SERIKALI imetumia kiasi cha Sh. Mil 728
kuwalipa amana zao wateja zaidi ya 695 wa Benki ya FBME ambayo Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) imeifutia leseni ya kufanya shughuli za kibenki hapa nchini.
Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu maswali
ya Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Rukia
Kassim Ahmed (CUF), aliyetaka kufahamu, pamoja na mambo mengine, hatma ya
wateja wa Benki hiyo baada ya kufutiwa leseni yake ya kujihusisha na masuala ya
kibenki Mei 8, 2017.
Mhe. Ahmed alitaka kufahamu msimamo wa
Serikali endapo fedha za kuwalipa wateja hao zinazotokana na kuuza mali, makusanyo
ya madeni na fedha zilizowekezwa kwenye taasisi nyingine na Benki hiyo
hazitatosha.
Aidha, alihoji kuhusu uamuzi wa Bodi ya
Akiba ya Amana ambao unaeleza kuwa hata kama mteja aliweka amana yake kwa fedha
za kigeni katika benki hiyo, watalipwa kwa fedha za kitanzania kwa kiwango
kilichokuwepo wakati Benki hiyo inafilisiwa Mei 8, 2017.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji alisema kuwa malipo ya wateja yanalipwa
kutokana na sheria ya mabenki na Taasisi za fedha ya mwaka 2006 kifungu cha 39,
na kwamba kinachofanyika hivi sasa ni utekelezaji wa sheria hiyo.
“Serikali
haina mpango wa kumuonea mteja yoyote, madeni yatakusanywa na fedha zitalipwa kwa kila mteja kulingana
na amana alizojiwekea, Serikali inalisimamia jambo hilo kwa umakini wa kiwango cha juu.” alisema Dkt.
Kijaji.
Katika swali lake la msingi Mhe. Rukia
Kassim Ahmed (CUF), alitaka kujua hatma ya wateja walioweka fedha zao katika
Benki ya FBME, baada ya Benki Kuu ya Tanzania kuifutia leseni ya kufanya
shughuli zake za kibenki na kuiweka chini ya ufilisi wa Bodi ya Bima ya Amana kuanzia
Mei 8, 2017.
Akijibu swali hilo Dkt. Kijaji alisema
kuwa hatua ya kwanza kwa mujibu wa sheria ni malipo ya fidia ya Bima ya Amana
ya kiasi kisichozidi Sh. 1,500,000 kutegemea na kiasi cha salio la amana wakati
beki inafungwa.
“Fedha za kulipa fidia hiyo zinatoka
katika Mfuko wa Bima ya Amana (Deposit Insurance Fund) unaosimamiwa na Bodi ya
Bima ya Amana (Deposit Insurance Board (DIB))” alisema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa wateja
waliokuwa na amana zisizozidi kiwango cha juu cha fidia cha Sh. 1,500,000
wakati benki inafungwa watapata fedha zao zote.
“Kiasi kitakachozidi kiwango hicho kitalipwa
kutegemea kiasi cha fedha kitakachopatikana kutokana na mauzo ya mali,
makusanyo ya madeni na fedha zilizowekezwa katika Taasisi nyingine”.alisema
Dkt. Kijaji.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
No comments:
Post a Comment