Kocha wa makipa wa timu ya Azam Fc, Idd Abubakar (pili kulia) akiwa pamoja makipa wanaounda kikosi cha timu hiyo.
KOCHA wa makipa wa timu ya Azam Fc, Idd Abubakar, amekiri upinzani mkali kwa makipa wake kikosini kwani wana jumla ya makipa wanne kikosini, Mghana Razak Abalora, Mwadini Ally, Benedict Haule na Metacha Mnata aliyepandishwa, wote wakiwa wanaunda kikosi cha timu kubwa kwenye eneo hilo.
Kwa sasa tokea Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ianze Agosti 26 mwaka huu, Abalora ameonekana kuwa chaguo la kwanza, akiwa mpaka sasa hajaruhusu wavu wake kuguswa kwenye mechi zote mbili za mwanzo, Azam FC ikiifunga Ndanda bao 1-0 kabla ya juzi kutoka suluhu na Simba.
Abubakar alisema kuwa upinzani huo ulidhihirika wakati wakiwa kwenye kipindi cha maandalizi ya msimu mpya nchini Uganda, ambapo kila kipa aliyepewa nafasi aliweza kukaa imara langoni.
“Upinzani upo mkubwa sana na isitoshe vilevile baada ya kuziangalia mechi za pre season tulizocheza kila mmoja anataka nafasi, hawa makipa wote wanne wanahitaji kucheza na viwango vya vyote mazoezini na mechi wanazopewa kila mmoja mechi yake ameitendea haki.
“Tulianza mechi ya kwanza na Mwadini (Ally) amecheza vizuri tu tumekuja tumecheza na Razak (Abalora) mechi mbili amecheza vizuri kwa hiyo kiwastani kiujumla kabisa upinzani upo mkubwa sana kwamba hakuna golikipa ambaye amebweteka kwamba hapa amefika katika hii nafasi,” alisema.
Alisema mpaka sasa ndani ya kikosi hicho hakuna kipa ambaye ndiye kila kitu kutokana na ushindani wanaouonyesha na namna kila mmoja alivyopewa nafasi wakati wa maandalizi ya msimu.
“Nadhani hata kwenye hii ligi hali itakuwa hivyo hivyo kwa kuwa kila mmoja yupo kwenye kiwango kizuri kabisa,” alisema.
Kocha huyo wa muda mrefu aliyedumu na Azam FC akiwa kama mchezaji aliyeipandisha timu hiyo hadi kuwa kocha wa eneo hilo, aidha amesema kuwa amepata makipa wachanga wanne ambao anawapika kwa ajili ya manufaa ya baadaye ya timu hiyo huku akikiri kuwa wanavimo vizuri.
“Ukizungumzia kuwaandaa makipa wa chini ambao ni junior (wadogo) yaani tukizungumzia waliochini ya umri wa miaka 20, nina magolikipa wanne kutoka chini hawa magolikipa wanne vilevile wanaushindani kila mmoja amekuja kwa staili yake.
“Unajua unapomchukua golikipa hasa hawa wa chini ya umri wa miaka 20, wengi wao wanakuwa hawajafundishwa hawajapa mafundisho kabisa yale ya ugolikipa lakini wanakuwa na fikra, sasa ile fikra unaichukua kwa kila mmoja kwa hiyo hivi sasa kila mmoja anauzuri wake,” alisema.
Alisema makipa hao wamewatoa kwenye programu zao mbalimbali za kusaka vipaji, akiwataja ambao ni Razak, Eliya, Mohamed na Abdulkarim.
No comments:
Post a Comment