Na Salum Vuai, MAELEZO
USHINDI wa kwanza kwa upande wa wanawake na wanaume kwenye mbio za kilomita 10 katika mashindano yaliyoandaliwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), zote zimechukuliwa na wakimbiaji kutoka Tanzania Bara.
Katika michuano hiyo iliyofanyika leo ikianzia makao makuu ya KMKM Kibweni mnamo saa 1:10 asubuhi, na kumalizikia viwanja vya Maisara mjini Zanzibar, Dickson Marwa kutoka Musoma aliibuka wa kwanza upande wa wanaume baada ya kukimbia kwa dakika 29:52:02.
Nafasi ya pili ilikwenda kwa Mkenya Lameck Mwakio aliyetimka kwa dakika 29:52:07, akifuatiwa na Nelson Mbuya aliyepeperusha bendera ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU), ambaye pumzi zake zilimuwezesha kukimbia kwa dakika 29:59:07.
Kwa matokeo hayo washindi hao walizawadiwa medali za dhahabu, fedha na shaba mtawalia.
Mwanadada Sarah Ramadhan kutoka Arusha alifanikiwa kunyakua medali ya dhahabu baada ya kuwatupa wafukuza upepo wenzake kwa dakika 37:18:25, huku Sharo Myryuti (Kenya) akishika nafasi ya pili akikimbia kwa dakika 37:38:43 na kuondoka na medali ya fedha.
Mwanariadha mzoefu wa michuano ya kimataifa Zakia Mohammed Mrisho kutoka Arusha, aliambulia namba tatu akifikisha muda wa dakika 38:43:45 na kutia mikononi medali ya shaba.
Mbali na mfukuzano huo mkuu, pia mashindano hayo yalipambwa kwa mbio za kushajiisha, ambapo mwanariadha mstaafu Faida Salmin kutoka Mkwajuni aliibuka kidedea kwa upande wa wazee wanawake kwenye kilomita mbili, huku Othman Aziz wa Jang’ombe akiwafunika wazee wenzake kwa upande wa wanaume.
Aidha resi kwa wakimbiaji wenye ulemavu wanawake, ziliwashuhudia wasichana kutoka Amani waking’ara kwa kushika nafasi zote tatu za kwanza, ambao kwa mpangilio ni Hadaa Khatib Simai, Amina Daud na Fatma Said.
Wakimbiaji wenye ulemavu wanaume, mshindi wa kwanza alikuwa Wahid Abdalla Abdalla (Jang’ombe), akifuatiwa na Ali Bora Msheza na Khamis Ali (wote kutoka Mkwajuni).
Wengine wenye ulemavu walioshinda kwenye patashika hizo ni Shukuru Khalfan (Dar es Salaam), Haji Ali Haji (Amani) pamoja na Yaina Hussein (Mwembeladu) ambao waliungana na washindi wengine kupokea zawadi mbalimbali walizokabidhiwa na viongozi tafauti akiwemo mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud.
Halikadhalika kulikuwa na michuano ya kuvuta kamba pamoja na kufukuza kuku iliyoshirikisha wachezaji wanawake na wanaume.
Michuano hiyo ya tatu kuandaliwa na KMKM, mbali na mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mjini Ayoub Mohammed Mahmoud, pia ilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utalii, Utalii na Michezo Rashid Ali Juma pamoja na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Moudline Castico.
Viongozi wengine ni Mshauri wa Rais Michezo na Utamaduni Chimbeni Kheri, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Sadalla ‘Mabodi’, Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Amour Hamil Bakari, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania Filbert Bayi, makamanda wa vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama na wadau wengine wa michezo.
Naibu Mkuu wa KMKM Kapteni Khamis Simba Khamis (suruali nyekundu) akianzisha mbio za Kilomita 10 (KMKM 10 Km Race) zilizoanzia Makao Makuu ya Kikosi hicho Kibweni na kumalizia viwanja vya Maisra Mjini Zanzibar.
Washiriki wa mbio za kilomita 10 zinazoandaliwa na KMKM wakianza kukimbiza kupitia mitaa mbali mbali ya Zanzibar baada ya kuzinduliwa na Naibu Mkuu wa Kikosi hicho Capteni Khamis Simba Khamis.
Washindanaji wa mbio za kilomita 10 wakipita katika mzunguko wa eneo la Kariakoo Mjini Zanzibar wakielekea viwanja vya Maisara ambapo ndio mwisho wa mbio hizo.
Mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 10 mwaka 2017 Dickson Marwa kutoka Dar es Salam akimaliza mbio hizo katika viwanja vya Maisara kwa kutumia dakika 29:52.02 akifuatiwa na Lamek Mwakio kutoka Kenya alietumia dakika 29:52.07. Mshindi wa tatu ni Nelson Prya.
Mshindi wa kwanza kwa upande wa wanawake Sara Ramadhani Makera kutoka Arusha akimaliza mbio hizo kwa kutumia dakika 37:18.25, Mshindi wa pili wanawake alikuwa Sharo Myryuti kutoka Kenya alitumia dakika 37:38.43 .
Mchezo wa kufukuza kuku ulikuwa miongoni mwa burudani iliyovutia watu wengi katika viwanja vya Maisara. Wapiganaji wa KMKM wakishindana kukimbiza kuku na kwamjibu wa sharia za mchezo huo atakaemkamata inakuwa ni zawadi yake.
Wapiganaji wa kike wa KMKM wakishiriki katika mchezo wa kuvuta kamba ambapo timu ya Kamandi Kaskazini walibuka washindi wa kwanza.
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayoub Mohd Mahmoud wa nne kutoka kushoto (waliokaa) akiwa na viongozi wengine mbali mbali wakifuatilia michezo iliyokuwa ikiendelea katika viwanja vya Maisra.
Fainali ya mchezo wa kuvuta kamba wanaume ambao uliwashirikisha wapiganaji wa KMKM Kamandi ya Kaskazini wakipambana na wapiganaji Kikosi cha Rada Masingi ambapo Masingini waliibuka washindi .
Katibu wa Klabu ya michezo ya KMKM Luteni Sheha Mohammed Ali akisoma risala ya mbio za kilomita 10 kwa mgeni rasmi katika viwanja vya Maisara.
No comments:
Post a Comment