Wednesday, December 20, 2017

China Yaunga Mkono Juhudi Za Rais Magufuli

Na Mwandishi Maalum, Beijing

China imeahidi kushirikiana na Tanzania kikamilifu katika miradi ya kipaumbele ambayo Serikali ya AwamuyaTano imepanga kuitekeleza ili kufikia azma yake ya uchumi wa viwanda ifikapo 2020 na baadaye uchumi wa Kati ifikapo 2025.

Hayo yalibainishwa leo jijini Beijing na Naibu Waziri wa Biashara wa China, Mhe. Qian Keming na baadaye kukaririwa tena na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mipango (NDRC), Bw. Ning Jizhe walipofanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Mahiga aliainisha na kufafanua namna Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Maguful iilivyokusudia kuwashirikisha wadau mbalimbali kwenye utekelezaji wa miradi ya kipaumbele ambayo inalenga kuchochea agenda ya uchumi wa viwanda. 

Miradi hiyo ni pamoja na kuendeleza nishati ya umeme ambapo Serikali imedhamiria kuzalisha umeme wa megawatts 5000 ifikapo mwaka 2020 ili kuharakisha utekelezaji wa agenda ya uchumi wa viwanda ambayo haitaweza kufanikiwa kama hakutakuwa na umeme wa kutosha na wauhakika.

Kutokana na uhalisia huo, Serikali imepanga kujenga kituo cha kuzalisha umeme wa megawatts 2100 kwenye mto Rufiji na kujenga njia za kusambaza umeme huo kutoka Rufiji, Chalinze hadi Dodoma na nyingine kutokaChalinze, Kilimanjaro hadi Arusha. 

Miradi mingine ni ujenzi wa mtandao wa usafiri wa reli na uboreshaji wa reli ya TAZARA, ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na viwanja vya ndege ikiwa ni pamoja na kujenga jengo la abiria katika Kiwanja cha ndege cha Mwanza. 

Waziri Mahiga alisisitiza umuhimu wa miundombinu hiyo kuunganishwa ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa katika uchumi. Aliongeza kuwa uchumi wa Tanzania unakua kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka na uchumi wa nchi za jirani ambazo zinategemea bandari za Tanzania pia unakua, hivyo kuendeleza na kuunganisha miundombinu ya usafiri ni muhimu kwa ustawi wa uchumi wa nchi hizo na uchumi wa Tanzania.

Aidha, Waziri Mahiga alieleza namna Serikali inavyoendelea na zoezi la kuhamisha makao makuu ya Serikali kwenda Dodoma na kukaribisha makampuni ya China kushiriki kwenye uwekezaji wa miundombinu mbalimbali kwenye mji huo mpya wa makao makuu.

Baadhi ya miundombinu muhimu inayohitajika Mjini Dodoma ni upatikanaji wa maji safi ya na ya uhakika na kuiomba China ishiriki katika ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro. Bwawa hilo likijengwa na kukamilika litasaidia sio tu kusambaza maji ya uhakika mkoani Dodoma bali hata mkoa wa Dar Es Salaam ambao matumizi ya maji yanaongezeka kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu kila siku.

Waziri Mahiga aliahidi kuwa Serikali yake itakamilisha taratibu zilizosalia ili mradi wa Mchuchuma na Liganga uweze kuanza kwa kuwa mradi huo ni muhimu sana katika sera ya uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Biashara aliahidi kuwa Serikali ya China itafanyia kazi kwa haraka miradi yote iliyowasilishwa ili Tanzania iweze kutimiza malengo yake ya kuwaletea maendeleo wanachi. 

Aliongeza kuwa Serikali yake itaharakisha kufanya upembuzi yakinifu wa miradi hiyo kwa madhumuni ya kutimiza masharti ya kampuni za uwekezaji na taasisi zinazotoa fedha nchini China.

Aidha, alipongeza hatua ya Serikali ya Tanzania ya kuweka mikakati ya kuzalisha umeme wa megawatts 5000 ifikapo mwaka 2020. Hivyo, aliahidi kuwa atazishawishi kampuni za China zinazozalisha umeme wa jua, upepo na joto ardhi zijek uwekeza nchini ili lengo hilo litimie kwa haraka.

Wakati huo huo, Waziri Mahiga alikutana na watendaji wa makampuni mbalimbali ya uwekezaji yaliyodhamiria kuwekeza nchini kwenye sekta mbalimbali. Makampuni hayo yanataka kuwekeza kwenye uzalishaji wa Sukari, ujenzi wa kiwanda cha kusindika mihogo, uagizaji wa mihogo mikavu toka Tanzania kwa wastani wa tani laki 3 hadi 5 kwa mwaka na huduma za kitalii kama ujenzi wa mahoteli yenye hadhi ya nyota tano. 

Kampuni hizo zote zimeomba kukutanishwa na wadau husika ili wkamilishe taratibu zinazotakiwa waanze uwekezaji haraka iwezekanavyo.

Waziri Mahiga aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa uamuzi wao wa kuwekeza Tanzania hawataujutia kwa kuwa Tanzania ni nchi tulivu na yenye amani, ina rasilimali nyingi na soko kubwa kutokana na kuwa mwanachama wa SADC na EAC. 

No comments: