Wednesday, November 29, 2017

Mahakama yapokea maelezo ya onyo ya anayedaiwa kuwa malkia watembo.

Na Karama Kenyunko blogu ya jamii.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepokea maelezo ya onyo ya mshtakiwa Yang Feng Glan anayedaiwakuwa malikia wa tembo, ambayo yatatumika kama moja ya kielelezo katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Glan ambaye ni raia wa China na watanzania wawili.

Maelezo hayo yamepokelewa na hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi anayesikiliza kesi hio.Kabla ya kupokelewa,askari Polisi wa kikosi kazi cha taifa cha kupambana na ujangili, E.1180 Koplo Emmanuel alieleza kuwa alitumia masaa mawili kuchukua maelezo ya onyo ya mshtakiwa katika Kituo cha Polisi cha Osterbay.

Koplo Emmanuel alidai hayoleo alipokuwa akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu,Faraja Nchimbi kutoa ushahidi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi.

Amedai,Septemba 27,2015 majira ya usiku alipigiwa simu na kaimu DCI akimtaka afike Polisi Osterbay ambapo alipofika hapo alimkuta mshtakiwa Yang Feng akituhumiwa kwa kujihusisha na tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo na kutakiwa amfanyie mahojiano.

Alidai katika mahojiano mshtakiwa alijitambulisha kwa jina la Yang, akamuuliza kama anatambua kosa lake na kwamba,Yang alimueleza kuwa anatuhumiwa na kujihusisha na nyara za Serikali ambazo ni meno ya tembo.

Baada ya kumueleza Haki zake za msingi ikiwamo kuwa ana Haki ya kuwa na ndugu, jamaa ama rafiki kama shuhuda wakati akitoa maelezo na yeye akaomba awepo jamaa yake Manfred Lyoto.

Alidai baada ya kutafutwa huyo Lyoto alidai kuwa na udhuru lakini ilipofika asubuhi ya Septemba 28,2015 Lyoto alikwenda kituoni hapo asubuhi na ndipo mshtakiwa akachukuliwa maelezo ya onyo kuanzia saa 2:00 asubuhi kwa mfumo wa kujieleza hadi saa 4:30 asubuhi.

Alidai kipindi chote hicho, Lyoto alikuwa akishuhudia maelezo ambayo Yang alikuwa akiyatoa kwa lugha ya kiswahili na alikuwa na afya njema na amani.Aliongeza kudai kuwa baada ys Yang kutoka maelezo yake na yeye kuwa anaandika,alimpatia ayasome na akamueleza hapo sahihi na Lyoto pia na wote kwa pamoja wakaweka saini zao kwenye kurasa 14 za maelezo hayo zilizopo kwenye karatasi saba.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa kesho kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Salvius Matembo na Philemon Manase ambao kwa pamoja, wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22,2014 walijihusisha na biashara ya nyara za serikali.

Washtakiwa hao wanadaiwa kufanya biashara ya vipande 706 vya meno ya Tembo vyenye uzito wa kilogramu 1889 zenye thamani ya Sh bilioni 13 bila ya kuwa na leseni iliyotolewa na Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

No comments: