Thursday, October 12, 2017

Benki ya TPB kuwajaza fedha wateja kupitia shindano la Western Union

Benki ya TPB imezindua rasmi promosheni ya huduma ya Western Union ambayo itawawezesha watumiaji wa huduma hiyo ya kifedha kushinda fedha, simu za kisasa za mkononi na kompyuta mpakato (laptop). 

Akizungumza jijini jana, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Ukuaji wa Biashara wa Benki ya TPB, Frank Mushi alisema kuwa wameamua kuanzisha shindano hilo kama kuwazawadia wateja wake katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.

Mushi alisema kuwa washindi wanaweza kupata kiasi cha fedha ambacho kitawawezesha kusheherekea sikukuu za mwisho wa mwaka, kulipa kodi ya nyumba na ada za watoto wao kwani watumiaji wawili wa Western Union wanaweza kushinda zawadi hadi kufikia sh Milioni 3.

Alisema kuwa mbali ya benki yao, promosheni hiyo pia itawashirikisha washirika wao kama Shirika la Posta Tanzania (TPC), Benki ya DCB, Benki ya Azania, Benki ya Wakulima ya Kagera, Benki ya Mwanga, Benki ya Amana, Benki ya Uchumi, Benki ya Maendeleo, Benki ya Njombe, Benki ya Mufindi na Benki ya Kilimanjaro.

‘’Promosheni tunayozindua leo ni ya miezi mitatu ambayo itaisha mwezi Januari 2018 na inakusudia kuwashukuru na kujiweka karibu zaidi na wateja wetu ambao wanaitumia huduma hii ya Western Union’’, alisema Frank Mushi.

‘’Kushiriki kwenye promosheni hii, wateja wanatakiwa kutuma au kupokea pesa kupitia tawi lolote la Benki ya TPB na washiriki wake, pindi unapotuma au kupokea pesa kuna kuponi utapewa na wafanyakazi wa benki kwenye tawi husika, utajaza na itakupeleka kushiriki kwenye droo hiyo. Droo ya kwanza itafanyika katikati ya mwezi Novemba 2017 ambayo itatoa washindi awwili na kila mmoja atapata laptop, na washingi watano ambao kila mmoja  atapata simu za kisasa za mkononi,” alisema Mushi.

Alisema kuwa droo ya pili itafanyika katikati ya mwezi Desemba 2017 na ya mwisho itafanyika Januari 2018. Alifafanua kuwa utoaji wa zawadi za washindi utafanyika kwenye tawi husika ambako mteja ametuma au kupokea pesa na kujaza kuponi ya kushiriki kwenye promosheni.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Huduma za Fedha na Uwakala wa shirika la Posta, Rehema Mbunda alisema anakaribisha wateja wote watembelee ofisi za Shirika la Posta kwa ajili ya kupata huduma za Western Union ambazo zitawapeleka moja kwa moja kwenye shindano la droo ya Western Union. 

 Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Ukuaji wa Biashara wa Benki ya TPB,  Frank Mushi (Katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa promosheni ya huduma ya Western Union ambayo itawawezesha watumiaji wa huduma hiyo ya kifedha kushinda fedha, simu za kisasa za mkononi na  kompyuta mpakato (laptop). Kushoto ni Kaimu Meneja wa  Huduma za Fedha na Uwakala wa shirika la Posta,  Rehema Mbunda  na kulia ni Kolimba Tawa wa Benki ya TPB ambaye ni Afisa Mkuu wa Uendeshaji
 Wafanyakazi wa TPB Benki na wafanyakazi wengine wa benki hiyo na wadau kutoka Amana Benki, Azania Benki na Shirika la Posta (TPC) wakionyesha baadhi ya zawadi ambazo washindi wa promotion ya Western Union watashinda.
 Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa benki ya TPB, Kolimba Tawa akizungumza katika uzinduzi wa promosheni ya Western Union. Wengine ni Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Ukuaji wa Biashara wa Benki ya TPB, Frank Mushi (Katikati) na Rehema Mbunda wa Shirika la Posta.
‘Warembo’ wa TPB Benki wakiwa katika pozi mara baada ya kufanikisha uzinduzi wa promosheni maalum ya Western Union ambayo itawazawadia washindi zawadi mbalimbali nono. 

No comments: