Tuesday, October 31, 2017

Serikali Yamshukia Zitto kwa Upotoshaji.

Na.Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Serikali imetoa onyo kali kwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mh. Zitto Kabwe juu ya taarifa za upotoshaji wa takwimu za Pato la Taifa alizozitoa hivi karibuni.

Taarifa hizo za Mh. Zitto zimeripoti kuwa ukuaji wa Pato la Taifa kwa robo ya pili ya mwaka 2017 kuwa ni asilimia 5.7 badala ya asilimia 7.8. Kasi ya ukuaji ya asilimia 5.7 ilikuwa ni kwa robo ya kwanza ya Januari hadi Machi 2017.

Onyo hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Bw. Daniel Masolwa Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa kutoka Ofisi ya Taifa za Takwimu (NBS),kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NBS,pamoja na  Mkurugenzi wa Sera na Tafiti za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw.Johnson Nyella wakati wakizungumza na Waandishi wa Habari.

Masolwa amesema kuwa upotoshaji huo uliofanywa na Mh. Zitto ni wa makusudi na unalenga kuonesha kuwa juhudi znazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano hazina manufaa kwa Wananchi.

“Napenda kukanusha kauli ya Mh. Zitto kuhusu taarifa zake zinazodai kuwa takwimu za Pato la Taifa zimepikwa, Mh. Zitto anatakiwa kujua kwamba kazi ya kukokotoa takwimu za Pato la Taifa ni ya kitaalam na inafuata miongozo inayotolewa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Takwimu na Shirika la Fedha Duniani (IMF)”,alisema Masolwa.

Ameongeza kuwa miongozo hiyo ni pamoja na mifumo ya pato la Taifa ya mwaka 2003 na 2008 na mwongozo wa kuainisha shughuli za kiuchumi Toleo la Nne ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka  2016 Tanzania imekuwa nchi ya pili kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara kwa utoaji, uchambuzi, usimamizi na usambazaji wa takwimu  kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Aidha Bw.Masolwa ametoa wito kwa taasisi yoyote ile au mtu binafsi anayetaka kutayarisha takwimu rasmi  kwa ajili ya kutunga sera na kupanga mipango ya maendeleo kupata maelezo ya kina kuhusu ukokotoaji na miongozo mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Tafiti za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania, Johnson Nyella amesema kuwa Mh. Zitto amekokotoa ukuaji wa Pato la Taifa anaodai kuwa ni sahihi kwa kuangalia tofauti kati ya ongezeko la ujazi wa fedha na mfumuko wa bei jambo ambalo sio sahihi kulitumia kama kipimo.

“Ukokotoaji wa aina hiyo umejengwa juu ya nadharia inayoitwa ‘quantity theory of money’ ambayo inasema mfumuko wa bei hutokea pale fedha zinapoongezeka kwa kasi zaidi kuliko uzalishaji wa vitu halisi ambayo si sahihi kutumia nadharia hiyo kuelezea mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi katika kipindi cha muda mfupi kama Mh. Zitto alivyofanya,” alifafanua Bw.Nyella.

Wawakilishi hao wa Benki Kuu na Ofisi ya Taifa ya Takwimu wamelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya taarifa za Ukuaji wa Pato la taifa kutolewa na Mh.Zito, na wakawaasa Wananchi na wanasiasa kuacha kupotosha takwimu za serikali na kuziomba mamlaka husika kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kupotosha umma kwa makusudi.
Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa toka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Daniel Masolwa (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo ichani) wakati akikanusha taarifa za upotoshaji kuhusu takwimu za pato la taifa mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Mkurugenzi wa Sera na Tafiti toka Benki Kuu Johnson Nyella
Mkurugenzi wa Sera na Tafiti toka Benki Kuu Johnson Nyella (kushoto)akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo ichani) wakati akikanusha taarifa za upotoshaji kuhusu takwimu za pato lataifa mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Meneja wa Takwimu za Pato la Taifa toka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Daniel Masolwa.

Picha na Eliphace Marwa – Maelezo. 

No comments: