Friday, October 27, 2017

NAIBU WAZIRI ATIMUA WANANCHI WALIOVAMIA HIFADHI YA KATAVI, AAGIZA WATUMISHI WALIOPIMA VIWANJA NDANI YA ENEO LA HIFADHI WACHUKULIWE HATUA ZA KISHERIA


Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kushoto) akipokea taarifa ya Serikali ya Mkoa wa Katavi kutoka kwa Mkuu wa Mkoa huo Mej. Jen. Mst. Rafael Muhuga baada ya kusomwa mbele yake jana alipotembelea mkoa huo kwa ajili ya kutatua migogoro ya hifadhi na wananchi.

NA HAMZA TEMBA -WMU-KATAVI
..............................................................
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, amewataka  wananchi wa Kitongoji cha Situbwike ambao wamevamia Hifadhi ya Taifa ya Katavi na kuanzisha shughuli za kibinadamu kinyume cha sheria waondoke kwa hiari ndani ya wiki mbili zijazo kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Naibu Waziri Hasunga amesema hayo jana katika Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi baada ya kutembelea kitongoji hicho chenye kaya zaidi ya 82 ndani ya hifadhi hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutatua migogoro kwenye maeneo ya hifadhi nchini.

"Naagiza, mamlaka husika muhakikishe wananchi hawa wanahama ndani ya wiki mbili zijazo, lazima sheria ziheshimiwe, ifikapo tarehe 10 Novemba, hatutaki tukute mtu hapa, atakayekaidi kitakachompata asitulaumu" aliagiza Naibu Waziri Hasunga.

Kwa upande wa wananchi wa kitongoji hicho ambao wamevamia hifadhi hiyo na kuanzisha shughuli za kilimo, makazi na ufugaji walikiri kuwa wapo ndani ya hifadhi na kwamba walipewa eneo hilo bila ya wao kujua na uongozi wa kijiji cha Stalike ambao kwa sasa haupo madarakani.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga alisema Serikali ya Wilaya hiyo ilitoa notisi ya siku 30 kwa wananchi hao waondoke jambo ambalo halijatekelezwa huku taarifa zikieleza kuwa baadhi yao wamekaidi kuondoka kwa madai kuwa mpaka waone polisi ndio watakusanya virago vyao.

Wakati huo huo, Naibu Waziri Hasunga ameuagiza uongozi wa TANAPA kuendelea na zoezi la uwekaji wa vigingi vya mpaka katika eneo hilo la hifadhi lenye mgogoro ikiwa ni pamoja na kupima umbali wa mita 500 kutoka kwenye mpaka huo na kuweka mabango yanayoonyesha kuwa eneo hilo haliruhusiwi kwa shughuli za kibinadamu kwa mujibu wa sheria.

Katika hatua nyingine, amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Mwailwa Pangani kuwatafuta maafisa ardhi waliohusika kuwapimia wananchi wa kitongoji cha Mgolokani eneo la makazi ndani ya hifadhi ya msitu wa Msanginya kinyume cha sheria.

"Nakuagiza Mkurugenzi wa halmashauri, wale wote waliopima eneo hili ndani ya hifadhi hii watafutwe wahojiwe, labda walikuwa na sababu, wakikutwa na makosa wachukuliwe hatua stahiki za kisheria, hawa wanapaswa kuwajibika" alisema Naibu Waziri Hasunga.

Aidha, alimuagiza mkurugenzi huyo kutafuta maeneo kwa ajili ya kuwagawia wananchi waliondolewa katika hifadhi hiyo ya msitu pamoja na wale walioondolewa hifadhi ya taifa ya Katavi waweze kuanzisha makazi mapya, kilimo na ufugaji.

Mwisho alitoa wito kwa watumishi wa Serikali, taasisi na mamlaka zote za Serikali kufanya kazi kwa ushirikiano kuepuka migogoro isiyo ya lazima inayosababishwa na mkanganyiko wa maamuzji baina ya viongozi wa Serikali.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mej. Jen. Mst. Rafael Muhuga (kulia) alipotembelea mkoa huo jana kwa ajili ya kutatua migogoro ya hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga akizungumza katika kikao na Mkuu wa Mkoa wa Katavi alipotembelea mkoa huo jana kwa ajili ya kutatua migogoro ya hifadhi.
Picha ya pamoja ya Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (wa pili kulia), Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mej. Jen. Mst. Rafael Muhuga, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Katavi na viongozi wa watumishi wa TANAPA,TFS na TAWA. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kushoto) akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mej. Jen. Mst. Rafael Muhuga (kulia) baada ya mazungumzo mafupi ofisini kwake alipotembelea mkoa huo jana kwa ajili ya kutatua migogoro ya hifadhi.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (kulia) akikagua eneo lililovamiwa na wananchi wa Kitongoji cha Situbwike na kuanzisha makazi na shughuli za kilimo na ufugaji ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi,  aliagiza wananchi hao kuondoka kwa hiari ndani ya siku 14 kabla ya kuondolewa kwa nguvu alipotembelea hifadhi hiyo jana mkoani Katavi. Kushoto ni Diwani wa Kata ya Stalike, Adam Chala.
Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (wa nne kushoto) akikagua moja ya kigingi cha mpaka kilichovunjwa na wananchi wa Kitongoji cha Situbwike ambao wamevamia Hifadhi ya Taifa ya Katavi na kuanzisha makazi na shughuli za kilimo na ufugaji, aliagiza wananchi hao kuondoka kwa hiari ndani ya siku 14 kabla ya kuondolewa kwa nguvu alipotembelea hifadhi hiyo jana mkoani Katavi. Kulia na Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Martin Loibooki.
Baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Situbwike ambao wamevamia hifadhi ya Taifa ya Katavi na kuanzisha makazi na shughuli za kilimo na ufugaji kinyume cha sheria wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga (hayupo pichani) wakati akiwapa maelekezo ya kuondoka hifadhini hapo kwa hiari ndani siku 14 zijazo kabla ya kuondolewa kwa nguvu alipotembelea hifadhi hiyo jana mkoani Katavi.

Baadhi ya nyumba za makazi zilizojengwa ndani ya hifadhi ya Taifa ya Katavi kinyume cha sheria. Akiwa Mkoani Katavi jana, Naibu Waziri wa Maliasili, Japhet Hasunga ameagiza wananchi waliovamia hifadhi hiyo wahamishe makazi yao kwa hiari ndani ya wiki mbili zijazo kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

No comments: