Na: Frank Shija – MAELEZO
Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) kimeanzisha huduma ya Dawati la Mhasibu itayaofanyika kwa mara ya kwanza tarehe 07 Oktoba 2017 kuanzia saa 3: 00 asubuhi katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salaaam.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama hicho Dkt. Fred Msemwa alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusiana na huduma hiyo leo jijini Dar es Salaam.
Dkt. Msemwa amesema kuwa kupitia Dawati hilo wahasibu, wataalam wa kodi, fedha na biashara watajumuika pamoja na kukutana na wananchi wa kawaida, wafanyabiashara wadogo na wakubwa na kuwapatia huduma bure.
“Kupitia Dawati hili la Mhasibu litatukutanisha na wadau wengine wa masuala ya biashara na ujasiriamali hili kwa pamoja tuweze kutoa huduma za mbalimbali za kijasiriamali zianazohusisha masuala ya mahesabu bila ya malipo” alisema Dkt. Msemwa.
Alizitaja huduma zitakazotolewa kupitia Dawati hilo kuwa ni pamoja na jinsi ya kusimamia biashara endelevu, namna ya kuandika andiko kwa ajili ya kupata mikopo na elimu ya kodi.Huduma zingine ni mikataba ya biashara, usimamizi wa biashara za familia, utunzaji wa kumbukumbu za fedha ambapo huduma zote zitatolewa bila malipo yoyote na hakuna kiingilio.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Dyoya James ametoa wito kwa wanataaluma za uhasibu na masuala ya kodi kujitokeza kwa wingi ili kuwezesha kufikiwa kwa lengo la utoaji wa huduma kwa wananchi watakaojitokeza.
Pia ametoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kutumia fursa hiyo adhimu kujitokeza kwa wingi katika viwanjwa vya Mnazi Mmoja ili waweze kunufaika na huduma ya Dawati la Mhasibu kwa kukutana na wataalamu mbalimbali watakaowafundisha mambo mbalimbali.
Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) ni chama cha kitaaluma kilichoanzishwa mwaka 1983 kwa ajili ya kuendeleza taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu Tanzania. Tanzania.
Mwenyekiti wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) Dkt. Fred Msemwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma ya Dawati la Mhasibu itakayofanyika tarehe 07 Oktoba 2017 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Chama hicho Dyoya James Dyoya na Afisa Mtendaji Mkuu wa TAA Bw. Patrice Sigungu.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) Dyoya James Dyoya (kushoto) akielezea jambo mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu huduma ya Dawati la Mhasibu itakayofanyika tarehe 07 Oktoba 2017 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo. Kutoka kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa TAA Bw. Patrice Sigungu na Mweneyekiti wa chama hicho Dkt. Fred Msemwa.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mkutano baina yao na viongozi wa Chama cha Wahasibu Tanzania (TAA) leo jijini Dar es Salaam.
Picha na: Idara ya Habari – MAELEZO
No comments:
Post a Comment