Thursday, December 21, 2017

DK.MABODI ATOA NASAHA KWA VIONGOZI

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Dk. Abdulla Juma Mabodi amewataka viongozi wa ngazi mbali mbali waliochaguliwa kwa ajili ya kuwatumikia wanachama  kujiandaa kisaikolojia kufanya kazi kwa weledi na ubunifu kwa lengo la kulinda hadhi na heshima ya chama hicho.

Rai hiyo ameitoa wakati akizungumza katika mahojiano maalum, amesema njia pekee ya viongozi waliochaguliwa ndani ya chama kuanzia ngazi za mashina hadi taifa kulipa mema kwa wanachama wao ni kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo endeleo kwa taasisi hiyo na kwa mwanachama mmoja mmoja.

Amesema baada ya Chama cha Mapinduzi kusajili rasmi jeshi lake la kisiasa kupitia uchaguzi huru na wa haki uliozingatia vigezo vyote vya kidemokrasia na Kikatiba , kwa sasa kazi iliyobaki ni kuanza mapambano kuhakikisha CCM inashinda kwa kishindo katika chaguzi za serikali za mitaa mwaka 2019 pamoja na uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Chama chetu kimepata viongozi wa ngazi mbali mbali ambao tumechaguliwa na wanachama wetu ili tuwatumikie kwa miaka mitano ijayo hivyo mimi nikiwa miongoni mwa waliochaguliwa nakuombeni tutumie uwezo na maarifa yetu kuleta mabadiliko ya kimaendeleo ndani ya chama.

Pia tutafakari kwa kina ni mambo gani ya msingi tunayotakiwa kuyafanyia kazi kabla ya 2020, ili tuyaweke katika mipango mikakati yetu kwa lengo la kuwahudumia wananchi wote.”, alisema Dk. Mabodi.

Aliwambia viongozi hao kwamba watambue kuwa baada ya kupewa jukumu la uongozi wanatakiwa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM mwaka 2015/2020 huku wakiongeza wanachama wapya  ndani ya taasisi hiyo.

Alisema  viongozi hao licha ya kuwa na majukumu ya kisiasa bado wanatakiwa kuwa na uthubutu wa kubuni miradi mbali mbali ya kiuchumi ili itoe ajira kwa wananchi ambao ndio mtaji wa kudumu wa Chama cha Mapinduzi.

Aidha amewashukru wanachama wa chama  hicho hasa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Tisa wa CCM Taifa kwa kumchagua kuwa miongoni mwa wajumbe  15 wa NEC kutoka Zanzibar na kuwaahidi kwamba ataendelea kuwa mwanachama, kiongozi  na mzalendo ndani nan je ya Chama.

Hata hivyo amewapongeza viongozi mbali mbali wakiwemo  Mwenyekiti wa CCM  Taifa Dkt. John Pombe Magufuli  na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar  Dkt. Ali Mohamed Shein  pamoja na Makamu Mwsenyekiti wa CCM Tanzania bara,  Philipo Mangula kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi waendelee kuzitumikia nafasi zao za uongozi.



Pamoja na hayo aliwakumbusha wanachama wa CCM kwamba wao ndio waajiri wa viongozi wote walioshika nyadhifa mbali mbali ndani ya chama hicho hivyo ni lazima wawe mstari wa mbele kulinda misingi,itikadi na thamani ya kisiasa ili maadui waotumia joho la vyama vya kisiasa kutaka kuindosha CCM madarakani wasifanikiwe kutekeleza mikakati yao.

No comments: