Mwenyekiti
wa Bodi ya TANESCO Dkt. Alexender Kyaruzi (katikati) na wajjumbe wa
bodi ya Shirika hilo, wakipatiwa maelezo walipotembelea kituo cha kupoza
na kusambaza umeme cha Mahumbika mkoani Lindi
Na Yasini Silayo
Shirika
la Umeme Tanzania TANESCO limewahakikishia Umeme wa uhakika wakazi wa
Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kutokana na uboreshwaji mkubwa wa
huduma za Uzalishaji, Usafirishaji na Usambazaji Umeme zinazoendelea
katika Mikoa hiyo.
Hayo
yamebainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa TANESCO, Dkt.
Alexander Kyaruzi alipofanya Ziara ya kikazi katika mikoa ya Lindi na
Mtwara akiambatana na wajumbe wengine wa bodi pamoja na viongozi
waandamizi wa TANESCO Makao Makuu na Kanda ya Kusini.
Akiongea
na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali Mkoani Lindi,
Dkt. Kyaruzi amesema kuwa tayari TANESCO imefanya matengenezo makubwa
katika mitambo ya kuzalisha umeme wa Gesi wa Megawati 18. Mtambo huo
unahudumia Mikoa ya Mtwara pamoja na Baadhi ya maeneo ya Lindi kupitia
laini mpya ya 132kV Mtwara-Mahumbika iliyokamilika tangu mwezi Julai
mwaka huu ikijengwa na mafundi wazawa kutoka ndani ya TANESCO kupitia
kampuni Tanzu yake iitwayo ETDCO.
"Mbali
na hali ya umeme kuimarika hivi sasa kutokana na matengenezo ya mitambo
ya Mtwara, Shirika hivi sasa linaendelea na maandalizi ya ujenzi wa
miradi miwili mikubwa ya Uzalishaji Umeme wa jumla ya megawati 540
Katika Mikoa hii pamoja na kuunga mikoa ya Kusini katika Umeme wa Grid
ya Taifa kwa Laini kubwa ya Msongo wa Kilovolt 400.
Awamu
ya kwanza ya ujenzi wa Mradii huu itakuwa kutoka Kinyerezi DSM mpaka
somangafungu Lindi ambapo patajengwa mtambo wa kuzalisha umeme wa
Megawati 240, mradi tayari umekwishaanza kwa kulipa fidia wananchi
walioko eneo la mradi ili wapishe kupitisha laini hiyo. Awamu nyingine
itaunga Somanga mpaka Mtwara ambapo kutajengwa pia mradi mkubwa wa
kuzalisha umeme wa Megawat 300. Songea tayari inaunganishwa na gridi
kupitia makambako na mradi unaelekea kukamilika kwa asilimia kubwa"
alisema Dkt. Kyaruzi
Aliongeza
kuwa kutokana na mikakati ya muda mfupi, ya kati na muda mrefu
iliyowekwa na TANESCO na Serikali ya awamu ya tano kwa ujumla, matatizo
ya umeme katika mikoa hiyo yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi wa kudumu na
hivyo kuchochea hamasa ya maendeo ya kiuchumi na Kijamii katika ukanda
huo.
Aliongeza
kuwa TANESCO inatarajia kupanua mifumo yake ya kusambaza umeme na
kuiunga na mifumo ya pamoja ya nchi za Kusini mwa bara la Africa,
Southern African Power pool (SAAP) kupitia Zambia pamoja na ile ya
Africa Mashariki Kupitia Nchi ya Kenya. Baada ya kuunganisha mifumo
hiyo Nchi itaweza kununua na hasa kuuza ziada ya umeme kwa Nchi hizo pale itakapohitajika.
Aidha
naye Mjumbe wa Bodi hyo Dkt. Lugano Wilson alisisitiza wakandarasi wa
miradi ya umeme katika mkoa huo na mikoa mingine kwa ujumla kuhakikisha
wanazingatia Viwango na Ubora wa kazi ili miradi hii iweze kutimiza
lengo kusudiwa la kuwahudumia wananchi kwa umeme wa uhakika na kuchochea
maendeo ya kiuchumi na kijamii.
"Mnapotekeleza
miradi hii kwa ubora na viwango vinavyotakiwa, wananchi watapata umeme
wa uhakika na kwa Upande wa TANESCO mtatupunguzia gharama za matengenezo
ya mara kwa mara yatokanayo na ujenzi wa laini yenye kiwango duni"
alisema Dkt. Lugano
Kwa
upande wa wananchi wa maeneo hayo walionesha kufarijika na kupata
shauku kubwa ya kuunganishwa na kuboreshewa huduma za umeme ambapo
mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Shabani alisema kuwa
"Licha ya changamoto za Umeme tulizokuwa nazo kipindi cha nyuma lakini
kwa kweli tumeshuhudia juhudi kubwa za viongozi wa Serikali, Wizara na
TANESCO wanaotutembelea na kutufariji kuwa hali itakuwa shwari, na kweli
sasa mambo yameanza kuwa mazuri umeme haukatiki tena mara kwa mara"
alisema Mwananchi huyo
Mwenyekiti
wa Bodi ya TANESCO Dkt. Alexender Kyaruzi akiongea na wananchi wa Mtama
Mkoani Lindi wakati wa ziara ya Bodi ya wakurugenzi wa TANESCO Katika
mikoa ya Lindi na Mtwara
No comments:
Post a Comment