Tuesday, October 17, 2017

SERIKALI YAWATAKA WADAU WA SEKTA YA AFYA YA BINADAMU, MIFUGO, WANYAMA PORI NA MAZINGIRA KUONGEZA KASI YA USHIRIKIANO NA MASHAURIANO

Mmoja wa washiriki wa warsha ya wadau wa sekta ya afya, mifugo, mazingira na wanyama pori kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar akichangia mada wakati wa warsha ya kujadili Mpango Mkakati wa Usalama wa Afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko itokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu iliyofanyika Jumatatu Oktoba 16, 2017.
Mwakilishi wa Shirika la DTRA kutoka nchini Marekani Bi. Jean Richard akizungumza na wadau wa sekta ya afya, mifugo, mazingira na wanyama pori wakati wa warsha ya kujadili Mpango Mkakati wa Usalama wa Afya (2017-21) katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko itokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu iliyofanyika Jumatatu Oktoba 16, 2017.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mbazi Msuya (wa pili kushoto)akifuatilia hotuba zilizokuwa zikitolewa na wadau mbalimbali wa warsha wadau wa sekta ya afya, mifugo, mazingira na wanyama pori iliyokuwa ikijadili Mpango Mkakati wa Usalama wa Afya (2017-21) katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko itokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu iliyofanyika Jumatatu Oktoba 16, 2017. Wa pili kulia ni Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Ritha Njau.
Mwakilishi wa Shirika la OIE katika nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Bw. Moetapele Letshwenyo akizungumza na wadau wa sekta ya afya, mifugo, mazingira na wanyama pori wakati wa warsha ya kujadili Mpango Mkakati wa Usalama wa Afya (2017-21) katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko itokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu iliyofanyika Jumatatu Oktoba 16, 2017.
Baadhi ya washiriki wa warsha ya kujadili Mpango Mkakati wa Usalama wa Afya (2017-21) katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko itokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu wakifuatilia hotuba za Viongozi mbalimbali wakati wa uzinduzi wa warsha hiyo iliyofanyika Jumatatu Oktoba 16, 2017 Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mbazi Msuya akizungumza na wadau wa sekta ya afya, mifugo, mazingira na wanyama pori wakati wa warsha ya kujadili Mpango Mkakati wa Usalama wa Afya (2017-21) katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko itokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu iliyofanyika Jumatatu Oktoba 16, 2017.
WashirIki wa warsha ya kujadili Mpango Mkakati wa Usalama wa Afya (2017-21) katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko itokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mbazi Msuya mara baada ya kuzindua warsha hiyo Oktoba 16, 2017 Jijini Dar es Salaam.

Na Ismail Ngayonga, MAELEZO.

SERIKALI imewataka wadau wa sekta za afya ya binadamu, mifugo, wanyama pori na mazingira kuongeza kasi ya ushirikiano na mashauriano ya pamoja ili kutekeleza vyema Mpango kazi wa usalama wa afya unaolenga kudhibiti magonjwa yaambukizwayo na wanyama kwenda kwa biandamu.

Hayo yalisemwa jana (juzi) Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu wa Maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mbazi Msuya wakati wa uzinduzi wa warsha ya wadau za sekta za afya, mifugo, mazingira na wanyama pori waliyojadili Mpango kazi wa Usalama wa Afya (2017-20) kupitia dhana ya Afya Moja.

Mbazi alisema  magonjwa yaambukizwayo na wanyama kwenda kwa wanadamu yanachukua takribani asilimi 60-75 ya magonjwa yote ya wanadamu, sambamba na kuleta athari kubwa kiuchumi, kiafya na kimaendeleo katika ngazi zote,hivyo wadau wa afya hawana budi kutafuta mbinu mbadala za namna ya kuyadhibiti na kuyatokomeza.

“Magonjwa ya kichaa cha mbwa, ugonjwa wa malale, kimeta, home ya bonde la ufa na mengineyo yameleta vifo kwa wanyama na wanadamu na hata ulemavu katika nyanja mbalimbali hivyo ni wajibu wetu wataalamu wa afya tuyapatie pamoja na kupata ufumbuzi wa kudumu kwa magonjwa haya” alisema Mbazi.

Aliongeza kuwa Tanzania imeridhia na kutekeleza agenda ya usalama wa afya duniani mwaka 2014, hivyo katika kuweka msisitizo wa agenda hiyo, suala la afya moja limepewa mkazo katika Nyanja mbalimbali ili kuweza kujiandaa na kujikinga na madhara yatokanayo na matishio mbalimbali ikiwemo magonjwa ya milipuko ya binadamu na wanyama.

Akifafanua zaidi Mbazi alisema kupitia dhana ya afya moja, Serikali imeweka malengo ya kuhakikisha kuwa sekta za afya ya binadamu, mifugo, wanyama pori na mazingira zinashirikiana kudhibiti athari za magonjwa kama msingi mkuu wa kulinda afya ya binadamu na wanyama.

Aliongeza kuwa hadi sasa Tanzania inaendelea kuwa miongoni mwa nchi chache zilizopiga hatua nzuri katika kujipnaga na kuboresha mahusiano ya sekta za afya, mifugo na utalii, na hivyo aliwataka wadau wa warsha hiyo kubaini changamoto zilizopo ikiwemo kuboresha miundio iliyopo katika kukabiliana na majanga ili iweze kuwa na manufaa zaidi.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Ritha Njau aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa uamuzi wa kuwakutanisha wadau wa sekta za afya, mifugo, mazingira na wanyama pori kuwa ni hatua nzuri katika kukabiliana na tishio la magonjwa ya milipuko yatokayo kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Aliongeza kuwa Mpango wa Serikali kuanzisha dhana ya Afya moja ni hatua mojawapo inayodhirisha dhamira ya Tanzania katika kukabiliana na vimelea vya magonjwa ya milipuko ya wanyama, juhudi ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimekuwa zikiungwa mkono na WHO pamoja na mashirika na taasisi mbalimbali ya afya duniani.

“Mwaka 2005 WHO ilianzisha kanuni maalum kwa nchi wanachama kuonyesha juhudi mbalimbali ilizonazo katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko itokanayo na wanyama na kuainisha vyanzo na asili ya magonjwa hayo” alisema Dkt Njau.


Naye Mkurugenzi wa Msaidizi wa Kitengo cha Udhibiti wa Magonjwa wa milipuko katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Dkt. Janeth Mghamba alisema kupitia Mpango kazi huo, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa madhara ya magonjwa ya wanyama kwenda kwa binadamu yanatokomezwa nchini.

No comments: