Thursday, November 2, 2017

WADAIWA SUGU WA MAJI WILAYA YA KIBONDO KUUNDIWA KIKOZI KAZI

Na Rhoda Ezekiel Kigoma.

MKUU wa Wilaya ya Kibondo Luis Bura ameahidi kuunda kikosi kazi, kitakacho pita na kukusanya kiasi cha shilingi milioni 50 kwa Wadaiwa sugu wa Mamlaka ya maji safi Wilayani kibondo na kuhakikisha zinalipwa na kukabidhiwa kwa bodi mpya ya maji pamoja na kusitishia huduma ya maji kwa wale wote watakao shindwa kulipia madeni yao ya Nyuma.

Aidha Bura aliwaagiza wale wote wanao lima karibu na vyanzo vya maji kuacha kulima na kuondoa mazao yao kabla ya kuanza kutolewa kwa nguvu na kuharibiwa,vyanzo hivyo kujaa michanga wakati wa masika kutokana na  baadhi ya wananchi kukosa uwelewa na kulima kwenye vyanzo na kupelekea  upungufu wa maji katika wilaya hiyo.

Akizungumza jana Wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya maji Wilayani humo Mkuu huyo alisema, Serikali hadi sasa imeingia gharama ya kulipia deni la umeme ili kuhakikisha Wananchi wanaendelea kupata maji , wakati kuna baadhi ya Taasisi zikiwemo za Serikali na Wananchi wanadaiwa kiasi cha zaidi ya milioni 50.

Alisema Mamlaka hiyo imekuwa ikijiendesha kwa hasara hali iliyo walazimu  kuanzisha mfumo mpya wa usambazaji wa maji kwa kutumia Sola ilikupunguza gharama za matumizi ya umeme ambayo hayaendani na Makusanyo ya mamlaka ya maji na kuagiza fedha hizo zitakazo kusanywa kuanzia kesho zipelekwe kwenye marekebisho ya sola na wananchi waweze kuepukana na kero ya ukosekanaji wa maji.

"Nimepitia orodha ya wadaiwa Mimi pia ni miongoni mwa wadaiwa nimekuta na mimi kuda deni kubwa halijalipwa, taasisi zote na Wananchi muhakikishe mnalipa deni hilo wananchi wamekuwa wakikosa maji kwakuwa uwezo wa mamlaka kulipia bili ya umeme haiwezi kutokana na madeni hayo kila mtu ataubeba msalaba wake nitahakikisha fedha hizo zinakusanywa ukishindwa kulipa utasitishiwa huduma", alisema Mkuu huyo.

Kwa upande wake Katibu wa Bodi ya maji ambae pia ni Muhandisi wa maji wa Wilaya ya Kibondo, Michael Nguruwe alisema kuundwa kwa bodi mpya kutasaidia kuleta mabadiliko mapya katika mamlaka ya maji na kumuomba Mkuu huyo kuwasaidia kukusanya fedha hixo ilikuweza kuanza kwa upya na kuhakikisha Wananchi wanapata maji ya kutosha.

Alisema Wao kama bodi mpya wameandaa mkakati mpya wa kuhakikidha wanawaondoa wote waliovamia vyanzo vya maji na kuanzisha vyanzo vipya vya maji ilikuwapa urahisi wananchi wa kupata maji katika maeneo yao na kuepukana na usumbufu wa ukosekanaji wa maji.

Nae Mwandisi wa Maji Mkoa Azizi Mtabuzi alisema bodi hiyo imeundwa kwa kufuata sheria na kanuni, kila mmoja ataingia katika bodi kwa kuwakilisha kundi lake , mwakilishi wa watumiaji maji wakubwa, Mwakilishi upande wa serikali Mkurugenzi mtendaji, mwakilishi wa madiwani, mwakilishi wa watumiaji wakubwa na Meneja wa mamlaka husika ni katibu wa bodi.

Aliwaomba wote waliochaguliwa katika bodi kuleta mabadiliko katika mamlaka, na wafahamu ya kuwa kazi ya bodi ni kusimamia watendaji na kuwashauri watendaji namna ya kufanya ilikuhakikisha mamlaka inaongeza ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha wananchi wanapata maji ya kutosha






No comments: