Wednesday, November 8, 2017

TFDA Yafuta Usajili wa Dawa zenye madhara kwa Binadamu

Na. Prisca Libaga-MAELEZO, Arusha.

Mamlaka ya chakula na dawa TFDA imezifutia usajili dawa mbalimbali za kutibu magonjwa ya binadamu na kuziondoa kwenye soko pamoja na kusitisha matumizi yake kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa wagonjwa.

Hayo yameelezwa jana Jijini Arusha na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Bw. Hiiti Sillo, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya wakufunzi wa ufuatiliaji juu ya ufundishaji na uhamasishaji wa masuala ya udhibiti wa madhara yatonayo na matumizi ya dawa zisizosalama kwa watendaji wa afya kutoka Wilaya zote za mkoa wa Arusha.

Bw. Sillo mesema katika kudhibiti matumizi ya dawa zisizofaa TFDA imeondoa dawa ya sindano aina ya Chloramphenical kwenye soko baada ya shirika la afya Duniani WHO, kubaini dawa hiyo ina madhara kwa watumiaji, Pia mamlaka hiyo imefuta usajili wa dawa zingine kama vile Ketoconazole, (vidonge) Phenylpropanalamine,Dextropropoxyphene,Nimesulide,stavudine 40, Gatifloxacin,Rofecoxib, pamoja na Celecoxib baada ya kuthibitika zina madhara kwa watumiaji. 

Aidha matumizi ya dawa kama vile Kanamycin,Amikacin na Levofloxacin zimebadilishwa ili ziweze kutumika kwa ajili ya kutibu ugonjwa wa kifua kikuu pekee.

Mkurugenzi huyo wa TFDA amesema mafunzo hayo yanashirikisha wakufunzi 60 nchini kote na yanafanyika katika mikoa mbalimbali yakiwashirikisha Madaktari, Manesi, na wafamasia walioko kwenye hospitali, vituo vya afya na Zahanati.

Bw.Sillo alieleza kwamba, lengo la mafunzo hayo ni kuongeza idadi ya wakufunzi wa masuala ya usalama wa dawa kutoka 73 hadi 133 na tayari katika kipindi cha miaka mitatu 2014/ 15 hadi 2017/18, Mamlaka ya chakula na dawa imehamasisha watendaji wa afya wapatao 2000 nchini kote na sasa uhamasishaji unaendelea katika mkoa wa Katavi.

Alisema mara baada ya mafunzo hayo wakufunzi hao watafundisha wenzao kwenye maeneo yao ya kazi ili kuongeza uelewa kwa wataalam wengi zaidi kufahamu taratibu zilizoko za udhibiti wa madhara yanayotokana na matumizi ya dawa zisizofaa.

Aliwakumbusha wakufunzi hao kwamba kila mtendaji wa afya ana wajibu wa kulinda afya za wagonjwa anao watibu au kuwahudumia na wajibu huo ni pamoja na kuhakikisha wagonjwa wanabaki salama na ikiwa watapata madhara hatua za kuwatibu zinachukuliwa na kutoa taarifa ili kuzuia kusambazwa zaidi kwa dawa zinazoleta madhara. 

Bw. Sillo alifafanua kuwa, kumekuwa na baadhi ya wataalam wa afya kudhani kuwa kwa kutoa taarifa kuwa dawa ina madhara inaonekana kuwa wao ndio wanaosababisha madhara hayo na kusisitiza kuwa dhana hiyo sio ya kweli, hivyo akawasisitiza watoe taarifa sahihi ili wananchi wafahamu madhara yatokanayo na matumizi ya dawa pamoja na hatua za kuchukua. 

Mamlaka ya chakula na dawa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma wametengeneza mfumo wa kielektroniki wa utoaji wa taarifa za usalama na madhara ya dawa ambao ulizinduliwa Oktoba 2016 na Waziri wa afya Mh.Ummy Mwalimu. 

Kabla ya kuzinduliwa mfumo huo taarifa za usalama na madhara ya dawa zilikuwa zikitolewa kwa kutumia fomu maalumu za njano ,kijani na blue ambapo watoa huduma za afya walikuwa wakitumia fomu za njano huku wagonjwa wakitoa taarifa kwa kutumia fomu za za kijani, na fomu za bluu zilitumika kutoa taarifa za ubora wa dawa na kama kuna dawa duni au bandia kwenye soko.

No comments: