Wednesday, December 13, 2017

Kaimu Mkurugenzi TAA, Ataka Madereva Wa Magari Ya Zimamoto kuyatunza


DSC_3434
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama mbele), akiongea na askari wa zimamoto na uokoaji wa kituo cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA). Mbele kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa JNIA, Bw. Johannes Munanka na (kulia) ni Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege nchini, Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa.
DSC_3447
Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka  (aliyesimama mbele) akitoa maelezo mbalimbali kwa askari wa zimamoto na uokoaji katika kikao kilichoitishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela.
DSC_3450
Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa (aliyesimama) akiongea na askari wa kituo cha zimamoto na uokoaji cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, katika mkutano ulioitishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela.
DSC_3458
Askari Ramadhani Mgogo wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), aliyesimama akichangia masuala mbalimbali kwenye mkutano ulioitishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (watatu kushoto) katika meza kuu.
DSC_3477
Kamanda wa Vikosi vya Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege, Kamishna Msaidizi, Christom Manyologa (wa pili kushoto) akiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wapili kulia) na Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka (kushoto), wakiwa na msimamizi wa chumba cha Habari na Mawasiliano cha kituo hicho, afande Joines Matucha.
……………..
Na Mwandishi Wetu
KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela  amewataka madereva wanaoendesha magari ya zimamoto na uokoaji kwenye viwanja vyote vya ndege Tanzania kuyathamini na kuyatunza magari hayo kwa kuwa wameaminiwa kufanya kazi hiyo.
Bw. Mayongela alitoa kauli hiyo kwenye Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), alipokwenda kujitambulisha na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili, ambapo alisema magari hayo yamenunuliwa kwa gharama kubwa, hivyo yanapaswa kutunzwa.
Alisema uthamini wao kwa magari hayo kutayafanya kudumu na kuyafanya kazi kwa muda mrefu bila kuharibika, jambo ambalo litachangia ufanisi wa kazi, ya uokoaji na usalama kwenye viwanja vya ndege, ambapo mbali na miundombinu pia lazima miundombinu ipewe kipaumbele.
“Najua wapo wenzenu wachache sio waaminifu wamekuwa wakitengeneza manunuzi hewa ya vifaa na hata mafuta kwa manufaa yao binafsi, lakini ninawaomba mujione nyie ndio wenye thamani kwa kuaminiwa kuendesha magari haya ya mamilioni ya fedha, kwani ni nyie tu mnayoweza kuyaendesha kutokana na kuwa na mitambo ya kisasa tofauti kidogo na mengine, hivyo basi tuyatunze ili tuisaidie serikali yetu isiingie gharama za mara kwa mara za kununua vifaa au magari mengine mapya,” alisisitiza Bw. Mayongela.
Hatahivyo, alisema zimamoto ni moja ya mambo ya msingi hivyo amewahakikishia kuwapeleka kozi za mara kwa mara za ndani na nje ya nchi, kutokana na mambo mbalimbali yanayobadilika duniani, na kwa kuanzia ataanza na askari wawili hadi wanne, kulingana na mafunzo wanayostahili kushiriki, na atahakikisha washiriki ndio wanaokwenda kufanyia kazi kwa vitendo katika utendaji wao na sio kupeleka mabosi ambao hawahusiki.
“Nia yangu ni nyie kufanya kazi kwa weledi na kufanyakazi kwa bidii, nisije kusikia hakuna fedha, lakini wakati huo huo mnamuona Mkurugenzi mkuu anapanda ndege kwenda Ulaya na kurudi hizo fedha zinatoka wapi, nasema kama kweli kuna mambo ya msingi basi zimamoto ni jambo la msingi, hivyo basi sisi wafanya maamuzi tunatakiwa kuangalia wanaostahili kupata mafunzo na waende, hivyo nitahakikikisha kwa kadri ya bajeti nitatenga mafungu ya kupeleka watu wangu hawa kwenye mafunzo, ili nao waende na wakati katika endeshaji kulingana na mabadiliko ya teknolojia na mashirika ya usafiri wa anga duniani yanavyoagiza,” alisema Bw. Mayongela.
Hatahivyo, ameahidi kwa mwaka wa fedha 2017/2018 TAA itanunua magari sita ya zimamoto na uokoaji pamoja na redio zitakazotumika kwa mawasiliano katika chumba cha habari na mawasiliano, kinachowasiliana na mnara wa kuongoza ndege.
Kutokana  na kuharibika kwa mara kwa mara kwa magari ya zimamoto kwenye viwanja vya ndege Tanzania ameahidi kufufua karakana ya kutengeneza magari hayo iliyopo JNIA, ambapo tayari amewaita mafundi waliopo hapo kukutana naye ili kuwasilisha changamoto na vifaa vinavyohusiana na magari hayo, ili waanze kutengeneza kwa haraka baada ya kununuliwa vifaa hivyo.
Pia aliwataka kuwa na ushirikiano wa dhati na wafanyakazi wa TAA katika utendaji wao wa kazi na kuwa walinzi wa mali za serikali kutokana na wao wamekula kiapo.
Naye Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji wa Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna Msaidizi Christom Manyologa alisema amefarijika kwa ujio wa Kaimu Mkurugenzi wa TAA, Bw. Mayongela,  ambaye ameonesha nia thabiti ya kushirikiana katika kazi.
Kamishna Manyologa alisema askari wa zimamoto na uokoaji , astahili kuheshimika zaidi kwani yeye ndio anayeweza kuingia ndani na kufika karibu ya ndege na pia anayewasiliana na waongoza ndege.
“Huyu askari anastahili kuheshimiwa kwanza anamamlaka makubwa ya kuwa karibu kabisa ya ndege, kupita ndani ya barabara ya kutua na kuruka kwa ndege hivyo anaweza kufanya lolote baya akiamua, hivyo watendewe vizuri,” alisema Kamishna Manyologa.

No comments: