Wednesday, November 15, 2017

Serikali kuzindua Ripoti ya Utafiti wa Kitaifa wa Matokeo ya UKIMWI 2016/17

Serikali inatarajia kuzindua Ripoti ya Utafiti wa Kitaifa wa Matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016/2017 katika Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani Desemba Mosi mwaka huu Jijini Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa na Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge, Sera, Kazi Vijana, Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama leo mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Siku ya Maadhimisho ya UKIMWI Duniani.

"Hii ni ripoti muhimu sana inayotokana na utafiti ambao huwa unafanyika kila baada ya miaka minne, ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2003/2004 ni taarifa ambayo husaidia kuonesha hali halisi ya maambukizi ya VVU kwa watu wa marika mbalimbali pamoja na mapendekezo ya kisera namipango ya kudhibiti UKIMWI nchini," amesema Mhe. Mhagama.

Aidha, amesema kuwa maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani yenye kaulimbiu "Changia mfuko wa maisha, Tanzania bila Ukimwi inawezekana" yatatoa fursa ya kutathimini hali halisi na mwelekeo wa udhibiti UKIMWI Kitaifa na Kimataifa ikiwemo kutafakari changamoto, mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya kudhibiti UKIMWI.

" Siku hii pia hutoa nafasi ya kuwakumbuka wale wote waliopoteza maisha yao kutokana na UKIMWI, kuwaenzi wale waliojitokeza na kutoa mchango wao katika kudhibiti UKIMWI, pamoja na kuwajali yatima waliotokana na vifo vinavyohusiana na ugonjwa wa UKIMWI" ameongeza Jenista Mhagama.

Pia amesema kuwa, lengo lingine ni kutafakari na kutekeleza kitaifa na kimataifa kauli mbiu inayotolewa kila mwaka kulingana na vipaumbele vya kidunia, kikanda na kitaifa.

Aidha, Mhe. Mhagama amebainisha baadhi ya matukio makuu yatakayoambata katika maadhimisho hayo ni Kongamano la Kitaifa la kutathimini hali na mwelekeo wa udhibiti UKIMWI nchini litakalofanyika kati ya tarehe 28 hadi 29 Novemba mwaka huu jijini Dar es Salaam ambalo litajadili mawasiliano ya utekelezaji wa afua za ukimwi nchini ili kujua mahali tulipotoka, tulipo na tunakoelekea.

Vilevile amesema kuwa, katika maadhimisho hayo kutakuwa na uzinduzi wa Mkakati/ Mwongozo wa Taifa wa Afua za Matumizi ya kujikinga na VVU ambao utafanyika tarehe 27 mwezi huu.

"Katika Maadhimisho hayo kutakuwepo na maonesho ya shughuli za wadau wa udhibiti UKIMWI nchini yatakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 24 Novemba mwaka huu yakijumiisha huduma mbalimbali na utoaji elimu na burudani kwa wananchi ikiwemo huduma za upimaji wa hiari wa VVU na ushauri nasaha, upimaji wa shingo ya kizazi, sukari, uzito, damu na elimu kupitia vikundi vya sanaa na burudani" amefafanua Mhe. Mhagama.

Mbali na hayo, Jenista Mhagama amesema kuwa, katika maadhimisho hayo Serikali itafaya uhamasishaji wa Mfuko wa Fedha za Kudhibiti Ukimwi nchini kupitia matembezi ya hisani tarehe 25 Novemba na pia chakula cha jioni maalumu kwa kuchangia mfuko huo Desemba Mosi.

Hata hivyo, Waziri Jenista ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo ili kupata huduma mbalimbali zitakazotolewa ikiwemo upimaji wa hiari wa VVU na ushauri nasaha.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI TACAIDS Dkt. Leonard Maboko amewahamasisha wananchi na wadau mbalimbali kuchangia Mfuko wa kudhibiti Ukimwi kwa kushiriki Marathoni, kuchangia kupitia kununua tshirt kwa shilingi 20,000 na pia kuchangia kwa hiari kupitia namba 0684 909090.

No comments: