Mkurugenzi wa Uchaguzi Kailima Ramadhani akiwa na kitabu cha wageni kwenye Ofisi ya Serikali ya
Mtaa wa Malindi Estate ambayo ipo kwenye nyumba ya mmoja wa wagombea wa Uchaguzi Mdogo
wa Madiwani Kata ya Mbweni. Picha na NEC.
Hussein Makame-NEC
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imejiridhisha kuwa uamuzi wa
kuvihamisha vituo 21 vya kupigia kura katika Kata ya Mbweni, jimbo
la Kawe katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, umezingatia
Sheria na Kanuni za Uchaguzi.
NEC imetoa msimamo huo, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa
baadhi ya wananchi na vyama vya siasa wakilalamika kuwa Tume ya
uchaguzi imehamisha vituo vinane (8) vya kupigia kura na kuvipeleka
kwenye Kituo cha Polisi, hatua waliyoeleza kuwa ni kuwanyima haki
wapiga kura katika kutimiza haki ya msingi.
Malalamiko mengine yaliyoifikia NEC ni kwamba Tume ilivihamisha
vituo vingine 15 kutoka maeneo ya awali na kuvipeleka maeneo
mengine jambo ambalo baadhi ya vyama havikukubaliana na uamuzi
huo.
Kutokana na malalamiko hayo, jana Jumanne Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani akiambatana na watendaji
wengine wa Tume, walitembelea maeneo hayo na kujiridhisha kuwa
mabadiliiko ya vituo yaliyofanywa na msimamizi wa uchaguzi
yamekidhi matakwa ya kisheria.
“Nimefika hapa jimbo la Kawe kata ya Mbweni, baada ya mwananchi
mmoja kunitumia ujumbe akiniambia kuwa kuna chama kimoja
kinachoshiriki Uchaguzi Mdogo wa Madiwani wa Kata ya Mbweni
kinalalamika kwamba Tume imehamisha vituo vya kupigia kura
kiholela,” alisema Ramadhani.
Mkurugenzi wa Uchaguzi aliongeza kuwa, chama hicho kimelalamika
kuwa vituo hivyo vimepelekwa kwenye eneo la kituo cha Polisi, kwa
hiyo huenda wapigakura wakanyimwa haki yao ya kupiga kura.
Alisema alipowauliza watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya
Kinondoni, majibu yao hayakumridhisha ndipo alipoamua kufika eneo
la tukio.
“Kwanza wanalalamika kwamba vituo vilivyohamishwa ni 27, lakini
ukweli ni vituo 21, vituo hivyo vimehamishwa kwa mujibu wa Sheria
kwa sababu Novemba mosi 2017, Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya
Kata aliviita vyama vinne na kufanya mkutano na aliwaambia
tunavihamisha vituo hivyo kwa sababu mbalimbali.
“Sababu alizozitoa msimamizi wa uchaguzi ni kwamba vituo vinane
vilikuwa shule ya Sekondari New Era na vituo saba7 vilikuwa jirani na
nyumbani kwa mgombea ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa
na vituo sita vilikuwa kwenye eneo la Kanisa,” alifafanua Kailima.
Alibainisha kuwa kifungu cha 20 (2) cha Kanuni za Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura za Mwaka 2015 na Kifungu cha 21
cha Kanuni za Uchaguzi Mkuu wa 2015, vinabainisha kuwa vituo vya
kupigia kura havipaswi kuwa kwenye maeneo ya watu binafsi,
kwenye maeneo ya ibada na kwenye kambi za jeshi.
Kutokana na msingi wa kanuni hizo, Kailima alithibitisha kuwa uamuzi
wa kuvihamisha vituo hivyo kwenye maeneo hayo ambao
umefanywa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Kawe ulikuwa
sahihi.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambaye
ndiye Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Kawe ilipo kata ya
Mbweni, Aron Kagurumjuri alisema malalamiko kuhusu kuhamishwa
kwa vituo hivyo yalitolewa na chama kimoja kati ya vyama vinne
ambavyo vitashiriki kwenye uchaguzi mdogo wa diwani wa kata hiyo.
Alisema Uchaguzi mdogo wa kata hiyo unafanyika baada ya
mahakama kutengua uchaguzi wa awali kutokana na ukiukwaji wa
baadhi ya taratibu za Uchaguzi.
“Tuko hapa kwa sababu chama kimoja kati ya vyama vinne
vinavyoshiriki Uchaguzi huu mdogo, kulalamika kwamba
tumehamisha vituo na kuvipelekea kwenye maeneo ambayo sio rafiki
kwa wapiga kura,” alisema Kagurumjuri.
Alifafanua kuwa hali halisi inaonesha kwamba kanuni na taratibu za
kupigia kura, haziruhusu kuweka kituo kwenye jengo la mtu binafsi,
na shule hiyo ambayo ilikuwa na vituo kadhaa ni shule ya mtu binafsi.
“Kwa hiyo kwa Uchaguzi huo wa mwakaa 2015 kanuni hizo zilikiukwa
sasa kwa uchaguzi huu kwa sababu tunataka tufanye Uchaguzi kwa
kufuata kanuni na sheria hatukutaka kuingia kwenye uvunjaji wa
kanuni na taratibu,”
“Baada ya kuhamisha vituo na kuvipeleka eneo hilo, ikazua
sintofahamu kwa chama kimoja na vyama vitatu vilivyoridhia ambapo
tulikuwa na mashaka inawezekana kilifaidika na vituo kuwepo
maeneo hayo,” alisema.
Kagurumjuri alisema vituo vingine vimehamishiwa kwenye eneo la
wazi na lenye usalama zaidi kwa wapiga kura pamoja na vitu vingine,
na kwamba wanaona halina shida.
No comments:
Post a Comment