Wednesday, September 13, 2017

Tanzania Yawa Mwenyeji wa Mkutano wa 37 wa Madini Afrika

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja ya Mkutano wa MakatibU Wakuu kutoka Nchi Wanachama wa Kituo cha Afrika cha Sayansi ya Jiolojia na Madini (AMGC). Wengine katika picha ni wawakilishi kutoka Nchi wanachama pamoja Makamishna na Wakuu wa Vituo vya Madini. 
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (katikati) baada ya kufugua kikao cha Makatibu Wakuu kutoka Nchi Wanachama wakiwa katika Kituo cha Afrika Sayansi ya Jiolojia na Madini (AMGC). Wengine ni Kamishna wa Madini, Mhandisi Benjamin Mchwampaka (kushoto) na Assa Mwakilembe (kulia).
Baadhi ya wawakilishi wa Bodi ya Kituo cha Afrika cha Sayansi ya Jiolojia na Madini (AMGC), wa kwanza kutoka kulia ni Mwenyekiti wa UNECA, Dkt. Koja Busia, Mwenyekiti wa Bodi, Masresha Gebreselassie, Mwenyekiti wa AUC, Frank Mugyenyi na Mkurugenzi Mkuu wa AMGC, Ibrahim Shaddad.
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe (anayeongea). Wengine ni washiriki katika kikao hicho.
Mshauri Mwelekezi wa AMGC, Timo Gawronski akitoa maelezo kwa washiriki wa kikao wakiwa katika maabara ya uchunguzi wa asili ya madini husika.

…………………..

Tanzania imekuwa Mwenyeji wa Mkutano wa 37 wa Masuala ya Kisera ya Kituo cha Afrika cha Sayansi ya Jiolojia na Madini (African Minerals and Geosciences Center (AMGC) ambao unafanyika jijin Dar es Salaam. 

Awali, mkutano huo ulianza kwa kuwakutanisha Wakurugenzi wa Bodi ya kituo hicho na kufuatiwa na mkutano wa tarehe 13 Agosti, 2017, uliowashirikisha Makatibu Wakuu kutoka nchi Wanachama wa kituo husika.

Akizungumza na Vyombo vya Habari wakati wa Mkutano wa Makatibu Wakuu, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe alisema lengo la kukutana ni kufanya tathmini na kuendeleza yale yaliyopangwa kutekelezwa na nchi wanachama ikiwemo kupanga mipango ya mwaka ujao na bajeti ya utekelezaji wa mipango hiyo.

Profesa Mdoe alisema kuwa yapo mambo ambayo waliyokubaliana katika mkutano wa 36 yakiwemo ujenzi ya Maabara ya kisasa kwa ajili ya nchi za Maziwa Makuu ambayo itasaidia katika shughuli za madini ikiwemo za uchunguzi wa madini, kukiwezesha kituo hicho kufanya shughuli zake vizuri na kusaidia nchi wanachama katika sekta husika.

Akizungumzia manufaa ya kituo hicho nchini, alisema kuwa kituo hicho kimekuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania hususan Taasisi za Vyuo Vikuu nchini ambazo zimekuwa zikikitumia Kituo hicho katika mafunzo mbalimbali.

“Sisi tumepata bahati kubwa ya kuwepo kwa kituo hiki hapa nchini. Tayari vipo Vyuo na wanafunzi ambao wamenufaika na uwepo wa kituo hiki. Kwetu sisi ni faida kwa sababu hatutumii gharama kubwa za kufuata huduma zinazotolewa na kituo hiki tofauti na nchi nyingine ambazo zipo mbali,” alisema Prof. Mdoe.

Aidha, alisema faida nyingine kwa nchi wanachama waliolipa ada kamili ni kupata punguzo la asilimia 40 la kutumia maabara za Kituo hicho.Akizungumzia malengo ya baadaye ya kituo hicho, alieleza kuwa ni kukifanya kuwa kituo bora zaidi ikiwemo kuongeza idadi ya wanachama kutoka nchi nane zilizopo sasa.

Hadi sasa nchi wanachama ni Tanzania, Msumbiji, Sudani Kaskazini, Ethiopia, Uganda, Kenya, Comoro na Angola.Sambamba na mkutano huo, itafanyika pia sherehe ya kuadhimisha miaka 40 ya kituo husika tangu kuanzishwa kwake.