Thursday, November 30, 2017

CHINA YAAHIDI KUFADHILI UJENZI WA RELI KWA KIWANGO CHA KIMATAIFA (SGR)

Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
BALOZI wa China hapa nchini, Wang Ke amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari kushawishi taasisi za fedha ikiwemo Benki ya EXIM ya nchini humo kushiriki ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa baada ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu wa mradi huo.

Alisema kuwa kutokana na ukubwa wa mradi huo, unaokadiriwa utagharimu Dola za Marekani bilioni 7.6 hadi kukamilika kwake, utahitaji kufanyiwa upembuzi yakinifu ili kukidhi masharti ya kupata mkopo kupitia Benki ya Exim na taasisi nyingine zitakazotaka kujenga mradi huo muhimu. 

“Mradi huu ni muhimu na wa kihistoria kwa nchi hizi mbili, China ingependa kuona mradi huo unaboreshwa ili uweze kutoa huduma ya kusafirisha mizigo na abiria na kwamba kuimarika kwake kutaokoa miundombinu ya barabara kwa kuwa shehena kubwa ya mizigo itasafirishwa kupitia reli hiyo.

Aidha, Balozi Ke alisema kuwa nchi yake inasubiri pia kukamilika kwa taratibu za ndani kati yake na Tanzania ili mradi wa reli ya TAZARA uanze  ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria kati ya Tanzania na Zambia pamoja na nchi za maziwa makuu.

Balozi Ke alitumia fursa hiyo kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kukusanya kodi, kusimamia matumizi adili ya fedha za umma, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kupambana na rushwa.

Akizungumza mara baada ya mazungumzo na mgeni wake, Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango alisema kuwa Serikali imeridhia uamuzi wa China wa kufanya upembuzi yakinifu wa mradi huo wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR) ili China kupitia taasisi zake iweze kujenga sehemu ya mradi huo.

“Tayari mradi umeanza kujengwa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, kwahiyo kujitokeza kwa China kutaka kufadhili ujenzi wa mradi huo kutasaidia kukamilisha mradi huo muhimu kwa haraka na kwa wakati” Alisema Dkt. Mpango.

Alisema pia kuwa China imeonesha nia ya kusaidia kuujenga na kuupanga mji wa Dodoma kutokana na nchi hiyo kuwa na uzoefu wa kupanga miji ambapo nchi hiyo imeonesha nia ya  kujenga miundombinu ya elimu, barabara, uwanja wa ndege wa kimataifa-Msalato, kujenga mfumo wa maji safi na maji taka pamoja na majengo ya kisasa.

Kuhusu biashara, Dkt. Mpango alisema wamekubaliana kuwa China itaisaidia Tanzania kukuza kiwango cha biashara ambapo takwimu zilizoko zinaonesha kuwa urari wa biashara kati ya nchi hizo unaonesha kuwa Tanzania imekuwa ikinunua bidhaa nyingi kutoka nchini humo kuliko inavyo uza bidhaa na huduma zake.

“Mwaka 2016 Tanzania iliuza China bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za marekani milioni 460 wakati China iliuza hapa nchini bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.2, kiwango ambacho ni kikubwa karibu mara 5 ya kile tulichowauzia” Alisema Dkt. Mpango.

Ili kuvutia Sekta ya utalii, Tanzania imeiomba China kuanzisha safari ya ndege wa moja kwa moja kutoka China hadi Tanzania ili kuvutia watalii wengi kutoka nchini humo na kwamba utaratibu utafanyika ili Mamlaka ya usafiri wa anga iweze iratibu na kusaini makubaliano ya ushirikiano na hivyo kufanikisha jambo hilo.

“China imeandaa maonesho makubwa ya uwekezaji na biashara ya bidhaa na huduma mbalimbali mwezi Novemba, 2018, hivyo wafanyabiashara wa Tanzania pamoja na  Bodi ya Utalii nchini wahakikishe wanashiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo ili kutumia nafasi hiyo kujitangaza” Alisistiza Dkt. Mpango.

Aidha, Dkt. Mpango alieleza kuwa Balozi Wang Ke, amesema kuwa Nchi yake itashiriki katika ujenzi wa miradi ya bandari ili kukuza masuala ya usafiri kwa kuboresha bandari za Tanga, Bagamoyo, Kigoma, Bagamoyo, Dar es Salaam, Mtwara na katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.

Waziri huyo wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alitoa wito kwa wawekezaji kutoka China na nchi nyingine kuja kuwekeza nchini katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.

Miradi mikubwa ambayo China imewekeza na kufadhili hadi sasa hapa nchini ni Reli ya TAZARA, Kiwanda cha Urafiki, ujenzi wa barabara, majengo, ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara hadi dar es Salaam, Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere Jijini Dare Salaam, Ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na miradi mingine kadha wa kadha.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati),  Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke (wa pili kulia), Mwakilishi wa masuala ya Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China Bw. Lin Zhiyong (wa pili kushoto) pamoja na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango  wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya pande hizo kuhusu Biashara, uwekezaji na ushirikiano, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Kulia) na mgeni wake Bi. Wang Ke, wakitoka nje ya Jengo la Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao uliohusu masuala mtambuka ya ushirikiano kati ya Tanzania na China.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke,  wakiagana   baada ya kumalizika kwa Mkutano kati yao ambapo balozi huyo aliahidi kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi, kijamii na kiutamaduni kati nchi hizo mbili, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam. 
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kulia) akiagana na Mwakilishi wa masuala ya Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China  nchini Tanzania Bw. Lin Zhiyong baada ya kumalizika kwa Mkutano kati ya Waziri huyo na Balozi wa nchi hiyo Bi. Wang Ke (hayupo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
 Kamishina wa Fedha za Nje Bw. John Rubuga (kushoto) na Afisa anayeshughulikia masuala ya nje katika dawati la China Bw. Alfonce Mayala kutoka Wizara ya Fedha na Mipango wakifuatilia kwa makini majadiliano kati ya Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke,  na Waziri wa Fedha na Mipango (hawapo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), wa pili kulia akieleza kuhusu fursa zilizopo katika Sekta ya Utalii wakati wa  Mkutano kati yake na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke, (hayupo pichani), Jijini Dar es Salaam, kulia ni Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. John Rubuga.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), wa tatu kulia akiwa katika mkutano na  Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke (wa pili kushoto) ambapo walikubaliana kuendeleza ushirikiano katika Biashara na uwekezaji kwa manufaa ya pande hizo mbili, mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akieleza kuhusu kuwa na uwiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China kwa manufaa ya pande hizo mbili wakati wa mkutano kati yake na Balozi wa China nchini Tanzania Bi. Wang Ke, (hayupo pichani), Jijini Dar es Salaam.
 Balozi wa China hapa Nchini Bi. Wang Ke, (katikati) akiongoza maafisa wake wa ubalozi wa nchi hiyo hapa nchini wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China hapa nchini, Bi. Wang Ke, akisisitiza jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Jijini Dar es Salaam.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments: