wilaya ya Rufiji,tukabaini vituo vya afya na zahanati hazikuwa na viwango vya ubora unaotakiwa, tukaona tuwapatie  shilingi milioni 10 kila kituo vilivyokidhi kwa ajili ya kuboresha miundombinu"alisema Waziri ummy.

Hata hivvyo aliipongeza kamati ya afya ya kijiji cha Nyamwage kwa kutumia ipasavyo shilingi milioni 10 kwa kuongeza urefu wa paa na kupaua,kuweka malumaru na kuongeza matundu ya choo pamoja na tundu moja la choo kwa ajili ya walemavu"nikupongeze mganga mfawidhi kwa kuboresha zahanati hii kwakweli unapaswa kupongezwa kwani umefanya vizuri ila badilika lugha chafu kwa wananchi haitakiwi,nakupa mwezi mmoja ila kwa upande huu mwingine umenifurahisa,mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni"

Aidha ,alitoa wito kwa wanawake  kuhudhuria kliniki pale wanapohisi kuwa wajawazito na hasa mahudhurio yote manne ili kuweza kujua hali zao kiafya na kuweza kupata matibabu pale wanapogundulika na matatizo na kujifungua salama"hatutaki kuona mwanamke mjamzito anafariki wakati wa kujifungua,ndiyo maana serikali ya awamu ya tano imeboresha huduma za afya na tumeanza ujenzi wa vyumba vya upasuaji wa dharura kwa mwanamke atakayepata uzazi pingamizi,kujifungua salama ni haki ya kila mwanamke mjamzito

Akisoma taarifa ya  Wilaya,Mkuu wa Wilaya ya Rufiji  Mhe.Juma Njwayo alisema mpango wa malipo kwa ufanisi umeongeza idadi ya akina mama wanaojifungulia kwenye zahanati na kutoka 3,382 mwaka 2016 hadi kufikia 4,086 mwaka 2017 na wanawake wanaohudhuria mahudhurio  manne kliniki wamefikia 3,955 mwaka 2017 kutoka 1,906 mwaka 2016.

"Hali ya upatikanaji dawa muhimu hivi sasa ni asilimia 91 na dawa zingine ni zaidi ya asilimia 50 na hii inachangiwa na mpango huu"alisema Mhe. Njwayo.

Malipo kwa ufanisi (RBF) wilayani Rufiji ulianza kutekelezwa mwaka 2016 kwa kupatiwa shilingi milioni 240 kutoka wizara ya afya na kila kituo cha afya ama zahanati kilipatiwa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuboresha miundombinu na inatekelezwa kwenye vituo kumi na mbili ambavyo vilikidhi vigezo vya mpango huo.
Waziri Ummy Mwalimu akipokea mabango kutoka kwa wananchi yenye jumbe mbalimbali kuhusiana na changamoto za Afya, wakati alipokuwa akitembelea Kituo cha Afya cha Ikwiriri na Zahanati ya Nyamwage katika ziara yake ya kuangalia utekelezaji unaofanyika kupitia mpango wa malipo kwa ufanisi unaotekelezwa katika mikoa nane nchini.
 Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  akimwelekeza mmoja wa Wazee waliopata vitambulisho vya Matibabu bure kwa Wazee wakati wa tukio hilo mapema leo Wilayani Rufiji.
  Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  akimkabidhi mmoja wa Wazee kitambulisho cha Matibabu bure kwa Wazee wakati wa tukio hilo mapema leo Wilayani Rufiji.
  Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwakabidhi baadhi ya Wazee vitambulisho vya Matibabu bure kwa Wazee wakati wa tukio hilo mapema leo Wilayani Rufiji.

Mpango wa Malipo kwa Ufanisi waleta mabadiliko hayo ikiwemo ujenzi na ukarabati wa choo na jengo hilo,kama jengo lionekanavyo pichani juu na chini Waziri Ummy akikagua choo hicho


   Waziri wa Afy,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu  akishangiliwa vilivyo na Wananchi wa Rufiji .

No comments: