Na Karama Kenyunko, Glogu ya Jamii.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya jinai (DPP) ameomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwapa siku 14 ili kukamilisha utaratibu wa kupeleka taarifa za kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya USD 527,540, Mahakama kuu.
Kesi hiyo inawakabili vigogo wa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco), Benhardard Tito aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Mwanasheria wa Rahco, Emmanuel Massawe na mfanyabiashara ambaye pia ni mwakilishi wa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Maghela Ndimbo amewasilisha ombi hilo leo Novemba 2, 2017 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa
Kufuatia maelezo hayo, Hakimu Simba ametoa ahirisho la mwisho na kuwaeleza upande wa mashtaka kuwa ataifuta kesi hiyo kwa kiwango ambacho washtakiwa hao hawatakamatwa tena.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 16, mwaka huu.
Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka nane ya uhujumu uchumi likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka, kula njama na kusababisha hasara ya USD 527,540.
Washtakiwa hao wadaiwa kuwa kati ya Septemba Mosi, 2014 na Septemba 30, 2015 kwa nia ya kutenda kosa walikula njama kinyume cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Tito, anadaiwa kuwa Februari 27, 2015 katika ofisi za Rahaco zilizopo Ilala alitumia madaraka yake vibaya kwa kuiajiri Kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd kama mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya Rahaco.
Tito na Massawe wanadaiwa kuwa Machi 12, 2015 wakiwa katika nyadhifa zao, walisaini barua ya kuihalalisha kampuni hiyo ya Afrika Kusini kuwa mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati na kutoa huduma za ushauri wa kifedha kuhusu mradi huo.
Aidha washtakiwa hao wanadaiwa kuwasilisha mkataba wa huduma ya ushauri kati ya kampuni hiyo ya Afrika Kusini na Rahaco.
Pia wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kusaini mkataba wa kutoa huduma za ushauri na kampuni ya Afrika Kusini bila ridhaa ya Bodi ya Zabuni ya Rahaco na kushindwa kuwasilisha mkataba walioingia na kampuni ya Afrika Kusini kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha wanaodaiwa kati ya Machi mosi na Septemba 30, 2015 katika ofisi za Rahaco, waliipa kazi kampuni hiyo ya ushauri na kuilipa kwa kutoa huduma za ushauri, malipo ambayo yaliisababishia Rahaco kupata hasara ya dola za Marekani 527,540.
Tito anadaiwa kuwa, Agosti 18, 2015 katika ofisi za Rahaco Ilala, ambapo kwa kutumia madaraka yake vibaya aliipa Kampuni ya Ujenzi wa Reli ya China kazi ya kujenga kilomita mbili za reli maeneo ya Soga iliyogharimu dola za Marekani 2,312,229.39 bila idhini ya Bodi ya Zabuni ya Rahaco.
No comments:
Post a Comment