Saturday, October 28, 2017

DKT. SHEIN AONGOZA SHEREHE ZA MIAKA 72 YA UMOJA WA MATAIFA (UN) ZANZIBAR

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa pongezi kwa Umoja wa Mataifa (UN) kwa kuendelea kushirikiana na kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo pamoja na kusaidia changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii katika karne hii ya 21 hapa nchini. 
 Dk. Shein aliyasema hayo katika hafla ya kuadhimisha mika 72 tangu ulipoanzishwa rasmi Umoja wa Mataifa (UN), hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, Mjini Zanzibar ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Umoja huo pamoja na wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Katika hotuba yake, Dk. Shein alisema kuwa Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Mashirika yake ya Maendeleo hapa nchini umeweza kutoa ushirikiano wake mkubwa katika kupambana na umasikini, maradhi, majanga na kusaidia sekta mbali mbali za maendeleo. 

 Alisema kuwa Umoja wa Mataifa (UN) pamoja na taasisi zake umekuwa ukishirikiana vyema na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kutoa mchango wake mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa mipango mbali mbali ya maendeleo katika sekta zote za kiuchumi na kijamii. 

Dk. Shein aliongeza kuwa ni miaka 53 tangu Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kuungana na kuunda Jamhuri ya Watu wa Tanzania mafanikio makubwa yameweza kupatikana kwa maendeleo ya Tanzania na watu wake, ambapo kwa upande wa Zanzibar mafanikio yamepatikana na kuweza kutekeleza mipango yake ya maendeleo ikiwemo Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020, MKUZA III, na Utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2015-2020. 

Aliongeza kuwa kwa mshirikiano ya pamoja mafanikio makubwa yamepatikana katika kutekeleza vizuri Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) tangu yalipowekwa mwaka 2000 hadi ulipomaliza utekelezaji wake mwaka 2015 sambamba na kutekeleza mipango na mikakati iliyowekwa jambo ambalo limewezesha kupiga hatua kubwa katika kuimarisha sekta zote za kiuchumi na kijamii. 

Dk. Shein alieleza kuwa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs) yameweza kuleta mafanikio katika kupambana na umasikini na kusisitiza kuwa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ulioanza baada ya kumalizika utekelezaji Malengo ya Maendeleo ya Milenia mwaka 2015, umeanza vizuri hatua za kupunguza umasikini na uimarishaji wa sekta za jamii hasa elimu, afya na usambazaji wa maji safi na salama. 

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejiweka imara katika Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, Kulinda Haki na Maslahi ya Makundi mbali mbali na Kulinda Mazingira juhudi ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa azma ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kupambana na kuondoa umasikini duniani. 

Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti katika kuyatekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yote 17 ili kuhakikisha kuwa Zanzibar inakwenda sambamba na ajenda zote zilizowekwa katika kuyafikia malengo hayo ifikapo mwaka 2030. 

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha utaratibu wa kutoa vipaumbele katika sekta muhimu za kiuchumi kwa kupitia Mafumo wa “Matokeo kwa Ustawi” yaani “Results for Prosperity” ulioanzioshwa mnamo mwezi Februari, mwaka 2014, ambapo Serikali iliweka vipaumbele katika maeneo matano ambayo ni kwenye Sekta ya Utalii, Kuimarisha Mazingira ya Biashara, kuongeza Ukusanyaji wa Mapato, Elimu na Afya. 

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kueleza kuwa ni miaka 72 tokea kuanzishwa kwa Umoja huo, umoja ambao umeanzishwa kwa madhumuni ya kuwatumikia watu ambao umekuwa ukijatahidi katika kuhakikisha jamii inaishi vizuri, inapata manufaa na manedeleo. 

Alieleza kuwa wananchi wa Tanzania wanafurahishwa sana na jitihada za Umoja wa Mataifa na Ofisi zake zote zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar na kuwapongeza wafanyakazi wa Mashirika ya Umoja huo wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar kwa mashirikiano mazuri wanayotoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi wake. 

Dk. Shein pia, alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar wamefurahi kwa mashirikiano makubwa yaliopo kati ya Zanzibar na Umoja wa Mataifa (UN) na kueleza kuwa kufanya hafla hiyo hapa Zanzibar ni ishara inayoonesha kuwa Zanzibar ni pahala penye amani, umoja na utulivu. 

Nae Mratibu Mkaazi wa Umoja wa Mataifa (UN) na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP) nchini Tanzania Alvaro Rodriguez alitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuyawekea mazingira mazuri Mashirika ya Umoja wa Mataifa na kuweza kutekeleza progmamu zake za maendeleo kwa ufanisi mkubwa. 

Aidha, alitoa pongezi na shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa mawasiliano yake ya moja kwa moja na Mashirika ya umoja huo ishara ambayo inaonesha ushirikiano mzuri uliopo kati ya pande mbili hizo hatua ambayo inawawezesha kujua kutoka kwake vipaumbele vilivyowekwa na Serikali. Mratibu Mkaazi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Umoja wa Mataifa utaendelea kuiunga Mkoa Zanzibar katika kuimarisha na kuendeleza sekta mbali mbali za maendeleo. 

Aidha, Alvaro Rodriguez alitumia fursa hiyo kueleza namna Mashirika ya Umoja huo yalivyochukua juhudi za kila aina kuisaidia Zanzibar katika majanga mbali mbali yaliyotokea yakiwemo maradhi ya kipindupindu, pamoja na kueleza mashirikiano yaliyofanyika katika kupunguza vifo vya akima mama na watoto pamoja na kuimarisha huduma mbali mbali za maendeleo zikiwemo afya, elimu, utamaduni, kilimo, uhifadhi wa Mji Mkongwe, maji safi na salama na sekta nyenginezo. 

Katika hafla hiyo viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walihudhuria wakiwemo Mawaziri, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud pamoja na viongozi wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa wanaofanya kazi zao hapa Zanzibar na Tanzania Bara pamoja na watendaji wao. 

Hafla hiyo pia ilitumbuizwa na kikundi cha taarab cha Tweekle, kinachoongozwa na Bi Maria Hamdani na kutoa burdani murua ikiwemo muziki laini pamoja na kuimba nyimbo za taarab za asili zilizotumbuizwa na waimbaji mahiri akiwepo Profesa Mohammed Bin Ilyas na wengineo. 

Umoja wa Mataifa (UN) ni chombo kinachoendesha ushirikiano baina ya Mataifa, ambao ulianzishwa Oktoba 24, 1945 kuchukua nafasi ya Shirikisho la Mataifa ambapo wakati unaasisiwa ulikuwa na wanachama 51 na hivi sasa una wanachama 193.
 Mabalozi wa nchi mbali mbali waliohudhuria katika sherehe za Umoja wa Mataifa UN kutimiza miaka 72 tokea kuasisiwa kwake zilizofanyika  katika Hoteli ya Serena Mjini Zanzibar mgeni rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barazaa la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barazaa la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein akiteta jambo na Mratibu Mkaazi wa Umoja wa  Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo UNDP Nchini  Tanzania Bw.Alvaro Rodriguez (kulia) wakati wa sherehe za kutimiza miaka 72  ya Umoja wa Mataifa UN, tokea kuasisiwa kwake zilizofanyika jana katika Hoteli ya Serena Mjini Zanzibar

No comments: