Tuesday, October 31, 2017

KWANDIKWA: ACHENI VITENDO VYA HUJUMA MIRADI YA UJENZI

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma wakati akikagua mashine ya kucharangia mawe kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha lami, mkoani Kigoma.
Mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation Zhu Wan Li akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa (wa tatu kushoto), kuhusu maendeleo ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha lami, mkoani Kigoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa akisikiliza maelezo ya Mhandisi Mkazi anayesimamia mradi wa ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha lami kutoka Kampuni ya DOCH Limited, Eng Mekbib Tesfaye, wakati akikagua ujenzi wake, mkoani Kigoma.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kidahwe-Kasulu yenye urefu wa KM 63 inayojengwa kwa kiwango cha lami, ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 52, mkoani Kigoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elias Kwandikwa, akisikiliza maelezo kutoka kwa Eng. Raphael Ndimbo (kushoto), katika chumba cha maabara ya mkandarasi wakati alipokuwa akikagua ujenzi wa wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha lami, mkoani Kigoma.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Elias Kwandikwa (Mb), amewataka wananchi wanaopata nafasi za kazi katika miradi ya ujenzi wa barabara kuwa wazalendo katika kulinda vifaa na kuepuka vitendo vya hujuma vinavyoweza kujitokeza ili kuhakikisha miradi hiyo inaenda kwa kasi na kumalizika kwa muda uliopangwa.

Mhe. Kwandikwa ametoa kauli hiyo wilayani Kasulu mkoani Kigoma, alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 inayojengwa na mkandarasi wa Kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation na kuelezwa kuwa kuna wizi wa mafuta kiasi cha lita elfu 23 zilizoibiwa hivi karibun ambapo amewataka wananchi kuwa na uzalendo kwanza katika miradi yote ya ujenzi katika maeneo yote.

“Wizi wa namna hii haukubaliki na mtandao ni mkubwa hivyo naagiza vyombo vya usalama vichukue hatua kali mapema ili kuweza kuondoa madhara makubwa zaidi”, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Amewataka makandarasi na wasimamizi wa miradi kutoa elimu kwa waajiriwa kila siku kabla ya kuanza kazi kukemea tabia za wizi na ubadhilifu wowote utakaowezea kutokea kwani ni moja ya sababu za miradi pia kuchelewa na gharama kuongezeka.

Kuhusu suala la ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha lami Mhe. Kwandikwa, ameridhishwa na kasi ya ujenzi ya mkandarasi huyo ambapo mpaka sasa maendeleo ya mradi umefikia asilimia 52.

Ameongeza kuwa mkandarasi aendelee kushirikiana na wananchi wa maeneo hayo kwa kuwatengenezea barabara nzuri ya mbadala hasa kipindi hiki cha mvua ili iweze kutumika kwa urahisi na kufanya wananchi kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo.

Aidha, Mhe. Kwandikwa, amesisitiza kuwa nia ya Serikali ni kufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami kwakuwa ni kiungo kikuu kwa nchi za Congo DRC, Burundi na Rwanda na mkoa wenye uzalishaji mkubwa katika sekta ya uvuvi, kilimo, madini na utalii.

Naibu Waziri Mhe. Kwandikwa ametoa wito kwa madereva wote nchini kuzingatia upakiaji wa mizigo kulingana na sheria na utaratibu waliopewa ili kuweza kuzilinda barabara zetu nchini zinazojenga kwa fedha nyingi.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kigoma Eng. Narcis Choma, amesema mradi wa ujenzi wa barabara hiyo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 60 ambazo zote ni fedha za ndani na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwakani.

Ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu KM 63 kwa kiwango cha lami ukikamilika utafungua fursa za ajira na uchumi na hivyo kuunganisha vizuri mkoa huo na mikoa mingine ya nchi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments: