Friday, November 17, 2017

SERIKALI YAAGIZA USHIRIKIANO KATI YA TSC, IDARA YA ELIMU NA WAKAGUZI WA SHULE ILI KUBORESHA ELIMU

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. George Joseph Kakunda anayeshughulikia Elimu, Maji, Kilimo, Mifugo na Maliasili, amefungua Mkutano wa kwanza wa kazi kwa Kaimu Makatibu Wasaidizi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) katika ukumbi wa chuo cha Mipango mjini Dodoma leo.

Mkutano huo ni wa kwanza tangu kuanzishwa kwa Tume ya TSC mwaka 2015, ambao hutakiwa kufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa malengo mbalimbali likiwemo kupitia kanuni, sheria na taratibu za Tume hiyo.

Akifungua kikao kazi hicho mjini Dodoma, ameagiza kuwepo kwa ushirikiano baina ya TSC, Idara ya Elimu na Wadhibiti Ubora wa Elimu (Wakaguzi) ngazi ya wilaya bila kuwepo kwa muingiliano wa majukumu ili kuinua kiwango cha elimu nchini badala la kuendelea kubishana na kuingiliana katika majukumu yao.

“Kuanzia sasa naagiza Maafisa Elimu wa Wilaya wote nchini, Wadhibiti wa Ubora kote nchini na Makatibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu katika Halmashauri zote nchini; kwamba ushirikiano wa kikazi ni jambo la lazima kwenu vinginevyo tutaendelea kudidimiza Ubora wa Elimu nchini”

Mhe. Kakunda amewaasa Wajumbe wa Mkutano huo kuendeleza mafanikio ambayo Tume mpya ya TSC imeyapata kwa kipindi kifupi cha mwaka mmoja kama kusimamia vema mikataba ya ajira za waalimu wanapoanza kazi, kwani ndio maisha yao.

“Mnapowasainisha mikataba ya kudumu ya kazi walimu wapya yenye masharti ya pensheni, tambueni kwamba, walimu wanaithamini sana mikataba hiyo kwa sababu licha ya kuhakikishia walimu uhakika wa ajira, mikataba hiyo huwaongoza walimu jinsi wanavyotakiwa kujiheshimu kazini ikiwa ni pamoja na kuainisha baadhi ya maadili yao kazi”

Aidha, amewataka wajumbe kutumia kanuni ya kuwathibitisha walimu kazini ndani ya mwaka mmoja bila kusubiri malalamiko ya walimu. “walimu wote wanaotimiza masharti yanayoonesha kuwa wameweza kutekeleza majukumu yao kwa ustadi na weledi unaotakiwa, wathibitisheni kazini ndani ya muda usiozidi miezi 12”,

Katika hatua nyingine, Mhe. Kakunda ameiagiza TSC kuwachukulia hatua wale wote watakaochelewesha kuwathibitisha walimu bila sababu za msingi, “nataka kuona hatua hatua zikichukuliwa dhidi ya wote ambao kwa namna moja au nyingine watachelewesha kuwathibitisha kazini walimu kwa muda mrefu bila sababu za msingi” Pia amewaasa wajumbe kusimamia vema suala la kuwapandisha madaraja walimu kwa mujibu wa kanuni ili kuondoa malalamiko na manung’uniko na kuongeza ufanisi wa kazi.

Lakini pia, Mhe. Kakunda ameshauri Kitengo cha Sheria katika Tume ya TSC Makao Makuu iwe Kurugenzi ya Sheria (Idara kamili) kutokana na umuhimu wa kazi za Tume kama Mamlaka ya Nidhamu.

Naye Katibu Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Winfrida Rutaindurwa, amesema Tume hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi kifupi tangu kuanzishwa kwake, kwa sheria namba 25 ya mwaka 2015, ikiwa ni pamoja na kuandaa Mpango Mkakati wa Tume kwa miaka mitano 2017/18 hadi 2021/22, kufunga mtambo wa malipo ya mishahara na upatikanaji wa taarifa muhimu za watumishi kwa wakati.

Amesema Tume pia imeweza, “kuandaa bajeti ya matumizi ya kawaida na mishahara wa Tume kwa mwaka 2017/2018, kutengeneza barua pepe za Serikali kwa ajili ya Watumishi wa Tume Makao makuu, kutengeneza tovuti ya Tume, kujiunga na Mkongo wa Taifa kutoka TTCL na kuratibu madai ya Watumishi ya likizo, kusafirisha Wastaafu, gharama za matibabu na posho za kujikimuambayo yaliwasilishwa kwa Mwajiri wa zamani ambayo ilikuwa ikiitwa Tume ya Utumishi wa Umma”

Rutaindurwa amesema pamoja na mafanikio zipo baadhi ya changamoto zinazoikabili Tume ya TSC ambazo ni ufinyu wa bajeti unaopelekea kutofanya uteuzi wa Viongozi wa ngazi ya Wilaya ambao ni Makatibu Wasaidizi, uhaba wa Ofisi za Tume ngazi ya Makao Makuu na Wilaya, upungufu wa vitendea kazi na samani Makao makuu na Wilayani.

Changamoto nyingine ni upungufu wa watumishi unaozorotesha utendaji wa Tume hiyo, “upungufu wa watumishi wa kada mbalimbali wilayani na makao makuu. Wanaopaswa kuwepo ni watumishi 775”na waliopo ni 417 na upungufu uliopo ni watumishi 358.

Aidha, amesema baadhi ya ofisi za TSC  katika mikoa na Halmashauri zisizo na Wakuu wa Wilaya zimeondolewa na kusababisha kupungua kwa ufanisi kwa ofisi za Tume ngazi ya Makao makuu na wilaya 139, ikiwa ni kutokana na ukosefu wa usimamizi wa karibu katika ngazi za mikoa.

Rutaindurwa amesema TSC inarajia kukamilisha zoezi la uteuzi wa Viongozi wa wilaya kabla ya kuisha kwa mwaka wa fedha 2017/18, kufuatilia mabadiliko ya muundo wa TSC ili kukidhi mahitaji yake, kutafuta uwezeshaji wa kuboresha mawasiliano ya kielektroniki makao makuu na wilayani, na pia kuandaa mazingira ambayo TSC itaongezewa bajeti kwani inahudumia watumishi zaidi ya asilimia 55 wa Serikali. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya TSC, Oliva Mhaiki amesema, tangu kuanzishwa kwa TSC mwaka 2015 na kuanza kazi mwaka 2016,  “Tume ilianza kushughulikia mashauri ya kawaida, lakini kutokana na wingi wa mashauri, tuliona tuyarudishe wilayani na kama Tume tumeona tujikite na mashauri ya rufaa”.

Kikao kazi cha Tume ya Utumishi wa Walimu ni cha siku mbili ambacho ni kikao cha kwanza tangu kuanzishwa kwa TSC mwaka 2015, kabla ya hapo ilikuwa ni Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ilivunjwa na kuanzishwa kwa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC).
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Joseph Kakunda anayeshughulikia Elimu, Maji, Kilimo, Mifugo na Maliasili akielekea kwenye ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma kwa ajili ya kufungua kikao kazi cha Makaimu Makatibu TSC Wasaidizi mjini Dodoma kushoto kwake ni Katibu Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Winfrida Rutaindurwa na kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya TSC, Oliva Mhaiki.
 Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Joseph Kakunda anayeshughulikia Elimu, Maji, Kilimo, Mifugo na Maliasili akitoa hotuba wakati wa  kufungua kikao kazi cha Makaimu Makatibu TSC Wasaidizi katika chuo cha Mipango mjini Dodoma, kushoto kwake ni Katibu Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Winfrida Rutaindurwa, Katibu wa Tume ya TSC Dodoma Manispaa na kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya TSC, Oliva Mhaiki. 
Baadhi ya Washiriki wa kikao kazi cha Makaimu Makatibu TSC Wasaidizi wa Wilaya 139 nchini, wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi Mhe. Kakunda hayupo pichani katika chuo cha Mipango mjini Dodoma.

Katika picha ya pamoja waliokaa, katikati ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Joseph Kakunda anayeshughulikia Elimu, Maji, Kilimo, Mifugo na Maliasili kushoto kwake ni Katibu Tume ya Utumishi wa Walimu Tanzania (TSC), Winfrida Rutaindurwa na kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya TSC, Oliva Mhaiki.

No comments: