Wednesday, November 15, 2017

ZANZIBAR KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO NJITI NOVEMBA 17 /2017

Na Ramadhani Ali – Maelezo 

Jamii ya wazanzibari  imeshauriwa kufikiria mikakati na huduma bora zitakazosaidia kupunguza idadi ya kuzaliwa na kufariki watoto njiti ili ambao wanakuwa mzigo kwao na Serikali kwa jumla.

Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bi. Asha Ali Abdalla alipokuwa akitoa tamko  kwa waandishi wa habari kuhusu siku ya maadhimisho ya watoto njiti duniani katika ukumbi wa Wizara hiyo Mnazimmoja Mjini Zanzibar.

Alisema sababu ya kufanyika maadhimisho ya watoto njiti duniani sio kuwabeza watoto hao lakini ni kuamsha hisia na kuinua uwelewa kwa wananchi na watoa huduma  ya afya ya watoto hao kwani iwapo hatua zinazofaa hazitachukuliwa wataendelea kuzaliwa na kufariki kwa idadi kubwa.

Alisisitiza kuwa Shirika la Afya duniani linaamini kuwa vifo vya watoto njiti vinaweza kuepukika kwa silimia 75 iwapo jamii ikishirikiana na Serikali wataweka mkazo huduma za kinga, ugunduzi wa matatizo mapema na matibabu bora na kwa wakati stahili.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya alikumbusha kuwa takriban watoto wote wanaozaliwa njiti wanakuwa na matatizo mengi ya kiafya yanayohitaji huduma za haraka kwa uokozi wa maisha yao.Alisema huduma hizo mara nyingi zinakuwa mzigo usiotarajiwa kwa familia, ndugu na jamaa na kupelekea changamoto nyingi zikiwemo za uzalishaji kiuchumi.

Alitanabahisha kuwa suala la msingi ni kufanyakazi kwa pamoja katika kutoa huduma sahihi na rahisi zitakazopelekea kupungua kuzaliwa watoto njiti vyenginevyo Zanzibar haitaweza kufikia lengo kuu la kumaliza vifo vinavyoweza kuepukika kwa watoto wachanga ifikapo mwaka 2030.

Alisema Wizara ya Afya imejipanga kutoa elimu ya Afya juu ya matatizo yanayochangia kuzaliwa watoto njiti, kuimarisha huduma zao katika ngazi zote na kuongeza wataalamu wanaotoa huduma za watoto njiti katika ngazi za hospitali, vituo vya afya na katika jamii.

Akieleza ukubwa wa tatizo la watoto njiti Katibu Mkuu alieleza kuwa takwimu kutoaka hospitali ya Mnazimmoja pekee zinaonesha kuwa kati ya watoto 347 waliofariki watoto njiti walikuwa 154 ambao ni asilimia 44.

Alizitaja sababu za kuzaliwa watoto njiti ni pamoja na maradhi yasiyoambukiza, wajawazito wenye umri chini ya miaka 20 na zaidi ya mika 40, kuwa na maambukizi wakati wa ujauzito, utumiaji wa dawa za kienyeji wakati wa ujauzito na ulemavu katika viungo vya uzazi.

Watoto njiti ni kizazi hai ambacho huzaliwa kabla ya kutimia wiki 37 za ujauzito ambapo kilele cha maadhimisho hayo  hufanyika  kila ifikapo tarehe 17 Novemba na kauli mbiu ya mwaka huu TUFANYE KAZI KWA PAMOJA KUWATUNZA WATOTO NJITI.                        
                                        
Wakati huohuo Muuguzi Mkuu wa hospitali ya Mkoa wa kaskazini Unguja Mwanamvua Said alisema kuwa ulezi wa watoto njiti unahitaji ushirikiano mkubwa kati ya hospitali na wazazi ili kudumisha afya ya watoto hao.
Muuguzi huyo alitoa ushauri huo wakati wa maadhimisho ya mtoto njiti yaliyofanyika kimkoa katika hospitali ya Kivunge.

Aliwataka wazazi kuacha tabia ya kuwalaza watoto njiti kwenye magodoro kwani kufanya hivyo kunaweza kuathiri afya ya mtoto kutokana na joto kali la magodoro.
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Ali Abdalla akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya mtoto Njiti yatakayofanyika tarehe 17 mwezi, mkutano huo ulifanyika Ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
 Daktari wa watoto Khamis Ali Abeid akitoa ufafanuzi wa masuala ya waandishi wa habari katika mkutano uliozungumzia maadhimisho ya mtoto njiti yatakayo fanyika tarehe 17 mwezi huu, mkutano huo  ulifanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.
 Muuguzi Maryam Juma Bakari kutoka Hospitali Kuu ya Mnazimmoja akitoa shukrani kwa waandishi wa habari katika mkutano huo.
Waandishi wa habari Makame Mshenga wa Maelezo na Rahma Suleiman wa Gazeti la Nipashe wakifanya zoezi la njia muafaka ya kumpatia huduma ya kumbeba mtoto njiti ili apata joto la mzazi (kangaroo) katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Wizara ya Afya.
Picha na Makame Mshenga.

No comments: