Wednesday, December 20, 2017

MBULU WAMPONGEZA KAMOGA KWA KUFANIKISHA MAENDELEO

Wakazi wa Kata ya Masieda Wilaya yards Mbulu Mkoani Manyara, wamemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Hudson Kamoga kwa jitihada zake binafsi zilizofanikisha kupata ufadhili wa kumalizia madarasa ya shule ya msingi Umbur. 

Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Masieda Yasenti Lazaro akizungumza wakati Kamoga akizindua madarasa matatu ya shule hiyo alisema wananchi wa eneo hilo wanashukuru kwa kuwezesha umaliziaji wa jengo la darasa la shule hiyo. 

Lazaro alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2014 na kusajiliwa mwaka 2015 ina wanafunzi 335 na vyumba vinne vya madarasa. Alisema bado wanakabiliwa na upungufu wa vyumba vitatu vya madarasa na nyumba za walimu kwani hivi sasa kuna nyumba moja pekee ya walimu wanne waliopo shuleni hapo. 

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Masieda, Nicomed Nada ameshukuru Rais John Magufuli kumteua Kamoga kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwani anawatumikia wananchi kwa kuacha alama ya maendeleo. Nada alisema Kamoga ni mbunifu kwenye suala la maendeleo na amekuwa akipigania vipaumbele vya wananchi wa wilaya hiyo kwenye elimu, afya na maji. 

Alisema Kamoga ni mbunifu wa maendeleo kwani alifika kwenye shule hiyo na kubaini tatizo la ukosefu wa madarasa, akazungumza na wadau wa maendeleo waliowezesha jambo hilo. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Hudson Kamoga alisema baada ya kutembelea shule hiyo na kubaini changamoto ya darasa, wakati Halmashauri haikuwa na fungu la kulimaliza, alizungumza na mdau wa maendeleo waliyejitoa sh10 milioni, kwa ajili ya kumalizia ujenzi huo. 

Kamoga alisema baada ya kuzungumza na wadau wa maendeleo, wakawezesha fedha hizo na kufanikisha ujenzi huo wa darasa, ambapo sh7 milioni zilimalizia ujenzi huo na sh3 milioni zikatumika kwenye utafiti wa maji wa Kijiji vya Mamagi na Genda. Aliwapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa kufanikisha upatikanaji wa matofali 60 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mengine ya shule hiyo. 

“Kuhusu changamoto ya upungufu wa madarasa mengine msiwe na shaka ninyi anzeni kisha tutawaunga mkono kama awali kwani kwenye hayo madarasa mengine mlitumia nguvu zenu kisha tutasaidiana pamoja,” alisema Kamoga.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga akipokea zawadi ya mbuzi baada ya wananchi wa Kijiji cha Masieda kumpatia kama shukrani ya kuwezesha umaliziaji wa jengo la darasa la shule ya msingi Umbur ambapo aliwapa shilingi milioni saba alizopata kwa wadau ambapo kati ya shilingi milioni 10 alizozipata saba alitoa kwa shule hiyo na nyingine milioni tatu zikapelekwa kwenye vijiji vya Mamagi na Genda ili kufanya utafiti wa upatikanaji wa maji. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga akizindua madarasa matatu ya shule ya msingi Umbur, ambapo moja kati ya madarasa hayo alimalizia ujenzi wake kwa kutumia fedha alizozipata kwa wadau wa maendeleo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuari ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Starnley Kamoga akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masieda.
Mzee wa jamii ya wairaq John Tluway wa Kijiji cha Masieda Wilayani Mbulu Mkoani Manyara akimpa zawadi ya majani, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Hudson Kamoga baada ya kuzindua madarasa matatu ya shule ya msingi Umbur.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Starnley Kamoga akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Masieda.

No comments: