Wednesday, September 13, 2017

Sister Jean Pruitt (17 October 1939–10 September 2017)


Sister Jean Pruitt ni mmoja wa watu walioitumikia Tanzania katika kukuza sana na kutetea haki za mtoto, akiwa amefanya kazi na taasisi ya kidini ya Marekani ijulikanayo kama Maryknoll Sisters na Kanisa Katoliki tangia mwaka 1966 na kutunukiwa tuzo kadhaa kwa mchango wake kwa jamii na utamaduni nchini.

Kumbukumbu zake zinaonesha kwamba Sister Jean alimaliza masomo yake katika shule ya Nativity jijini Los Angeles Marekani mwaka 1953, na baadaye Bishop Conaty High School mwaka 1957. Mwaka uliofuata alijiunga na taasisi ya Maryknoll Sisters jijini Los Angeles, na hadi mwaka 1967 alihitimu shahada ya kwanza ya Elimu Chuo Kikuu cha Mary Rogers jijini New York.  Mwaka 1968 alihitimu mafunzo ya Ustawi wa Jamii Chuo Kikuu cha Buffalo hapo hapo New York. 
Mwaka 1969, Sister Jean aliletwa Tanzania na Maryknoll Sisters kufanya kazi na Kanisa Katoliki, akianza kushughulika na taasisi ya Misaada ya Catholic Relief Services, akishughulika zaidi na maendeleo ya afya ya vijana na watoto wa Tanzania.
Toka awasili nchini miaka hiyo, alianzisha taasisi kadhaa kwa nia ya kusaidia wasanii vijana. Mwaka 1972 alianzisha Kituo cha Utamaduni cha Nyumba ya Sanaa jijini Dar es salaam ambacho kikaja kuwa  mojawapo ya  taasisi mashuhuri alizoanzisha na zilizofanikiwa sana.
Uwanja ilipojengwa Nyumba ya Sanaa hivi sasa ni makao makuu ya benki ya NMB, ambao kwa kutambua umuhimu wake, wametenga sehemu moja kwa ajili ya nyumba ya sanaa. Lakini sio kubwa kama ilivyokuwa yenyewe, kabla ya kuvunjwa, jambo ambalo Sister Jean alililalamikia san asana, hasa ikizingatiwa yeye binafsi aliomba eneo hilo toka kwa Rais wa wakati huo Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. 
Mwaka huo huo alianzisha tawi la Caritas, na mwaka 1988 alikuwa mwanzilishi mwenza wa chama cha Urafiki  wa Tanzania na Msumbiji (TAMOFA), na mwaka 1992 akanzisha kituo cha kulelea watoto wa mitaani cha Dogodogo Centre kukabiliana na ongezeko la watoto hao jijini Dar es salaam. 
Mwaka 2000 Sister Jean akawa Gavana wa mtandano wa
Global Network of Religions for Children|Global Network of Religions for Children - Africa (GNRC-Africa), ambapo alianzisha program kadhaa ikiwemo ya “Elimu kwa ajili ya Amani” iliyofana sana katika kuelimisha watoto na vijana juu ya mtangamano, kuvumiliana na kutatua migogoro. 
Sister Jean pia alikuwa mmoja wa waanzilishi wa taasisi ya The Stepping Stone Trust Fund kusaidia watoto na vijana walio katika maisha magumu nchini Tanzania. 
Katika harakati zake lukuki za kusaidia kukuza sanaa na utamaduni wa Tanzania, hasa hasa baada ya kuanzisha Kituo cha Nyumba ya Sanaa, Sister Jean alivumbua vipaji vingi ambavyo baadaye vikapata umaarufu mkubwa ulimwenguni. Mmoja wa vipaji alivyovumbua ni msanii wa kuchora na kuchonga George Lilanga.
Patrick Francis Imanjama ni msanii mwingine anayejulikana kimataifa akitokea mikononi mwa Sister Jean, akijulikana zaidi kwa uchoraji wa mtindo wa etching na vitabu. Kwa msaada wa mama huyu Imanjama aliweza kufanya maonesho kimataifa nchi kadhaa zikiwemo Ujerumani, Austria na Marekani. 
Wasanii wengine waliovumbuliwa na Sister Jean walikuwa ni Augustion Malaba, Henry Likonde na Edward Kiiza.
Katika kutambua mchango wake mkubwa kwa jamii ya Tanzanioa, Sister Jean alitunukiwa tuzo kadhaa za heshima. Mwaka 1983 alitunukiwa tuzo ya heshima ya Taifa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwa mchango wake katika kuendeleza SIDO. December 17, 2005 alitunukiwa tuzo ya kitaifa ya ZEZE  kwa mchango wake wa kuendeleza sanaa na utamaduni wa Mtanzania. 
Agosti 4, 2013: Rais wa wakati huo Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa kijana Hamisi Mohamed  na wenzake aliyetoka kushinda Ubingwa wa Dunia wa Mchezo wa kuruka kamba huko Orlando, Marekani, Kijana huyo ni moja ya matunda ya kituo cha Dogodogo Centre kilichoanzishwa na Marehemu Sister Jean Pruitt. Angalia video hapo chini.


No comments: