Abrahamu Too kutoka Kenya ameibuka mshindi wa
kwanza kwenye mbio za km 42 Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza jana
baada ya kumaliza kwa muda wa saa 02:22:45, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki
mwenzake kutoka nchini humo Moris Motima aliyetumia muda wa saa 02:23:19
Kivutio katika mbio hizo
ilikuwa ni Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Bi Juliana Shonza ambae
mbali na kuzindua mbio hizo pia alishiriki katika mbio za km 3 akiambatana na
viongozi wengine wa serikali.
Nafasi ya tatu katika mbio
hizo pia ilichukuliwa Mkenya George Onyacha aliyetumia muda wa saa 02:23:27,
ikiwa sekunde chache nyuma ya mpinzani wake.
Katika mbio hizo zilizoanzia
na kuhitimishwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini humo ilishuhudiwa nafasi ya kwanza
hadi ya saba zikishikwa na wakimbiaji kutoka nchini Kenya huku nafasi ya nane
ikienda kwa Mtanzania Paschal Mombo alietumia muda wa saa 02:30:43.
Akizungumzia siri ya ushindi
wake, mbali na kusifia uratibu mzuri wa mbio hizo uliomuwezesha kukimbia bila
changamoto yoyote Too alisema ni kujituma kufanya zaidi mazoezi na kukaa
kambini muda mrefu ili kufanya vizuri katika michuano ya mwaka huu.
“Maandalizi ya mwaka huu ni
mazuri na washiriki wameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka jambo linalotufanya
wanariadha kujiwekea mikakati mizuri ili kuweza kukabiliana na ushindani mkali
uliopo katika mbio hizi na ninashukuru Mungu nimefanikiwa,” alisema.
Upande wa wanawake mshindi wa
kwanza ni Mkenya Alice Gradys Otero aliyetumia muda wa saa 02:48:18 akifuatiwa
na Mkenya mwenzie Tecla Chebet aliyetumia saa 02:54:28 huku nafasi
ya tatu ikishikwa na Mkenya Flavious Kwamboka alietumia muda wa saa 02:57:32.
Mtanzania Brabuelia Bryton
kutoka mkoani Moshi alishika nafasi ya sita kwa upande wa wanawake katika mbio
hizo akitumia saa 03:14:41
Washindi wa kwanza katika mbio
hizo zilizofanyika kwa mara ya nane jijini humo waliibuka na kitita
cha Sh 4 milioni kila mmoja, washindi wa pili Sh 2 mil na washindi watatu Sh
Mil 1.
Kwa upande wa mbio za km 21 Peter
Limo kutoka Kenya aliibuka mshindi wa kwanza baada ya kumaliza kwa muda wa saa
01:05:24, akifuatiwa kwa karibu na mshiriki mwenzake kutoka nchini humo George
Wayaki aliyetumia muda wa saa 01:05:50
Nafasi ya tatu katika mbio
hizo pia ilichukuliwa Mtanzania Chacha Boy aliyetumia muda wa saa 01:05:59,
ikiwa sekunde tisa tu nyuma ya mpinzani wake.
Upande wa wanawake mshindi wa
kwanza ni Mkenya Dorifin Omare aliyetumia muda wa saa 01:17:12 akifuatiwa na
Mkenya mwenzie Alice Mogiare aliyetumia saa 01:18:30 huku nafasi ya tatu
ikishikwa na Mkenya Maiselina Issa alietumia muda wa saa 01:19:55.
Mtanzania Siatha Romanus
kutoka mkoani Arusha alishika nafasi ya sita kwa upande wa wanawake katika mbio
hizo akitumia saa 01:25:58
Katika mashindano hayo
ilishuhudiwa washiriki ambao pia ni wadhamini wa mbio hizo kutoka makampuni ya PUMA, Tiper, NSSF, RedBull,
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), New Mwanza Hotel, EF Out door, CF
Hospital, KK Security, na kampuni ya uchapishaji ya SDS wakishiriki kikamilifu
katika mbio za KM 5 sambamba na watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino.
Akizungumza kabla ya kukabidhi
zawadi kwa washindi, Naibu Waziri Shonza alisema aliwapongeza washiriki na waandaaji
wa mbio hizo na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana kwa pamoja ili
kurejesha hadhi ya mchezo wa riadha nchini.
“Tanzania inaweza kurejea
katika ramani ya dunia kwenye michezo kama tukijikita katika maandalizi mazuri
ya kuibua na kuviendeleza vipaji vya vijana wetu nchini hasa kuanzia ngazi ya
shule za msingi.” Alisema.
Naye Rais wa Shirikisho la
riadha nchini (RT) ambae pia ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu Bw Anthony Mtaka
mbali mbali na kuwapongeza waandaaji wa
mbio hizo alisema licha ya wingi wa washiriki kutoka ndani ya nchi bado taifa
linakabiliwa na uhaba wa wanaridha wa mbio ndefu yaani km 42 na wachache
wanaofanya vizuri kwenye mbio hizo wamekuwa wakishindwa kushiriki mbio kama
hizo zinazofanyika ndani ya nchini.
Abrahamu Too kutoka Kenya
akimaliza katika nafasi ya kwanza kwenye mbio za km 42 Rock City Marathon zilizofanyika
jijini Mwanza jana baada ya kumaliza kwa muda wa saa 02:22:45, akifuatiwa kwa
karibu na mshiriki mwenzake kutoka nchini humo Moris Motima aliyetumia muda wa
saa 02:23:19.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa
na Michezo, Bi Juliana Shonza akizungumza na waandishi wa habari kabla ya
kuzindua mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jijini Mwanza jana ambapo alikimbia mbio za km 3 akiambatana na
viongozi wengine wa serikali.
Baada ya uzinduzi kazi
ikaanza!
Mbali na kuzindua mbio hizo
pia Naibu Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Bi Juliana Shonza (wa pili
kulia)alishiriki kikamilifu katika mbio mbio za km 3 akiambatana na viongozi
wengine wa serikali.
Mbali na washiriki kutoka
ndani ya nchin pia pia washiriki kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo China na
Marekani nao hawakuwa nyuma.
Rais wa Shirikisho la riadha
nchini (RT) ambae pia ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu Bw Anthony Mtaka akizungumza
kwenye warsha ya kukabidhi zawadi kwa washindi ambapo pamoja na mambo mengine
aliwapongeza waandaaji wa mbio hizo kampuni ya Capital Plus Internantional
(CPI).
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa
na Michezo, Bi Juliana Shonza ( katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na
washindi wa kwanza hadi wa tatu wa mbio za Km 42 (waliosimama nyuma) mara baada
ya kuwakabidhi zawadi pamoja na medali. Wengine ni pamoja na Rais wa Shirikisho
la riadha nchini (RT) ambae pia ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu Bw Anthony Mtaka(wa
tatu kushoto), waandaaji pamoja na viongozi wa mchezo huo.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa
na Michezo, Bi Juliana Shonza (Kushoto) akikabidhi zawadi kwa washindi wa mbio
za Km 42 kwa upande wa wanawake ambapo washindi wa kwanza hadi watano wote
walitoka nchini Kenya.
Naibu Waziri wa Habari, Sanaa
na Michezo, Bi Juliana Shonza (Kushoto) akikabidhi zawadi kwa washindi wa mbio
za Km 5 ambazo zilikuwa mahususi kwa washiriki wenye ulemavu wa ngozi pamoja na
washiriki kutoka kwenye mashirika mbalimbali (corporate race)
Meneja Mahusiano Mkuu wa
Kampuni ya kuhifadhi mafuta nchini Tiper, Bw Emanuel Kondi (kulia)
akikabidhi zawadi kwa mmoja wa washindi wa mbio hizo. Kampuni ya Tiper ni moja
ya wadhamini wakubwa wa mbio hizo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo
kuisaidia Serikali kutangaza utalii kupitia michezo pamoja na kuinua ya michezo
kupitia riadha.
Baadhi ya washindi wa mbio
hizo, waandaaji na viongozi wa mchezo wa Riadha wakiwa kwenye picha ya pamoja
na Meneja Huduma kwa wateja Kanda ya Ziwa kutoka kampuni ya ndege ya Precision Air, Bi Isabella
Mwalwiba mara baada ya kukabidhiwa zawadi zao. Kampuni ya Precision ni miongoni
mwa wadhamini wakubwa wa mbio hizo.
Baadhi ya washindi wa mbio
hizo wakipokea zawadi zao kutoka kwa muwakilishi wa kampuni ya CF Hospital ya
jijini Mwanza.zawadi zao. CF Hospital ni miongoni mwa wadhamini wa mbio hizo.
Baadhi ya washindi wa mbio
hizo, waandaaji na viongozi wa mchezo wa Riadha wakiwa kwenye picha ya pamoja
na Meneja Kanda wa kampuni ya Ulinzi ya KK Security, Bi Levina
Vedasto mara baada ya kukabidhiwa zawadi
zao. Kampuni ya KK Security ni miongoni mwa wadhamini wakubwa wa mbio hizo
ambapo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waliwahakikishia washiriki uwepo wa ulinzi
na Usalama.
Baadhi ya washiriki kutoka
ndani na nje ya nchi wakifurahia medali zao!
Baada ya ushindi ilikuwa ni
furaha tupu!
No comments:
Post a Comment