Monday, November 6, 2017

WAZIRI UMMY AWATAKA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KUAMSHA ARI YA JAMII KUSHIRIKI KATIKA SHUGHULI ZA MAENDELEO

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb), (Kushoto) akisalimiana na Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga (katikati) wakati alipowasili kufungua Mkutano wa Mwaka wa wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Mjini Dodoma.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu(Mb), akisalimiana na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike wakati alipowasili kufungua Mkutano wa Mwaka wa wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Mjini Dodoma.
 Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akitambulisha washiriki wa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii kwa mwaka 2017 unaofanyika Chuo cha Mipango mkoani Dodoma na kujumuisha Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya Taifa, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Mitaa na wawakilishi kutoka Sekta na Mashirika mbalimbali nchini.
 Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Elimu Bw. Tikson Nzunda akifafanua neno wakati wa Mkutano MKuu wa Kitaifa wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii kwa mwaka 2017 unaofanyika Chuo cha Mipango mkoani Dodoma kuhusu umuhimu wa kuwatumia wataalamu wa Maendeleo ya Jamii katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo yao.
 Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga akitambulisha malengo ya Mkutano Mkuu wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii 2017 na kumkaribisha Mgeni rasmi Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu kufungua Mkutano wa Mwaka wa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu(Mb) akisisitiza maafisa Maendeleo ya Jamii nchini kuamsha ari ya wananchi kushiriki katika shughuli za kimaendeleo kuelekea uchumi wa Viwanda wakati akifungua Mkutano wa wataalam wa Sekta ya Mandeleo ya Jamii unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Mjini Dodoma.
 Baadhi ya Maaafisa Maendeleo ya Jamii wakisikiliza maelekezo ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu(Mb)(hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii nchini unaofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.  
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu(Mb) akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI mara baada ya kufungua Mkutano wa wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii Mjini Dodoma.
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu(Mb) (katikati) akijadiliana jambo na Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Elimu Bw. Tikson Nzunda (kulia) mara baada ya kufungua Mkutano wa wataalam wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii Mjini Dodoma kushoto ni Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW

Na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
Serikali imewataka Wataalam wa Maendeleo ya Jamii kurejesha ari na hamasa ya jamii kushiriki katika kazi za maendeleo ili kutoa mchango katika kufikia Tanzania ya Viwanda na yenye uchumi wa kati.

Kauli hii imetolewa MJini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 12 wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii unafoanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma.

Mhe. Ummy Mwalimu  amesema kuwa kupitia Mkutano huo Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wanatakiwa  kutoa  mapendekezo kuhusu mbinu bora zitakazosaidia kurudisha ari na hamasa ya jamii kushiriki katika maendeleo na hivyo kusaidia kufikia uchumi  wa kati na wa viwanda.

Mhe. Ummy Mwalimu amefafanua kuwa wataalam wa maendeleo ya jamii ndiyo wenye jukumu la kuhamasisha utekelezaji wa miradi ya kisekta hususan kilimo, afya, elimu, na miundo mbinu na kadhalika.

“Wataalam wa  Maendeleo ya Jamii watumie fursa hii kujitathmini ili kupata majibu ya namna bora ya kutekeleza majukumu yao ya kuamsha ari ya wananchi kushiriki kwenye uzalishaji na kutokomeza ukatili wa jinsia ambao unapunguza kasi ya kufikia uchumi wa kati na maendeleo jumuishi” alisema Mhe. Ummy.

Waziri Ummy ameeleza kuwa Kaulimbiu ya Mkutano wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii kwa Mwaka 2017  ambayo ni  “Amsha Ari ya Ushiriki wa Wananchi Kufikia Uchumi wa Viwanda” inatafsiri azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa na Tanzania ya Viwanda ili kufikia uchumi wa kati. 
     
Naye Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bibi. Sihaba Nkinga amesema kuwa katika awamu ya sasa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii wana wajibu wa kuelimisha na kuamsha ari ya wananchi kufanya kazi za uzalishaji kwa bidii kwa kuzalisha mali ghafi zinazohitajika na viwanda na kuwekeza kwenye viwanda vidogo vidogo na vya kati.

Bibi Sihaba Nkinga amefafanua kuwa malengo ya Mkutano huo umezingatia  tathmini ya mchango wa Sekta ya Maendeleo ya Jamii katika kuamsha  ari na hamasa ya wananchi kushiriki na kuchangia maendeleo kwa kushirikiana na viongozi wa Sekta na Idara nyingine katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike amewaasa Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na wadau  kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kujitoa katika kufanya kazi za kujiletea maendeleo katika maeneo yao.

Lengo la Mkutano huu wenye kauli mbiu isemayo “Amsha Ari ya Ushiriki wa Wananchi Kufikia Uchumi wa Viwanda” ni kuhakikisha Wizara na wadau wanashirikiana katika kuamsha ari ya wananchi kufanya kazi za maendeleo na kusimamia Mpango ya kutokomeza ukatili wa jinsia ambao kwa kikasi kikubwa unapunguza kasi ya Taifa kufikia uchumi wa viwanda.

No comments: