Friday, November 17, 2017

MWENYEKITI WA ALAT NA MEYA WA MANISPAA YA SHINYANGA ATOA MSAADA WA PAMPU YA MAJI KATA YA CHIBE

Mwenyekiti wa Jumuiya ya serikali za mitaa nchini Tanzania (ALAT) na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam ametoa msaada wa pampu ya maji na mifuko 10 ya saruji vyenye thamani ya shilingi milioni 2.5 kwa ajili ya kumaliza tatizo la maji katika kitongoji cha Mwamapalala kata ya Chibe katika manispaa ya Shinyanga. 

Mukadam amekabidhi msaada huo wa pampu ya maji na mifuko ya 10 ya saruji kwa diwani wa kata ya Chibe John Kisandu leo Ijumaa Novemba 17,2017 kwa ajili ya mradi wa maji katika mtaa wa Mwamapalala katika kata hiyo ambayo inakabiliwa na kukosekana kwa huduma ya maji. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo,Mukadam alisema hivi karibuni alitembelea kata ya Chibe,ndipo diwani wa kata hiyo akaomba msaada wa kutafutiwa pampu ya maji baada ya wananchi kujitolea kuchimba kisima kirefu. 

“Kutokana na ombi hilo,nimetafuta wafadhili na kupata msaada huu kutoka kwa Farana Hirji aliyenipatia fedha kwa niaba ya Roshan Chatur nikanunua pampu hii na saruji hii itakayotumika kukamilisha ujenzi wa kisima”,alieleza Gulam. 

“Kupitia msaada huu wananchi wa Chibe watapata huduma ya maji safi na salama kwani mhandisi wa maji wa manispaa amefika katika kisima hicho na kutuhakikishia kuwa maji hayo ni salama kwa matumizi ya binadamu”,alisema Mukadam. 

Hata hivyo alisema aliwataka wadau kuendelea kushirikiana na serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kama vile maji,afya na elimu. Naye Kaimu katibu mkuu ALAT,Abdallah Ngodu ambaye yupo katika ziara kutembelea halmashauri mbalimbali nchini,alimpongeza Gulam kwa jitihada anazochukua katika kumaliza kero za wananchi. 

“Lengo la ALAT ni kuhakikisha tunatatua kero za jamii ambazo nyingi zipo katika sekta ya maji,afya na elimu,hivyo kwa kushirikiana na serikali tutaendelea kutatua changamoto hizi”,alisema Ngodu. 

Naye Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga,Rajabu Masanche alikiri kuwepo kwa changamoto za maji katika manispaa hiyo hivyo kuwaomba wadau kujitokeza kusaidia huku akiwataka wananchi kutunza miundombinu ya maji. 

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Chibe,John Kisandu alimshukuru Mukadam kwa kumpatia msaada huo ambao utakuwa msaada kwa wananchi hao ambao wanakabiliwa na tatizo la maji. 

“Kata ya Chibe ina wakazi zaidi ya 3,000 na kuna mitaa minne ambayo ni Busambilo,Chibe,Mwalugoye na Mwamapalala,mitaa yote ina shida ya maji,wananchi wa Mwamapalala walijitolea kuchimba kisima nikamuomba mheshimiwa Gulam atupatie msaada wa pampu na leo ametupatia,tunamshukuru sana”,alieleza Kisandu. 
Zoezi la kushusha pampu ya maji kwenye gari likiendelea wakati Mwenyekiti wa Jumuiya ya serikali za mitaa nchini Tanzania (ALAT) na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam akikabidhi pampu ya maji na mifuko 10 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa kisima kirefu cha maji katika kata ya Chibe manispaa ya Shinyanga- Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog 
Kaimu Mhandisi wa maji manispaa ya Shinyanga Nkinda Seni (wa nne kushoto) akishusha mabomba ya pampu ya maji.Katikati ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya serikali za mitaa nchini Tanzania (ALAT) na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam 
Mwenyekiti wa Jumuiya ya serikali za mitaa nchini Tanzania (ALAT) na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam akizungumza wakati wa kukabidhi pampu ya maji na mifuko ya saruji kwa diwani wa kata ya Chibe John Kisandu kwa ajili ya ujenzi wa kisima kirefu katika mtaa wa Mwamapalala. Kushoto ni pampu ya maji na mifuko ya saruji. 
Mwenyekiti wa Jumuiya ya serikali za mitaa nchini Tanzania (ALAT) na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam akishikana mkono na diwani wa kata ya Chibe John Kisandu wakati wa akikabidhi pampu ya maji na mifuko ya saruji.Wa kwanza kulia ni Kaimu katibu mkuu ALAT,Abdallah Ngodu na Kaimu Mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga,Rajabu Masanche wakishuhudia zoezi la makabidhiano. 
Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mhandisi wa maji manispaa ya Shinyanga Nkinda Seni na Katibu tawala wilaya ya Shinyanga,Boniface Chambi wakishuhudia tukio la makabidhi 
Kaimu katibu mkuu ALAT,Abdallah Ngodu akimpongeza Mwenyekiti wa Jumuiya ya serikali za mitaa nchini Tanzania (ALAT) na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam (kushoto) kwa kutoa msaada wa pampu ya maji katika kata ya Chibe katika manispaa ya Shinyanga. 
Kaimu katibu mkuu ALAT,Abdallah Ngodu akishikana mkono na diwani wa kata ya Chibe,John Kisandu.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

No comments: