Tuesday, September 5, 2017

RC MTAKA APIGA MARUFUKU USHURU WA BIASHARA NDOGONDOGO MAARUFU KAMA MATANDIKO

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Kata ya Dutwa(hawapo pichani) Wilayani Bariadi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Igaganulwa wakati wa ziara yake aliyofanya kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe.Festo Kiswaga akizungumza na wananchi wa Kata ya Dutwa (hawapo pichani)katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Igaganulwa wakati wa ziara Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka aliyofanya Wilayani humo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Diwani wa Kata ya Dutwa Wilayani Bariadi, Mhe.Mapolu Nunde Mkingwa akizungumza na wananchi wa Kata hiyo (hawapo pichani)katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Igaganulwa wakati wa ziara Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka aliyofanya Wilayani humo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Igaganulwa Kata ya Dutwa (hawapo pichani) Wilayani Bariadi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Kijijini hapo wakati wa ziara yake aliyofanya kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Diwani wa Kata ya Sapiwi, Mhe. James Kibuga Wilayani Bariadi akizungumza na wananchi wa Kata ya Dutwa (hawapo pichani)katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Igaganulwa wakati wa ziara Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka aliyofanya Wilayani humo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi akifafanua jambo katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Igaganulwa wakati wa ziara Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka aliyofanya Wilayani humo kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

……………………………..

Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amepiga marufuku Halmashauri zote Mkoani humo kutoza ushuru wa biashara ndogondogo zinazofanywa na wananchi kwa kutandika na kupanga bidhaa zao chini au kuuzwa katika mabeseni maarufu kama matandiko.



Mtaka ametoa agizo hilo baada ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Igaganulwa, Mhe.Nhandi Masaka Kachala na baadhi ya wananchi kutoa malalamiko yao kuhusu ushuru huo, wakati wa ziara yake wilayani Bariadi yenye lengo la kusikiliza kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi .



Amesema suala hilo lilishatolewa maelekezo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli, hivyo Halmashauri zinapaswa kubuni vyanzo vipya vya mapato vyenye tija kwa Halmashauri na wananchi badala ya kutegemea kutoza ushuru unaowakwaza wananchi.



“Kama kuna Halmashauri bado inatoza ushuru wa matandiko wamechelewa sana, kuanzia kesho hamna huo ushuru, kama ninyi mnafikiri mapato ni kutoza tandiko la nyanya, dagaa, mchicha na ninyi kama wakuu wa idara hiki ndicho chanzo mnachokifikiria kichwani hiyo kazi haiwafai, mkatafute kazi nyingine ya kufanya” alisema Mtaka.

“Halmashauri lazima ibuni chanzo cha mapato chenye tija kwenye Halmashauri na watu. Sasa mtu anahangaika na beseni lake la nyanya wewe unamtoza ushuru, umechangia nini, beseni si lako nyanya si zako” alisema Mtaka.

Aidha, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kuhakikisha kuwa inarejesha asilimia Kumi ya mapato yanayokusanywa inayokusanywa kutoka katika vijiji vyote kwenye kila robo mwaka ili Vijiji hivyo viweze kutekeleza mipango ya maendeleo iliyowekwa.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewahamasisha wananchi kuendelea kulima pamba kwa kuwa Serikali imekusudia kujenga kiwanda cha bidhaa ya Afya zitokanazo na zao la pamba mkoani humo na wataalam wanaofanya upembuzi yakinifu wanatarajia kufika Mkoani Simiyu Septemba 20 mwaka huu kuja kuona eneo kitakapojengwa kiwanda.

Amesema wananchi wasikate tamaa kulima pamba kwa sababu ya matatizo ya kihistoria na kuwaeleza kuwa, Serikali ya Mkoa imepanga mikakati madhubuti ya kuirudisha pamba kuwa dhahabu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata mbegu bora, dawa, pembejeo zote na suala la bei ya pamba itaanza kujadiliwa mapema.

Ameongeza kuwa wananchi wasiache kulima mazao jamii ya mikunde hususani choroko na dengu kwa kuwa Serikali inashughulikia suala la upatikanaji wa soko la uhakiki pamoja na kupunguza au kuondoa kabisa madalali katika biashara ya mazao hayo ili wananchi wanufaike kupitia kilimo.

Akitolea ufafanuzi hoja ya Diwani wa Kata ya Ikungulyabashashi Mhe.Bupi Maduhu Litunga ya kupimiwa maeneo, Mkuu wa Mkoa huyo wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bariadi kupitia Idara ya Ardhi, kuitisha mikutano katika Vijiji vyote ambavyo wananchi wanahitaji kupimiwa maeneo na baadae awasilishe mihutasari ya vikao hivyo Ofisini kwake tarehe 13/09/2017.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe.Anthony Mtaka amekamilisha ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi ambapo amesikiliza na kutatua kero za wananchi katika sekta ya Elimu,Afya, Kilimo, Mifugo, Ardhi, Ujenzi, Biashara na Uchumi pamoja na suala la utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) ambazo amezitolea maelekezo na ameahidi kufuatilia utekelezaji wake.

No comments: