Monday, October 30, 2017

SERIKALI YATENGA MILIONI 700 ZA MAJI MIRERANI

Serikali imetenga shilingi milioni 700 milioni kwa ajili ya kuanzisha mradi wa maji kwenye Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara utakaopunguza kero ya maji kwenye eneo hilo.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji Isack Kamwelwe ameyasema hayo kwenye ziara yake ya siku moja Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara. Waziri Kamwelwe alisema radi huo wa maji utasababisha asilimia 85 ya wananchi wa mji huo kupata maji ya uhakika.

Alisema mradi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa kwani fedha za mradi huo zimeshatengwa tayari. limuagiza meneja wa mamlaka ya maji safi Babati (Bawasa) mhandisi Idd Msuya kuhakikisha mradi huo wa Mirerani unaanza na kukamilika ndani ya muda wa miezi sita.

"Baada ya Rais John Magufuli kufanya ziara yake hivi karibuni kwenye mji mdogo wa Mirerani alitoa ahadi ya kupatiwa maji wananchi wa eneo hilo hivyo nikiwa Waziri mwenye dhamana hiyo amehakikisha agizo hilo limetekelezwa," alisema Waziri Kamwelwe. Alisema baada ya Rais Magufuli kuagiza maji ya uhakika yapatikane Mirerani na zoezi la ujenzi wa ukuta wa kuzunguka machimbo ya Tanzanite kuanza, yeye kama Waziri aliamua ashughulikie suala la maji Mirerani.

Kwa upande wake, meneja wa Bawasa, mhandisi Idd Msuya alitoa ahadi kwa Waziri kuwa watasimamia ipasavyo mradi huo wa maji na kuhakikisha unaanza ndani ya muda wa miezi sita. Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula alimshukuru Waziri Kamwelwe kwa kuitembelea kwa mara ya pili Simanjiro na kuahidi neema ya maji kwenye miji ya Mirerani, Orkesumet na kijiji cha Naisinyai.

Chaula alisema wilaya hiyo ina vipaumbele vitatu vya elimu, afya na maji, hivyo ziara hiyi imekuwa na manufaa makubwa kwao kwani kipaumbele chao kimojawapo cha maji kitapatiwa ufumbuzi. "Umekuwa Waziri mchapakazi tangu ukiwa Naibu wa Wizara hii na kila tukikupigia simu juu ya mradi wa maji wa kutoka mto Ruvu hadi Orkesumet ulikuwa unatupa ushirikiano wa kutosha," alisema mhandisi Chaula.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Jackson Sipitieck akimshukuru Rais Magufuli kumpandisha cheo Waziri Kamwelwe kuwa Waziri kamili wa Wizara hiyo, ambaye awali alikuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo.

Sipitieck alisema Waziri Kamwelwe ni mchapakazi mahiri kwani hii ni mara yake ya pili kufika wilayani Simanjiro kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji. Alimshukuru Waziri Kamwelwe kwa kufuatilia ipasavyo mradi mkubwa wa maji kutoka mto Ruvu hadi Orkesumet kwani utasaidia wananchi na mifugo kupata maji ya uhakika.

"Pia tunashukuru kwa kukubali ombi letu la kututengea fedha kwa ajili ya ujenzi wa eneo la bwawa la Langai linalotegemewa na wafugaji wa kata tatu za Langai, Loiborsoit na Naberera ambalo lilipasuka na kusababisha maji kupungua ghafla na kukauka," alisema Sipitieck.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro Zuwena Omary alisema wananchi wa eneo hilo wanategemea vyanzo mbalimbali vya matumizi ya maji ikiwemo mto, mabwawa, chemchem, mifereji na visima vifupi na virefu. 
Waziri wa Maji na Umwagiliaji mhandisi Isack Kamwelwe akizungumza juu ya utekelezaji wa miradi mitatu ya maji kwenye Wilaya ya Simanjiro Mkoani  Manyara, (kushoto) ni Mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Zephania Chaula na kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Jackson Leskar Sipitieck. 

 Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro Zuwena Omary akisoma taarifa ya Wilaya hiyo kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji mhandisi Isack Kamwelwe. 
 Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula akimshukuru Waziri wa Maji na Umwagiliaji mhandisi Isack Kamwelwe kwa  utekelezaji wake wa miradi ya maji Simanjiro. 

No comments: