Katika kuelekea kumbukumbu ya miaka Kumi na Minane ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Kituo cha Uhuru FM kupitia Kampeni yake ya Gusa Maisha Yao, kimefanikiwa Kugusa Maisha ya baadhi ya Watanzania wenye uhitaji kwa kutoa misaada ya Vyakula na vitu mbalimbali.
Tangu kuanza kwa Kampeni ya Gusa Maisha Yao, Kituo cha Uhuru FM kimetembelea Vituo vyenye uhitaji wa Faraja, ambapo kimetoa msaada wa vitu vikiwemo Vyakula katika Kituo cha Watoto Yatima-Chakuwama, na Kituo cha Tumaini la Maisha cha Watoto wenye Maradhi ya Saratani kilichopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Misaada hiyo iliyotolewa na Wasikilizaji pamoja na wadau mbalimbali imepelekwa pia katika Kituo cha Vijana walioathirika na Dawa za Kulevya, Soba House kilichopo Kigamboni jijini Dar es salaam.
Kesho, Alhamis, Wafanyakazi wa Uhuru FM, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali watajitolea kutoa Damu katika zoezi litakalofanyika kwenye Viwanja vya Jengo la CCM, Mkoa wa Dar es salaam, Tandika Sokoni, pamoja na Kiwanda cha Nguo Urafiki.
Kilele cha Kampeni ya Gusa Maisha Yao awamu ya kwanza kitafanyika Jumamosi hii katika Viwanja vya MwembeYanga, Temeke, jijini Dar es salaam kwa kuhusisha Tamasha la Michezo na Burudani ya Muziki kutoka kwa Wasanii mbalimbali nchini kuanzia Majira ya Asubuhi hadi Jioni.
No comments:
Post a Comment