Thursday, November 30, 2017

FINLAND YAIPATIA TANZANIA MSAADA WA BILIONI 75 KUENDELEZA MISITU, MAFUNZO YA UONGOZI NA UBUNIFU

Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania na Finland zimetiliana saini mikataba mitatu yenye thamani ya Euro milioni 28.8 sawa na Shilingi bilioni 75 kwa ajili ya kuendeleza misitu, ubunifu na masuala ya uongozi.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa mikataba hiyo, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James amesema, msaada huo kutoka Finland umetolewa ili kuendeleza  uwezo wa viongozi na kufanya maamuzi sahihi yenye tija kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa, mradi ambao unasimamiwa na Taasisi ya Uongozi, ambapo kiasi cha Euro milioni 9.90 zimetolewa kuendeleza mradi huo.

Aidha Serikali ya Finland imetoa kiasi cha Euro milioni 8.95 kwa mradi wa  kuiimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kutengeneza mazingira rafiki kwa wabunifu ili kuweza kubuni na kuendeleza ubunifu wao na kuchochea ukuaji wa viwanda. 

Bw. James alisema fedha hizo zitatumika kuwasaidia wabunifu kwa kuwapatia vifaa na msaada wa kitaalamu ili kuyaendeleza mawazo yao na kuyafanya yawe ya kibiashara na kuweza kusaidia kubadili mawazo hayo kuwa viwanda. 

“Fedha hizi zitasaidia kutatua changamoto katika viwanda vilivyopo nchini ili vifanye kazi kwa ufanisi kwa kuwaunganisha wanataaluma mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na wabunifu wachanga, wataalamu kutoka vyuoni, wataalamu kutoka Serikalini na Sekta binafsi” Alisema Bw. Doto James

Eneo lingine lililonufaika na msaada huo ni programu ya misitu, ambayo imepatiwa Euro milioni 9.95 kwa lengo la utuzaji wa misitu na uongezaji thamani ya mazao yatokanayo na misitu ili kuongeza kipato kwa Wananchi, kupunguza umasikini na kulinda mazingira.

Katibu Mkuu amemshukuru balozi wa Finland Nchini, Mhe. Pekka Hukka kwa msaada walioutoa na kwa kuunga mkono shughuli za maendeleo za Serikali, na kuongeza kuwa Finland wamekuwa wakifadhili miradi mbalimbali nchini, ukiwemo mradi wa kilimo biashara Mkoani Lindi na Mtwara (LIMAS), uliogharimu Euro milioni 9, Mradi wa kuimarisha usambazaji na upatikanaji wa umeme wa uhakika Jijini Dar es Salaam, uliogharimu Euro milioni 25, na Programu ya maboresho ya Serikali za Mitaa, Euro milioni 10.5

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Profesa Joseph Semboja aliiishukuru Serikali ya Finland kwa kuendelea kuisaidia Taasisi hiyo.
‘Hii ni mara ya tatu Finland wamekuwa wakitusaidia kuendeleza jitihada zilizoanzishwa na Serikali yetu ambapo awamu ya kwanza ilikuwa ni mwaka 2012 ambapo walitupatia Euro milioni 7, mwaka 2014 Euro milioni 12 na sasa wametupatia Euro milioni 9.90 huu ni msaada mkubwa’ alisema Profesa Semboja.

Aidha kwa upande wake Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano na Serikali yake, na kuongeza kuwa msaada huo ni muhimu sana katika kutimiza malengo ya maendeleo ya nchi.Amesema msaada huo ukitumika ipasavyo hasa katika kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya misitu utasadia kuongeza ajira na kuongeza pato la Taifa.

Ameitaka Serikali kupitia Wizara ya nishati,  kushirikiana na sekta binafsi na kuitumia fursa hiyo ya kuboresha misitu ili kuiongezea nchi mapato zaidi yatakayotokana na makusanyo ya kodi.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) akionesha kalamu aliyozawadiwa na Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka (kushoto) ambayo imetengenezwa kwa mbao, akionesha uzalendo wa matumizi ya misitu. Kutoka kulia ni Kamishna wa Bajeti Wizara ya Fedha na Mipango Bibi. Mary Maganga na Kamishna wa Fedha za Nje Bw. John Rubuga.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James (kulia) akitia saini moja kati ya mikataba mitatu yenye jumla ya shilingi bilioni 75 kama msaada kwa Tanzania, Kushoto ni Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka kwa pamoja wakisaini mikataba hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) akibadilishana mkataba na Balozi wa Finland Bw.Pekka Hukka. Mkataba wa kwanza wa Euro milioni 9.9 ni kwa ajili ya kusaidia Taasisi ya Uongozi, wa pili wa Euro milioni 8.9 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa ubunifu na watatu wa Euro milioni 9.5 ni kwa ajili ya program ya misitu.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) pamoja na Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka (kushoto) wakionesha moja ya mikataba mara baada ya kumaliza kutia saini mikataba hiyo.
Mkuu wa Taasisi ya Uongozi Prof. Joseph Semboja (Kulia) akiishukuru Serikali ya Finland kwa kuwapatia msaada wa Euro milioni 9.9 ambayo itawasaidia kuendesha shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo. Kushoto ni Balozi wa Finland Bw. Pekka Hukka.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (katikati, waliosimama mbele) akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya hafla ya utiaji saini mikataba mitatu ya jumla ya shilingi bilioni 75. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments: