Sunday, November 19, 2017

UTAFITI MAPATO NA MATUMIZI KAYA BINAFSI WAANZA TANZANIA BARA

Benny Mwaipaja

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amezindua zoezi la ukusanyaji wa Takwimu za utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, utakaogharimu shilingi bilioni 10 zilizotolewa na Benki ya Dunia.

Lengo la utafiti huo utakaofanywa na Ofisi Kuu ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni kupata takwimu zinazohusu shughuli za kijamii na kiuchumi, mapato na matumizi, hali ya makazi na umiliki wa rasilimali katika ngazi ya kaya.

Dkt. Mpango alisema kuwa Utafiti huo utaiwezesha Serikali kupima kiwango cha hali ya umaskini wa kipato, chakula na pengo baina ya matajiri  na maskini kuanzia kipindi cha mwaka 2013 hadi sasa.

“Takwimu zilizopo hivi sasa zinaonesha kwamba kiwango cha umasikini wa kipato ulipungua kutoka asilimia 34 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 28.2 mwaka 2012” Alisema Dkt. Mpango.

Alisema pamoja na takwimu hizo, bado kiwango cha umasikini ni kikubwa na kwamba Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali inahakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za msingi za kijamii kwa kadri uchumi unavyokua hivyo kupunguza kama si kumaliza kabisa tatizo la umasikini.

“Nimefurahi kuelezwa kuwa utafiti huu utakusanya takwimu katika kaya binafsi 10,460 kwa Tanzania Bara kuanzia Novemba 2017 hadi Novemba 2018 na kwamba kupitia zoezi hili, Serikali ya Awamu ya Tano imetoa ajira kwa vijana wapata 620 katika maeneo ya vijijini na mijini” alieleza Dkt. Mpango.

Aliwaasa wadadisi hao kufanyakazi zao kwa umakini na weredi mkubwa ili takwimu zitakazopatikana ziwe sahihi na kuonya kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaojaribu kuvuruga zoezi hili.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa alieleza kuwa ukusanyaji wa Takwimu za utafiti wa mapato na matumizi ya kaya binafsi utafanyika katika maeneo 754 yaliyochaguliwa kitaalamu kwa kutumia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

“Utafiti huu utakuwa wa saba tangu Tanzania ipate uhuru wake mwaka 1961, ambapo tafuti nyngine zilifanyika 1969, 1991/92, 2001, 20117 na mwaka 2011/12” aliongeza Dkt. Chuwa.

Alisema kuwa utafiti huo mpya utafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa ijulikanayo kama Survey Solution (CAPI) na kwamba matokeo ya awali ya utafiti huo yanatarajiwa kutolewa ndani ya miezi sita ijayo ili nchi iweze kufahamu kiwango cha umasikini uliopo katika jamii hivi sasa baada ya kufanyika kwa utafiti kama huo miaka mitano iliyopita.

“Utafiti wa mwisho uliofanyika mwaka 2011/2012 uliotumia karatasi uligharimu shilingi bilioni 20 lakini kwa kutumia teknolojia mpya, utafiti huu utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 10 pekee” alisisitiza Dkt. Chuwa.

Dkt. Chuwa alisema kuwa anaamini matokeo ya utafiti huo yatakuwa chachu ya kupata takwimu za msingi kwa ajili ya kufuatilia na kutathimini utekelezaji wa program mbalimbali za kitaifa na kimataifa zenye kulenga kupunguza kiwango cha umasikini nchini.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu ya TEHAMA Bw. Baltazar Kibola alisema kuwa watatoa ushirikiano wakutosha kwa wadadisi hao katika ngazi zote kuanzia Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata, Vijiji na Vitongoji ikiwemo kufanyia marekebisho vitendeakazi vya kukusanyia takwimu hizo vikipata hitililafu ili azma ya Serikali ya kupata takwimu sahihi itimie kama ilivyopangwa.
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu  (NBS) Dkt. Albina Chuwa akitoa maelezo kuhusu namna utafiti  wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi utakavyotekelezwa wakati wa kufunga mafunzo ya wadadisi na uzinduzi wa wa zoezi la ukusanyaji takwimu za utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi, Mjini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara Fedha na Mipango Dkt. Khatibu Kazungu akimkaribisha  Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kufunga mafunzo ya Wadadisi, na kuzindua zoezi la ukusanyaji wa Takwimu za Utafiti wa Mapato na Matumizi wa Kaya Binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, Mjini Dodoma.

 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akizungumza jambo wakati wa kufunga mafunzo ya Wadadisi na kuzindua zoezi la ukusanyaji wa Takwimu za Utafiti wa Mapato na Matumizi wa Kaya Binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, mjini Dodoma, utakaohusisha kaya binafsi 10,460.

 Meza Kuu (Walioketi) wakiwa katika picha ya pamoja na Wasimamizi wa zoezi la ukusanyaji wa Takwimu za Utafiti wa Mapato na Matumizi wa Kaya Binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, mjini Dodoma. Utafiti huo utahusisha kaya binafsi 10,460.

 Wadadisi wa Takwimu za Utafiti  wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara wa Mwaka 2017/2018, wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa hafla ya uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), (hayupo pichani), Mjini Dodoma.
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu  (NBS) Dkt. Albina Chuwa akitoa maelezo kuhusu namna utafiti  wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara utakao gharimu shilingi bilioni 10, wakati wa kufunga mafunzo ya wadadisi na uzinduzi wa wa zoezi la ukusanyaji takwimu za utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi, Mjini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) akizungumza jambo wakati wa kufunga mafunzo ya Wadadisi na kuzindua zoezi la ukusanyaji wa Takwimu za Utafiti wa Mapato na Matumizi wa Kaya Binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, mjini Dodoma, utakaohusisha kaya binafsi 10,460. 
Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI, anayeshughulikia TEHAMA Bw.  Baltazar Kibola, akieleza mikakati ya Ofisi yake katika kusaidia kufanikisha zoezi la ukusanyaji wa takwimu za utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi Tanzania Bara mwaka 2017/2018, uzinduzi huo umefanyika mjini Dodoma. 
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments: