Kaimu
Mkrugenzi Mkuu wa TACAIDS Bw.Jumanne Issango akieleza jambo kwa
waandishi wa habari(hawapo pichani) wakati wa mkutano kuhusu changamoto
na mafanikio katika kupambana na virusi vya ukimwi nchini kulia ni Kaimu
Mkurugenzi Muitiko wa kitaifa wa TACAIDS Bi.Audrey Njelekela mkutano
uliofanyika katika ukumbi wa ofisi za TACAIDS leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Paschal Dotto-MAELEZO)
Na Fatma Salum – MAELEZO
Tume
ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imeendelea kuiasa jamii kuhusu
kubadili tabia ili kuepuka maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwani ugonjwa
huo bado ni janga kwenye nchi yetu.
Hayo
yamesemwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo Bw.Jumanne Issango
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu
mafanikio na changamoto za tume tangu ilipoanza kutekeleza majukumu
yake.
“UKIMWI
bado ni changamoto katika maendeleo ya Taifa letu na umeendelea
kuathiri kila sekta, kila imani, matajiri na masikini nchini kote hivyo
ni wajibu wa kila mmoja kujitathmini mwenendo wake na kuacha tabia
hatarishi ambazo zinachangia kuongeza maambukizi ikiwemo uasherati,
ngono zembe, ulevi na kadhalika,” alisema Issango.
Alieleza
kuwa kwa miaka ya karibuni hali ya maambukizi ya UKIMWI imeendelea
kupungua ingawa kuna tofauti kwenye mikoa, wilaya na makundi ya
kijamii.Issango alibainisha kuwa kiwango cha maambukizi Tanzania Bara ni
asilimia 5.3 na takwimu hizo ni kutokana na Utafiti wa Viashiria vya
UKIMWI mwaka 2012.
Kwa
mujibu wa utafiti huo wanawake walioambukizwa ni asilimia 6.2 na
wanaume ni asilimia 3.8 ambapo idadi ya Watanzania wanaokadiriwa kuishi
na VVU ni zaidi ya milioni 1.5.“Mikoa inayoongoza kuwa na maambukizi
makubwa ni Njombe asilimia 14.8, Mbeya asilimia 9 na mikoa yenye
maambukizi ya chini zaidi ni Manyara asilimia 1.5, Tanga asilimia 2.4 na
Dodoma asilimia 2.9,” alifafanua Issango.
Aidha
alisema kuwa licha ya maambukizi mapya kupungua kwenye jamii bado
kiwango cha maambukizi kwenye makundi maalum kimeendelea
kuongezeka.Akitaja makundi hayo Issango alisema kuwa ni pamoja na
madereva wa magari ya masafa marefu, wachimba madini, wavuvi, wafungwa
na wale wanaofanya biashara ya ngono.
Kwa
upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Muitikio wa Kitaifa kutoka Tume
hiyo Bi. Audrey Njelekela alisema Serikali kupitia TACAIDS inaendelea
kufanya jitihada mbalimbali za kukabiliana na janga hilo ikiwemo kuandaa
na kutekeleza mikakati madhubuti itakayosaidia kupunguza maambukizi kwa
kiasi kikubwa.
“Mkakati
wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2013/14 – 2017/18 unalenga ifikapo
2018 kiwango cha maambukizi kishuke kufikia asilimia 0.16
ikilinganishwa na mwaka 2012 ambapo utafiti unaonesha maambukizi ni
asilimia 0.32,” alisema Njelekela.
Alitaja
hatua nyingine zinazochukuliwa na tume hiyo ni pamoja na kuendelea
kutoa elimu kwa umma hasa kwa vijana, wanawake wajawazito na makundi
maalum ikiwemo kujenga Vituo vya Maarifa vinavyotoa huduma za VVU/UKIMWI
kwa madereva wa magari ya masafa marefu.
Aliongeza
kuwa juhudu za Serikali kutoa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya
UKIMWI (ARVs) zimesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo
ambapo kwa sasa wanaotumia dawa hizo ni zaidi ya watu laki 8.
Pia
Serikali imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa Shughuli za Kudhibiti UKIMWI
kwa ajili ya kusaidia kununua dawa, kutoa elimu ya UKIMWI, kupima,
kufanya tafiti na kutoa elimu ya uzazi kwa vijana.
TACAIDS
ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 22 ya mwaka 2001 kwa lengo la kutoa
uongozi wa kimkakati, uratibu na kuimarisha juhudi za wadau wote
wanaojishughulisha na kudhibiti UKIMWI nchini.
No comments:
Post a Comment