Saturday, December 16, 2017

Mgalu Awataka Wakandarasi Wa REA kuongeza kasi Utekelezaji Wa Miradi

Msimamizi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Pangani kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Mahenda S. Mahenda (kulia) akitoa maelezo kuhusu uzalishaji wa umeme katika kituo hicho kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kushoto) katika ziara aliyoifanya mapema leo tarehe 15 Desemba, 2017 katika kituo hicho.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Pangani mapema leo tarehe 15 Desemba, 2017
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ( wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika ziara hiyo.


Na Greyson Mwase, Tanga

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaojenga miundombinu ya usambazaji wa umeme vijijini chini ya Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kuongeza kasi ili miradi yote iweze kukamilika ifikapo mwaka 2019.

Mgalu aliyasema hayo mapema leo tarehe 15 Desemba, 2017 katika ziara yake aliyoifanya katika kijiji cha Bwitini wilayani Korogwe mkoani Tanga, lengo likiwa ni kukagua hatua ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini iliyopo chini ya REA Awamu ya Tatu na kutorishishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Mgalu aliambatana na watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Alisema kuwa, Serikali ilikwishawalipa wakandarasi wote malipo ya awali na kuwataka kuanza kazi mara moja lakini wamekuwa wakifanya katika kasi ndogo hususan katika hatua ya upembuzi yakinifu.

“ Wakandarasi wengi wamekuwa wakichukua muda mrefu kutekeleza miradi kwa kisingizio cha kufanya upembuzi yakinifu wakati fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi zimekwishatolewa, nichukue fursa hii kuwatangazia wakandarasi wote nchini kuanza kazi mara moja,” alisema Mgalu

Aliendelea kusema kuwa mkandarasi yeyote atakayefanya kazi kwa kiwango kisichoridhisha atanyang’anywa kazi na kupewa mkandarasi mwingine mwenye uwezo wa kufanya kazi kulingana na kasi inayotakiwa na Serikali.

Alisema kuwa wananchi wengi kwa sasa hususan walipo katika maeneo ya vijijini wanahitaji nishati ya umeme kwa gharama nafuu, hivyo wamechoka na masuala ya michakato.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mgalu aliwataka wakandarasi wote nchini kununua vifaa kutoka ndani ya nchi hususan transfoma na nguzo badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi kama ilivyoagizwa awali.

Akielezea mikakati ya serikali katika uboreshaji wa upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, Mgalu alisema kuwa serikali kupitia REA Awamu ya Tatu inasambaza umeme katika vijiji vyote nchini ambapo ifikapo mwaka 2019 karibia vijiji vote vitakuwa na umeme wa uhakika.

Aliendelea kuelezea mikakati mingine kuwa ni pamoja na matumizi ya nishati jadidifu kama vile jua hususan katika maeneo yasiyofikiwa na umeme kutoka Gridi ya Taifa, ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji wa Stieglers Gorge na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia wa Kinyerezi I na Kinyerezi II.

Alisisitiza kuwa serikali imeweka mkakati wa kufufua mkoa wa Tanga kiuchumi hivyo kuwataka wawekezaji ndani ya nchi kuwekeza kwenye viwanda katika mkoa huo.

Alieleza kuwa kutokana na uwepo wa mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania katika mkoa wa Tanga, mahitaji ya umeme yatakuwa makubwa hivyo Wizara ya Nishati imejipanga katika kuhakikisha kuwa nishati ya uhakika inapatikana.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mgalu aliwataka wananchi wa Tanga kutoharibu vyanzo vya maji katika Bonde la Mto Pangani yanayotumiwa katika uzalishaji wa umeme katika kituo cha kufua umeme cha Hale ili kutoathiri uzalishaji wa umeme katika mkoa huo.

Alisisitiza kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua hali za kisheria wananchi watakaobainika wanaharibu mazingira.

No comments: