Thursday, November 2, 2017

KUCHELEWA KUTOA FEDHA ZA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA WANANCHI KWASABABISHA MWEKAHAZINA WA KALIUA KUKALIA KUTI KAVU

NA TIGANYA VINCENT

KUCHELEWA kupelekwa fedha ambazo zilitakiwa kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi ili waweze kukamilisha Mradi wao wa Ujenzi wa jengo la Mashine ya Usindikaji wa Mafuta katika Kijiji cha Kombe umesababisha Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kupewa wiki mbili kuhakikisha fedha hizo zinafika haraka la sivyo atakuwa amejiundoa kazini mwenyewe.

Msimamo huo umetolewa jana wilayani Kaliua na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri wakati alipotembelea Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Mashine ya kukamulia mafuata ya alizeti ambao umekwama kumalizika kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya Halmashauri kuchelewa kupeleka fedha ambazo ilitakiwa itoe.

Alisema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wananchi wamejituma kujenga jengo kwa ajili ya kuweka mashine ya kusindika mafuta ya alizeti lakini  Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua hadi hivi sasa hajitoa milioni 4 zilizotakiwa kuunga mkono nguvu za wananchi hao.

 Aidha Mwanri aliongeza kuwa pia kiasi kingine ni zile milioni 17 zilizotolewa na Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Miombo kwa ajili shughuli mbalimbali kama vile ufugaji kuku, kilimo cha uyoga, ufugaji nyuki zimekwama kupelekwa kwa walengwa kwa sababu ya Ofisi ya Uhasibu ya Halmashauri hiyo kuchelewesha wakati Wilaya nyingine zimeshapeleka kwa walengwa na kuanza kufanyakazi. Alisema kuwa hawezi kumvumilia mtumishi wa sampuni hiyo ambaye ameshindwa wa kutumia fedha miradi kwa wakati ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi katika kuwainua kiuchumi na kuwaletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla kwa sababu ya urasimu usio na maana kwani kufanya hivyo ni kuwakatisha tamaa.

Mwanri alisema kuwa ndani ya wiki mbili mbili anataka kupata majibu ya hatua ambazo zimefikiwa katika kuhakikisha kuwa fedha hizo za mradi endelevu wa miombo zimeshapelekwa eneo husika na Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua imeshawakabidhi wananchi hao milioni 4 ili wamalizie  jengo la mashine yao.

Mwanri alisema kuwa kinyume cha hapo wahusika wote watakuwa wamesbabisha mradi huo kutofanikiwa waanze kuondoka kwa hiari yao. Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa alitoa siku mbili kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kuhakikisha wanapeleka taarifa ya miradi yote inayotekelezwa na gharama zake na muda wa kukamilisha mradi. Alisema kuwa hatua hiyo inataka kufanya Ofisi yake kuwa na uhakika wa thamani halisi ya fedha na ubora wa mradi ili kuona kama kweli utawanufaisha wananchi.

 Naye Mratibu wa Mradi wa Miombo Wilayani Kaliua Bennett  Kamara alisema kuwa taratibu zote za kuhakikisha kuwa fedha zilizotolewa na miombo zinatolewa na Mkurugenzi Mtendaji ili ziunge mkono juhudi za wananchi zilishakamilika muda mrefu  lakini kwa muda mrefu fedha hizo bado ziko ofisi ya Uhasibu.

 Kwa upande wa Katibu Tawala Msaidizi Dkt. Philip Ntiba alitoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua kutoa haraka fedha mapema ili kuwakatisha tamaa wananchi waliojitolea nguvu zao kuanzisha mradi huo.

No comments: