Thursday, November 2, 2017

MAJABA ALIVYOPOKELEWA KWENYE NYUMBA YAKE BUNJU B JIJINI DAR

 Nyumba iliyopo Bunju B ilivyokuwa kabla ya makabidhiano jana. Mkurugenzi wa Mkuu wa Global Group, Eric Shigongo (wa kwanza kulia) na George Majaba (wa pili kulia) pamoja na Meneja Mkuu wa Global, Abdallah Mrisho wakijadiliana jambo. ... Shigongo akizungumza machache mbela ya nyumba hiyo kabla ya kumkabidhi George Majaba jana. Mara baada ya kukata utepe, Shigongo akifungua nyumba hiyo. Ndani ya nyumba kushoto, George Majaba, Afisa Masoko, Jimmy Haroub, Mkurugenzi Mtendaji, Eric Shigongo, mke wa Majaba, Meneja Mkuu, Abdallah Mrisho na Mhariri Mwandamizi, Elvan Stambuli wakifurahia mandari ya nyumba. George Majaba akiwa na majirani zake wapya wa Bunju B kwenye nyumba yake mpya, hapo walikuwa wakimkaribisha. Majaba akizungushwa kuoneshwa mandari ya nje ya nyumba yake mpya.

Msafara wa magari ukiongozwa na pikipiki zaidi ya tano ulitokea makao makuu ya Global Group Sinza Mori Dar, huku Mshindi wa Shindano la Nyumba Awamu ya Pili, George Majaba akiwa kwenye gari la wazi aina ya BMW huku mke wake akiwa kwenye gari lingine na watoto wao . 

Msafara ulipita Barabara ya Shekilango, ukaingia Barabara ya Ali Hassani Mwinyi kisha ukaingia New Bagamoyo, njiani kwa kuwa kulikuwa na gari la matangazo, watu walikuwa wamejipanga kumshuhudi Majaba aliyejawa na tabasamu akipita akiwa kwenye gari hilo la wazi. 

 Msafara ulipofika Tegeta umati ulikuwa mkubwa na wengi waliokuwa wakimuona Majaba walikuwa hawaamini macho yao kwani yeye mshindi alikuwa akiwapungua mkono na msafara ukawa unaenda kwa mwendo wa polepole, hali iliyofanya baadhi ya wananchi kumkaribia mshindi na walisikika wakisema ‘Hongera, Hongera!” Lakini abiria waliokuwa kwenye mabasi ya daladala nao walionekana wakitoa vichwa vyao madirishani na kumpongeza Majaba ambaye mara zote alikuwa na tabasamu usoni. 

 Hali ilikua hivyo hivyo msafara ulipofika Boko na baada ya kufika Bunju msafara ulisimama kabla ya kuingia Barabara ya Mabwepande ambapo kwa mwendo mfupi tu msafara uliingia kwenye nyumba mpya ya Majaba. Mara baada ya kufika, Meneja Mkuu, Abdallah Mrisho alitambulisha kwa wageni na wenyeji waliofika kushuhudia makabidhiano hayo na kisha akampa nafasi Mkurugenzi Mtendaji wa Global Group, Eric Shigongo kusema machache. “Kifupi leo tunamkabidhi nyumba yake Bwana Majaba. 

Ni jambo linalofurahisha kuona yupo hapa na familia yake ya mke na watoto watatu, hivyo bila kupoteza muda karibuni tufungue nyumba,” alisema Shigongo. Baada ya kusema maneno hayo Shigongo, Majaba na mkewe walishika utepe na Shigongo akaukata kuashirika kuwa sasa wamekabidhiwa nyumba yao. 

 Baadaye Majaba na watu wengine wakiongozwa na Shigongo waliingia ndani na kuoneshwa kila chumba, baadaye nje na uani ambako kulikuwa na nafasi kubwa na Shigongo alimuambia mke wa Majaba kwamba eneo hilo anaweza kufanyia miradi kama ya kufuga. Wenyeji walimkaribisha Majaba na baadaye wakapiga picha ya pamoja huku wakimpongesha kwa kushinda nyumba hiyo. Shughuli hiyo iliisha saa moja kasoro robo jioni. 

HABARI NA ELVAN STAMBULI, PICHA MUSSA MATEJA.

No comments: