Wednesday, October 25, 2017

KESI YA LULU: USHAHIDI WA MUSHUMBUS WASOMWA MAHAKAMANI

Na Karama Kenyunko, Glogu ya Jamii.


MAHAKAMA Kuu Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kwa kushirikiana na wazee wa baraza wa mahakama hiyo kesho wanatarajia kutoa muhtasari wa kesi ya mauaji ya bila kukusudia inayomkabili msanii wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu anayedaiwa kumuua msanii mwenzake marehemu Steven Kanumba.

Jaji Sam Rumanyika amesema kuwa muhtasari huo utasaidia wazee wa baraza kupitia shauri hilo na kuamua kama Lulu anahatia ama la. Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wao kwa Stafu Sajenti, E 103  Nyagea (53) kusoma maelezo ya ushahidi ya Josephine Mushumbus ambayo aliyarekodi.

Maelezo hayo yalisomwa baada ya wakili wa utetezi, Peter Kibatala kumueleza Jaji Rumanyika kuwa wanaomba askari huyo ayasome maelezo ya Mshumbus ambaye ni shahidi wao pili kwa sababu yeye ndiye aliyemuandikia na yuko mbali hawezi kupatikana kwa urahisi. 

Akisoma maelezo hayo, amesema kuwa anamfahamu Mushumbus na ndiye aliyeandika maelezo yake ya ushahidi. Amesema kuwa katika maelezo hayo Mushumbus alijitambulisha kuwa ni Daktari, ana miaka (46) Mkazi wa Bunju National Housing na aliyaandika maelezo hayo April 23, 2012.

Akimnukuu Mushumbus, askari huyo alisoma kuwa;MShumbusi alimwambia kuwa yeye ni mmiliki ya clinic ya precious inayotoa tiba mbadala iliyopo katika jengo la Mawasiliano barabara ya Sam Nujoma.

Katika clinik yake alikuwa akitibu wateja wa aina mbali mbali akiwemo marehemu Steven Kanumba ambaye alimfahamu tangia Agosti mwaka 2011 alipofika katika clinic yake hiyo kwa Mara ya kwanza kwa ajili ya kutoa sumu mwilini, na kuanzia hapo akawa na mazoea ya kwenda hapo clinic kwa ajili ya huduma hiyo.

Ameendelea kusoma na kueleza, Kanumba alikuwa akienda pale na alikuwa anapima afya yake kwa kutumia machine kuchunguza mwili wake wote. Amedai katika Maelezo yake Mshumbus alidai kuwa Kanumba aligundulika kuwa na mafuta (cholesteol) na tatizo la moyo ‘Heart attack’ na upungufu wa hewa ya oxygen kwenye ubongo.

Matatizo hayo yalimletea udhaifu wa mwili mfano alikuwa na maumivu makali ya moyo, akili kuchoka mara kwa mara.

Ameeleza kuwa katika maelezo yake alidai, katika matibabu yake  aligundua kuwa Kanumba alikuwa anafanya mazoezi ya kutanua misuli ambapo alimshauri aachane na mazoezi hayo kwa muda sababu mzunguko wake wa damu haukuwa mzuri na ungeweza kumpelekea sababu za kifo au kupooza.

Ili ujue MTU amekufa kwa kupoteza hewa misuli yake hubadilika rangi na kuwa ya bluu.

Aliendelea kusoma , siku chache baada ya ushauri wake huo kwa Kanumba, alisikia kuwa amefariki.

Hata hivyo, aliwahi kunieleza anamaumivu makali yanamuumiza sana moyo lakini hakuniambia ni tatizo gani, aliniomba nimpe ushauri nasaha, lakini sababu siku hiyo nilikuwa na Wateja wengi na muda haukutosha tulipanga tukutane siku nyingine lakini bahati mbaya hakuweza kupata nafasi hiyo kwani nilisikia Kanumba amefariki.

Shahidi Nyangea akadai, baada ya kumaliza kurekodi maelezo ya Mshumbusi, aliyapeleka kwa RCO ambaye alimwambia ampelekee sajenti Ernatus ambaye ndio alikuwa mpelelezi wa kesi

Baada ya kumaliza kusoma maelezo hayo, Hakimu alitoa nafasi kwa upande wa mashtaka kumuhoji maswali shahidi ambapo Kibatala alidai huyo hakuwa shahidi ni msomaji tu wa maelezo ya shahidi ambaye hajapatikana lakini upande wa mashtaka kupitia Wakili Faraja George uliiomba mahakama imtambue askari huyo kama shahidi na sio msomaji maelezo ya Mushumbus.

Hakimu Rumanyika alikubaliana na upande wa mashtaka na kusema kuwa, askari huyo anasimama kama shahidi wa pili wa upande wa utetezi na hana kinga yoyote ya kumfanya asiulizwe maswali, ingawa maswali aliyotakiwa kuulizwa ni yale tu yanayomuhusu yeye siyo mauudhui yaliyoko ndani ya ushahidi

Kutokana na mvutano wa kisheria Jaji Rumanyika alitoa uamuzi ambapo alisema askari huyo atatumbulika kama shahidi.

Kesi hiyo itaendelea kesho.

No comments: