Thursday, September 21, 2017

TAASISI YA TACC YATOA MAFUNZO KWA VIJANA WAJASIRIAMALI WILAYANI KIABAHA YA KUWAJENGEA UWEZO KATIKA KUPAMBANA NA SOKO LA AJIRA

NA VICTOR MASANGU, KIBAHA .

VIJANA wajasiriamali zaidi ya 50 kutoka Wilayani Kibaha Mkoa Pwani wamepatiwa mafunzo kwa lengo la kuweza kujifunza stadi mbali mbali za maisha pamoja na namna ya kuweza kujiajiri wao wenyewe kupitia biashara ndogo ndogo wanazozifanya ili kuweza kupambana na wimbi la umasikini na  kujikwamua kiuchumi kwa lengo la kuweza kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo.

Mafunzo hayo ya vijana ambayo yanafanyika mjini Kibaha kwa muda wa siku 14 yameandaliwa na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya ushindani na biashara Tanzania  (TECC) kwa kushirikiana na wadau  mbali mbali wa maendeleo kwa lengo la kuweza kuwawezesha vijana hao  ili waweze kupambana na changamoto inayowakabili kwa sasa ya upatikanaji wa soko la  ajira.

Akizungumza katika uzinduzi wa programu  hiyo ya kuwasaidia vijana wajasiliamari Mkurugenzi mtendaji wa  Taasisi hiyo ya TECC Sosthenes Sambua amesema kwamba lengo lao kubwa ni kuhakikisha kwamba inawakomboa vijana hao kwa kuwajengea uwezo wa kuweza kujikwamua kimaisha.

Naye Meneja wa Shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Pwani Agnes Yesaya amesema lengo lao kubwa ni kuhakikisha inatoa mafunzo zaidi kwa vijana waliopo katika vikundi mbali mbali pamoja na kuwapatia mikopo pamoja na kuwajengea uwezo kwa ajili ya kuanzisha viwanda vidogo ambayo itaweza kuwapa fursa ya kujiendeleza zaidi katika  kukuza mitaji yao.

“Sisi kama sido Mkoa wa Pwani lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba tunawasaidia vijana katika kuwapatia mafunzo mbali mbali ya ujasiriamali pamoja na stadi za maisha kwa lengo la kuweza kupambana na ajira, hivyo tunatarajia baada ya mafunzo haya yataweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa vijana wetu ikiwemo kupambana na wimbi la umasikini.,”alisema Yesaya.

Kwa upande wake Afisa vijana  halmashauri ya mji Kibaha  Mwanaishamu Nassoro amebainisha kuwa mafunzo hayo ana imani yataweza kuwa ni mkombozi mkubwa kwa vijana hao kutokana na  hapo awali walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya soko la upatikanaji wa  ajira hivyo kuwapa wakati mgumu katika kujikwamua kimaisha.

Kadhalika aliongeza kuwa mikakati waliyojiwekea halmashauri ya mji kibaha katika kuwasaidia vijana wajasiriamali ni kuhakikisha asilimia tano iliyotegwa kwa ajili yao inawanufaisha kwa kuwapatia mikopo mbali mbali ambayo itaweza kuwasaidia kujiendeleza zaidi katika kufanya biashara zao na kukuza mitaji yao.

Nao baadhi ya vijana ambao wameshiriki katika mafunzo hayo akiwemo Hussen Peter  na Eveline Ndunguru  walisema kuwa baaada ya mafunzo hayo wataweza kutumia ujuzi walioupata katika kujiajiri wao wenywe ili kuweza kujiendesha wenywe kimaisha bila ya kuwa tegemezi.

TAASISI hiyo ya TECC hadi sasa imeshatoa mafunzo mbali mbali ya kuwawezesha vijana wajasiliamali kutoka  baadhi ya mikoa mbali mbali hapa nchini  zaidi ya 1200 ambao wamefundisha mbinu mbali mbali ambazo zitaweza kuwasaidia katika kujiajiri wao wenyewe pamoja na kujenga viwanda vidogovidogo.

 Meneja wa shirika la kuhudumia viwanda vidogo vidogo (SIDO) Mkoa wa Pwani Agnes Yesaya akizungumza jambo mara baada ya uzinduzi wa progamu ya kuwasaidia mafunzo mbali mbali  vijana wajasiriamali zaidi ya 50  kutoka Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani (PICHA NA VICTOR MASANGU)
 Mkurugenzi mtendaji wa  Taasisi  ya TECC, Sosthenes Sambua ambao ndio waandaaji wa mafunzo hayo ya vijana akizungumzia kuhusina na mikakati ya kuwawezesha vijana hao  ili waweze kutimiza ndoto zao mara baada ya kupatiwa ujuzi katika mafunzo hayo.
 Baadhi ya washiriki katika mafunzo hayo wakiwa wametulia kwa ajili ya kusikiliza mafunzo ya ujasiliamali.


Mmoja wa vijana wajasiriamali akizungumza na baadhi ya wenzake katika mafunzo hayo kuhusina na jinsi alivyoweza kupata fursa ya kuweza kujiajiri yeye mwenyewe na kupitia mafunzo aliyoyapata hayo awali.(PICHA ZOTE NA VICTOR MASANGU)

No comments: