Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza kuwa kampeni ya kupanda na ustawishaji miti isiishie Dodoma mjini tu bali ienee katika Wilaya zote za mkoa wa huo na hatimaye nchi nzima.
Makamu wa Rais aliyasema hayo kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa kijani,alisema upandaji miti si kwa ajili ya kuhifadhi mazingira tu bali ni fursa ya kiuchumi, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambapo alitolea mfano mti mmoja uliokomaa unaweza kunyonya hadi kiasi cha kilo 150 za gesi ya hewa ya ukaa kwa mwaka,husaidia kupunguza joto, kusaidia kuboresha afya zetu za mwili na akili kama tafiti zinavyoonyesha .
“Ni dhahiri, kampeni hii ya kuifanya mji wa Dodoma kuwa wa kijani ni kuunga mkono uamuzi wa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli wa kuhamishia Makamo Makuu ya Nchi kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma kwa vitendo.” Alisema Makamu wa Rais.Makamu wa Rais amewataka Viongozi na Wana Dodoma kuipokea kampeni hii kwa mikono miwili na kutoa kila aina ya ushirikiano ili kufikia lengo zuri lililokusudiwa.
Makamu wa Rais ambaye alihamia rasmi mjini Dodoma siku ya ijumaa tarehe 15 Desemba, 2017 alitoa pongezi kwa Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba na Ofisi yake kwa kuja na wazo zuri .
Makamu wa Rais alisisitiza kuwa hategemei kuona zoezi la upandaji miti lianze na kuisha leo, na badala yake liwe la kudumu, pia alizitaka manisapaa zitunge sheria ndogo zitakazoelekeza shule, chuo, taasisi na familia kuanzisha bustani ndogo za miti zitakayomudu mazingira husika,Makamu wa Rais aliendelea kusema kuwa ni vyema kupunguza ukataji wa miti kiholela ambapo alizitaka sheria, kanuni na taratibu zizingatiwe kabla ya kukata miti na kusema tupande miti kabla ya kukata mti.
Makamu wa Rais alimalizia kwa kutoa shukrani kwa kampuni ya TATU Mzuka kwa kujitoa na kuhakikisha kampeni hii inatekelezwa na kutoa wito kwa Bodi ya Bahati Nasibu ya Taifa ya Tanzania iige mfano na kuelekeza makampuni mengine ya bahati nasibu yaweze kutoa mchango wake katika shughuli za kijamii hususan kwenye suala la hifadhi ya mazingira.
Pia Makamu wa Rais alitoa shukrani kwa Jeshi la Kujenga Taifa Makotopora, DUWASA, Magereza na Tanzania Forest Services (TFS) kwa kujitoa na kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hili.Mwisho, Makamu wa Rais aliwataka Wanawake wa mkoa wa Dodoma kuanzisha vikundi mbali mbali vya upandaji .
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiandaa mti wake kabla ya kuupanda mara baada ya kuzinduzi kampeni ya kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa Kijani iliyofanyika kwenye chanzo cha maji bonde la Makutupora, Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipanda mti mara baada ya kuzinduzi kampeni ya kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa Kijani iliyofanyika kwenye chanzo cha maji bonde la Makutupora, Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa Kijani iliyofanyika kwenye chanzo cha maji bonde la Makutupora, Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akitoa maelezo ya kampeni ya kupanda miti wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kuufanya mji wa Dodoma kuwa wa Kijani iliyofanyika kwenye chanzo cha maji bonde la Makutupora, Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
No comments:
Post a Comment