Na John Nditi, Ulanga.
KAMPUNI ya TanzGraphite imesema itawajengea nyumba zenye hadhi ya juu kaya za kijiji cha Epanko, wilayani Ulanga , mkoani Morogoro zinazohama kwa kupisha mradi mkubwa wa uchimbaji wa madini ya Kinywe (Graphite) na itahakikisha kuwa, maisha ya watu wanaohama yanabaki kama ilivyokuwa awali ikiwa na kuboreshwa zaidi.
Meneja Mahusiano wa TanzGraphite, Bernard Mihayo , alisema hayo kwenye taarifa ya Kampuni hiyo katika kikao cha tisa cha kikosi kazi kilichokutana Septemba 14, mwaka huu mjini Mahenge , wilayani humo.
Kikao hicho kilichokuwa ni cha kujadili na kupokea mrejesho wa vikao vya wananchi kuhusu mpango wa uhamishaji makazi (RAP) kupisha mradi wa madini ya kinywe wa Epanko kilihudhuriwa na wajumbe wa vitongoji vya Kazimoto, Epanko A, Itatira , Mbera, Epanko B na Luli .
Wawakilishi wengine ni kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro, Ofisi ya madini mkoa , Ofisi ya wilaya ya Ulanga , halmashauri na wadau wengine wa mradi huo.
Madini ya Graphite ‘Kinywe’ kwa sasa yanahitajika kwa wingi duniani kutokana na matumizi ya kutengeneza vitu mbalimbali ikiwemo betri za simu , kompyuta mpakato ‘laptop’ na penseli .
Kwa mujibu wa Meneja Mahusiano wa TanzGraphite , utafiti uliofanywa na Kampuni hiyo umebaini madini hayo yanapatikana kwa wingi na kwa ubora zaidi eneo la Kijiji cha Epanko, wilayani Ulanga, mkoa wa Morogoro.
Alisema ,ndani ya eneo linalohitajika kuendesha mradi , lina kaya zipatazo 320 ambazo nyumba zake zimejengwa zaidi kwenye mabonde ambayo pia yanatumika kwa shughuli za kilimo.
Meneja Mahusiano wa TanzGraphite alisema , kaya nyingine zipatazo 80 zinaishi nje ya eneo la mradi , isipokuwa zinamiliki ardhi na mashamba ndani ya eneo la mradi huo.
Pamoja na hayo alisema, ndani ya eneo la mradi kuna miundombinu ya kijamii kama shule ya msingi, ambayo ndiyo shule pekee iliyopo katika kijiji cha Epanko , Kanisa Katoliki, na jengo la zahanati ya kijiji ambayo bado haijakamilika.
Naye Mwakilishi wa Afisa Madini Mkazi wa mkoa wa Morogoro, Athuman Kwariko alisema , serikali ipo tayari kusimamia sekta ya madini na inajipanga kuanzisha Kamisheni ya Madini.
Alisema , madini ni mali ya wananchi na yanakasimiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa manufaa ya watu wote na kwa hiyo Serikali inasisitiza uwekezaji na kusimamia sekta ya madini na wananchi kuwa tayari kuwapokea wawekezaji kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Kamati ya kikao kazi hicho , Valence Kidumu alisema, pamoja na mipango mizuri iliyowasilishwa na Kampuni katika kikao hicho aliishauri Kampuni iwasilishe taarifa hiyo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kinachotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
“ Taarifa hii tuliyoipokea leo hapa ni nzuri na unaungwa mkono na wajumbe wote , lakini ni vyema Kampuni ikatoe pia kwa Madiwani kwenye kikao cha baraza kinachotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu kwa kupata baraka zao” alisema Kidumu ambaye pia ni Ofisa Ardhi wa wilaya hiyo.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Lucas Mwaisaka , aliwataka viongozi wa serikali ya Kijiji Epanko kuitisha kikao halali utakachoridhia kupitishwa kwa mpango wa uhamishaji wa makazi ili utekelezaji uweze kuanza na Kampuni hiyo.
Awali mkuu wa wilaya ya Ulanga, Jacob Kassema alisema, juhudi kubwa zimefanyika kutoa elimu ya ushirikishwaji wananchi kuhusu miradi mbalimbali ukiwemo wa Epanko ambapo asilimia 82 ya kaya za zimekubali kuthaminiwa kupisha mradi uchimbaji wa madini ya Kinywe.
Kiongozi wa wa kimila wa kabila la Wapogoro wa kijiji cha Epanko , wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro (Mbuyi ), Redemta Masura ( wapili kushoto) akiwa na viongozi wa Kijiji hicho wakipitia taarifa ya mpango wa uhamishaji makazi kupisha mradi wa madini ya Kinywe wa Epanko , wakati wa kikao cha tisa cha Kikosi Kazi iliyowashirikiasha wajumbe wa kutoka vitongozi sita wa kijiji hicho , viongozi kiserikali na kijamii kilichofanyika hivi karibuni mjini Mahenge.
Baadhi ya viongozi wa serikali wa wilaya ya Ulanga na mkoa wa Morogoro wakiungana na vitongoji vya kijiji cha Epanko wakiwemo na wakimila na kijamii kupitia taarifa ya mpango wa uhamishaji makazi kupisha mradi wa madini ya Kinywe wa Epanko katika kikao cha tisa cha Kikosi Kazi cha mpango wa uhamishaji makazi kupisha mradi wa madini ya Kinywe wa Epanko kilichofanyika hivi karibuni mjini Mahenge.
Baadhi ya viongozi wa kamati ya Kikosi kazi kutoka serikali za vitongoji vya kijiji cha Epanko wakiwemo wa kimila na kijamii wilayani Ulanga wakijumuika na wa ngazi ya wilaya hiyo na mkoa wa Morogoro kupitia kwa pamoja taarifa ya mpango wa uhamishaji makazi kupisha mradi wa madini ya Kinywe wa Epanko kilichofanyika hivi karibuni mjini Mahenge.
Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Lucas Mwaisaka (kulia) akimkabidhi Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Epanko, Kata ya Nawenge, wilayani Uanga, Eliza Liwemba, ( kushoto) Mpango wa Uhamishaji Makazi (RAP) wa Mradi wa Madini wa Epanko wakati wa kikao cha tisa cha Kikosi Kazi cha mpango huo kilichowashirikisha wajumbe wa kutoka vitongozi sita wa kijiji hicho , viongozi kiserikali ya wilaya na mkoa ambacho kilifanyika hivi karibuni mjini Mahenge. ( Picha na John Nditi).
No comments:
Post a Comment